Saturday, June 13, 2015

MAJAMBAZI WAWILI WAPOTEZA MAISHA KATIKA MAJIBIZANO YA RISASI NA POLISI JIJINI DAR ES SALAAM. BUNDUKI TATU NA RISASI 15 ZAKAMATWA



Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata bunduki tatu katika matukio tofauti jijini Dar esSalaam. Katika tukio la kwanza tarehe 12/06/2015 Polisi walipata taarifa kuwa huko maeneo ya Mbagala Charambe (W) kipolisi Mbagala (M) Kipolisi Temeke kuna majambazi wenye silaha wamepanga kufanya tukio la ujambazi katika kampuni ya FM ABRI TRANSPORTERS iliyopo eneo ka Kurasini jijini Dar es Salaam

Polisi walikwenda kuweka mtego na walipofika eneo la tukio majambazi yalianza kuwafyatulia risasi nao walijibu mapigo na kufanikiwa kuwajeruhi kisha kuwakamata watuhumiwa wawili wenye silaha aina ya MARK IV yenye namba 308139 ikiwa na magazine yenye risasi sita. Bunduki nyingine ni SHORT GUN yenye namba TZCAR 356460 ikiwa na risasi saba ndani ya magazine. Bunduki zote hizi zimekatwa vitako na mitutu.
Aidha, zimekamatwa pikipiki tatu eneo la tukio zenye namba T.769 CJW, MC.423 ASH, na MC.982 ASG pamoja na simu za mkononi zipatazo nane za aina mbalimbali.


Katika hatua ningine, maeneo ya Pori la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkabala na Mawasiliano Towers (W) Kipolisi Oysterbay (M) Kipolisi Kinondoni, askari wakiwa doria walitilia shaka mtu mmoja aliyekuwa pembezoni mwa pori hilo akiwa na pikipiki. Walipomsogelea ili kumhoji,  aliiacha pikipiki na kutokomea porini. Askari waliikagua pikipiki yake namba MC. 406 AKF Boxer rangi nyeusi. Pia waliipekua kwa kina na kufanikiwa kupata Bastola moja nambari 152072 E yenye risasi tano ndani ya magazine ikiwa imefichwa katika kiti (Seat) cha pikipiki hiyo.



MAFANIKIO YA OPARESHENI YA KUPAMBANA NA MAJAMBAZI JIJINI DAR ES SALAAM PAMOJA NA UHALIFU MWINGINE.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na oparesheni kamambe ya kuwasaka na kuwakamata majambazi wa kutumia silaha pamoja na uhalifu mwingine ili kuhakikisha wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanaishi na kufanya shughuli zao za kila siku bila hofu ya uhalifu. Katika oparesheni hiyo iliyoanza tarehe 01/06/2015 Hadi sasa, Jeshi limepata mafanikio yafuatayo:


KUKAMATWA SILAHA AINA YA AK.47 NA RISASI 13
Tarehe 09/06/2015 saa 08:45hrs asubuhi maeneo ya Yombo Relini (W) kipolisi Buguruni (M) wa Kipolisi Ilala polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kukamata silaha aina ya AK47 yenye namba M73B1-130887 ikiwa na magazine yenye risasi 13.
Mafanikio haya yalipatikana baada ya majambazi watatu kumvamia mtu mmoja DHARAMPAL S/O NARALADE, Miaka 32, Mhasibu wa Kampuni ya Mohamed Enterprises mara alipotoka getini katika ghala la kampuni hiyo lililopo Kiwalani Bombom na kisha kumpora begi dogo ndani yake kulikuwa na kompyuta mpakato (laptop).
Baada ya uporaji wananchi walitoa taarifa polisi. Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliyafuatilia majambazi hayo yaliyokuwa na pikipiki mbili zenye namba MC467 AKR Boxer nyekundu na MC274 ASS Boxer nyeusi hadi maeneo ya Kiwalani relini ambako walitelekeza pikipiki hizo. Wananchi wenye hasira kali waliweza kumshambulia jambazi aliyekuwa na silaha kwa mawe na polisi waliweza kuwazuia lakini kwa bahati mbaya majeraha aliyokuwa ameyapata yalisababisha kifo chake.
Majambazi wengine walikimbia kabla hawajakamatwa. Pikipiki zinashikiliwa kituo cha Polisi Buguruni kwa uchunguzi na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Temeke.

KUKAMATWA KWA BASTOLA NA RISASI ZAKE SITA
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata bunduki nyingine aina ya BASTOLA yenye namba za usajili TZCAR 91456 ikiwa na magazine yenye risasi sita ndani yake.
Tukio hili lilitokea tarehe 08/06/2015 majira ya saa nane mchana maeneo ya Tabata Ubaya (W) kipolisi Buguruni (M) Ilala Polisi waliweka mtego kwa lengo la kukamata kundi la vijana baada ya kupokea taarifa kuwa kundi hilo linapanga kwenda kufanya tukio ka uhalifu.
Baada ya askari kanzu kuweka mtego ili kuwanasa vijana hao walistuka na kukikimbi ambapo walidondosha silaha tajwa hapo juu. Uchunguzi  unaendelea ili kujua mmiliki halali wa silaha hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watu hao.


S. N. SIRRO
NAIBU KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

No comments: