Sunday, August 9, 2015

SHEIKH JALALA--Tukiaminiana tutavuka kwa Amani Uchaguzi Mkuu ujao

Kiongozi mkuu wa kiroho wa waislam Dhehebu la shia Ithnasheriya Tanzania SHEIKH HEMED JALALA akizungumza na baadhi ya wanahabri nje ya semina hiyo waliotaka kujua mambo mbalimbali kuhusu lengo la semina hiyo
 Imeelezwa kuwa kama viongozi wa dini na madhehebu yote nchini Tanzania wataamua kukaa meza moja na kujadili pamoja na kushauriana njia za kuitunza amani ya nchi hususani kipindi hiki kigumu kuelekea uchaguzi mkuu, hakuna mtanzania atakayeanzisha vuguvugu lolote la uvunjifu wa amani kwani itasaidia watanzania kuaminiana kwa kila mmoja na imani yake.

Kauli hiyo imeelezwa leo jijini Dare s salaam na kiongozi mkuu wa kiroho wa waislam dhehebu la shia Ithnasheriya Tanzania SHEIKH HEMED JALALA wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na dhehebu hilo kwa wanahabari na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari semina iliyokuwa na lengo la kujadili kwa kina wajibu wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii.
Amesema kuwa ,kutokuaminia kwa baadhi ya watanzania kumekuwa ndio chanzo kikubwa cha vurugu ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara  huku akitolea mfano utafiti uliowahi kufanyika na kuonyesha kuwa zaidi ya asilimia 78 ya watanzania hawaaminiani ikiwa na maana kuwa katika watanzania 10 ni watanzania 2 tu ndio wanaoaminiana,jambo ambalo amesema lazima viongozi wa dini kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa wanasaidia kurudisha imani kwa watanzania.
Sheikh JALALA amesema kumekuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani nchini Tanzania huku akivitaja kuwa ni pamoja na chuki baina ya waumini wa dini tofauti tofauti ambapo watu wamekuwa wakikashfu dini za wengine,migogoro ya ardhi,mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi,dhuluma na ukandamizaji dhidi ya wanawake,pamoja na migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Kiongozi huyo ameshauri kuwa ili watanzania hususani waumini wa dini mbalimbali kuwa kitu kimoja hasa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu lazima viongozi wa dini zote bila kujali imani zao kuanza kuunda kamati za amani kila mkoa nchini Tanzania wakutane na kuweka mikakati ya kuwaunganisha waumini wao kuwa kitu kimoja.

Akizungumza na wanahabari mbalimbali ambao walipata nafasi ya kuhudhuria semina hiyo amesema kuwa huu ni wakati wa wanahabari kuwa makini na habari wanazotoa kwa watanzania kwani wao ndio wameshikilia amani ya nchi kwa kutumia kalamu zao, hivyo lazima wanahabari wahakikishe kuwa wanatoa habari ambazo zinawaunganisha watanzania na sio kutoa habari ambazo zinaweza kuwagawa watanzania na mwisho kusababisha machafuko yasiyokuwa na faida kwao

Semina hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali,wanataaluma wa habari nchini akiwemo mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam CHARLES KAYOKA, pamoja na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari.

No comments: