Thursday, August 6, 2015

KAMPUNI YA SIMU YA TIGO, HUAWEI WAZINDUA SIMU YA WATU WA HALI YA CHINI JIJINI DAR ES SALAAM LEO

 Meneja wa Vifaa vya Huawei,  Peter Zhang Nchini (kulia), akionesha aina ya simu ya Huawei Y 360 na Y 625 ambazo zina uwezo wa hali ya juu katika matumizi ya nyanja mbalimbali wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi katika uzinduzi wa simu hizo. Kushoto ni Meneja wa Vifaa na Intaneti kutoka Tigo, Mkumbo Myonga.
 Meneja wa Vifaa na Intaneti kutoka Tigo, Mkumbo Myonga, akizungumza katika mkutano huo.
Wanahabri kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa ya uzinduzi huo.
Kampuni ya Tigo Tanzania na kampuni ya kutengeneza simu za mkononi ya Huawei washirikiana kuzindua simu mbili za kisasa,  Huawei Y360 na Y625 ikiwa mwendelezo wa ugunduzi na matumizi katika nyanja ya utandawazi.  
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa simu hizo, Meneja wa vifaa vya Huawei, Peter Zhang, amesema kuwa simu za Huawei Y360 na Y625 zina uwezo wa hali ya juu na zinapatikana kwa bei  nafuu itakayozifanya zipate umaarufu sokoni.  

“Tunafuraha ya kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Tanzania kwa mara nyingine tena tukiamini kuwa uzinduzi huu wa simu za kisasa utaleta mafanikio na mabadiliko makubwa na ya kisasa katika mawasiliano ,” Alisema Zhang. 

“Simu ya Huawei Y360 inapatikana kwa bei nafuu sana ikiwa katika mfumo wa android na kioo cha mbele chenye inchi nne na kuipa sifa kubwa ya matumizi katika mitandao ya kijamii kama vile ‘Facebook’, ‘Instagram’, ‘Twitter’ na ‘WhatsApp’, na halikadhalika, simu ya Huawei Y625 ina kioo cha mbele chenye ukubwa wa inchi tano, na uwezo wa kutumia laini mbili za simu na ikiwa katika mfumo wa android,” aliendelea kusema.  

Akizungumza kwenye  hafla hiyo, Mkuu wa kitengo cha vifaa na intaneti wa Tigo, David Zacharia alisema kuwa, kampuni ya Tigo Tanzania imejitolea katika kuendeleza na kubadilisha maisha ya Watanzania kuwa ya kidigitali, na uzinduzi wa simu mpya za kisasa utaiwezesha jamii kukabiliana na hali ya kiteknolojia inayokuwa kwa kasi na kuufanya ulimwengu wa mawasiliano kuwa kijiji kimoja.  

“Simu Ya Huawei Y360 ni bora na inapatikana kwa bei nafuu katika soko la ushindani ikiwa na uwezo wa kupiga picha kwa kutumia kamera zake za mbele na  nyuma na pia ina uwezo wa kutumia laini mbili za simu kutoka mitandao tofauti huku ile ya Huawei Y625 ikiwa na ubora wa kipekee na kioo  cha mbele chenye ukubwa wa inchi tano.” Alisema Zacharia.

Simu hizi zitapatikana katika maduka ya Tigo kwa bei nafuu, ambapo Huawei Y360  itauzwa kwa Tsh. 160,000 na Huawei Y625 ikiuzwa  kwa Tsh. 295,000. Wateja watafurahia ofa kabambe kama vile kifurushi cha muda wa maongezi cha Tsh 5,000, data/intaneti ya 2GB na muziki bure kwa muda wa miezi sita.    

No comments: