CHAMA CHA DEMOKRASIA NA
MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
SALAAM ZA RAMBIRAMBI
MSIBA WA EDSON KAMUKARA
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa kifo
cha aliyekuwa mmoja wa waandishi wa habari mahiri na mhariri wa gazeti la
mtandaoni, Mwanahalisi Online, Edson Kamukara, kilichotokea ghafla jana jioni
katika mazingira yanayodaiwa kuwa ni ajali ya moto.
Kumwelezea Edson
Kamukara ambaye kabla ya kuhamia Mwanahalisi Online linalomilikiwa na Hali Halisi
Publishers, alikuwa Mhariri wa Gazeti la Tanzania Daima, akiwa ametokea Gazeti
la Jambo Leo ambalo alijiunga nalo akitokea Gazeti la Majira, katika nafasi hii
ya salaam za pole yenye ukurasa mmoja, linaweza kuwa jambo gumu sana.
Marehemu
Kamukara alikuwa mmoja wa waandishi makini na mahiri ambao tasnia ya habari
ingeweza kujivunia kuwa nao (wakiwa hai) kwa muda mrefu, hususan katika
changamoto kadhaa ambayo taaluma hiyo adhimu inapitia kwa sasa nchini Tanzania.
Katika
salaam hizi, CHADEMA kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano ambayo kutokana na
majukumu yake ya kila siku ilifanya kazi kwa ukaribu wa kitaaluma na kikazi na
Kamukara, inaweza kutaja sifa nne kati ya nyingi alizokuwa nazo Kamukara;
1. Uthubutu wa kukataa rushwa na
kusimamia maadili ya taaluma.
2. Kupenda kazi yake.
3. Nidhamu ya kazi.
4. Uwezo wa kutimiza majukumu yake
kazini.
Mbali ya
kumsaidia kupata zawadi katika mashindano ya tuzo za umahiri wa uandishi wa
habari, chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), tunaamini sifa hizo pia zilimfanya
Kamukara awe miongoni mwa waandishi vijana walioweza kuaminiwa na kukabidhiwa
majukumu ya uhariri katika vyombo vya habari vikubwa akiwa na umri mdogo, baada
ya kuwa ameandaliwa na kuiva kuchukua nafasi muhimu katika kutimiza uandishi wa
habari unaowajibika kwa umma.
Zinahitajika
kurasa kadhaa kuweza kumwelezea Edson. Kwa masikitiko makubwa CHADEMA kupitia Idara
ya Habari na Mawasiliano, kinatoa salaam za pole na rambirambi kwa familia,
ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na msiba
huu wa Kamukara.
Salaam hizi
za pole pia ziwafikie wafanyakazi wenzake katika Kampuni ya Hali Halisi
Publishers wamiliki wa Gazeti la Mwanahalisi Online kwa kuondokewa na mtumishi
mwenzao ambaye tunaamini hadi mauti yanamkuta si tu walifanya naye kazi lakini
waliishi naye vizuri.
Aidha chama
kinatoa salaam za pole kwa tasnia nzima ya habari nchini hususan kwa waandishi
wa habari kwa kuondokewa na mwandishi mwenzao katika wakati ambao mchango wake
ulikuwa bado ukihitajika katika mapambano ya kitaaluma na kikazi.
Tunaungana pia
katika maombolezo ya msiba huu na wapenzi wote wa kazi za Kamukara ambao wengi
wao hususan baada ya kuwa wamesoma makala yake kwenye Gazeti la Mawio toleo la Alhamis
wiki hii (jana) ambako alikuwa akiandika mara kwa mara, watakuwa bado hatawaki
kuamini kuwa Edson Kamukara katutoka na hatuko naye tena katika ulimwengu huu
wa kimwili.
Wakati
tukimwombea mapumziko ya amani huko aliko Edson Kamukara, tunamwomba Mwenyezi
Mungu awatie nguvu wafiwa wote na kuwajaalia ujasiri wa kuukubali ukweli huu
mchungu na moyo wa subira katika wakazi huu wa majozni mazito.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Imetolewa leo Ijumaa, Juni 26, 2015
na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA ACT WAZALENDO
CHAMA cha Alliance ForChange and Transparance( ACT- Wazalendo.)kinachozingatia msingi wa utu, undugu na uzalendo kwa Taifa,kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwandishi wa Habari Edson Kamukara.
Kutokana na msiba huo Chama kinatoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu jamaa na marafiki,waaandishi wa Habari na wafanyakazi wote wa Halisi Publishers kwa kuondokewa na mtu ambaye mchango wake kwa Taifa ulikuwa unahitajika kwa kiasi kikubwa hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu katika nchi
Tunawaombea kwa mungu wawe na uvumilivu na kuzidi kumuombea marehemu apate pumziko la amani.
Kichama tumempoteza mtu aliyekuwa akituelekeza upungufu wetu kupitia kalamu yake hali iliyotufanya tujirekebishe kila tunapobaini ukweli wa ukosoaji wake.
Tunazidi kumuombea kwa Mungu ampe faraja katika utangulizi wake huu, huku tukiwa na mengi mema ya kujifunza kutoka kwake.
Imetolewa na
Samson Mwigamba
Katibu Mkuu Taifa ACT-Wazalendo
26/06/2015
No comments:
Post a Comment