Tuesday, August 11, 2015

Taarifa rasmi kuhusu afya ya mh MBOWE kwa sasa



Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema Mhe. Freeman Mbowe ameshauriwa na madaktari apumzike baada ya jana kukimbizwa hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati alipojisikia vibaya ghafla akiwa kwenye msafara wa kumsindikiza mgombea urais wao kuchukua fomu za kugombea urais ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).



Akiongea na waandishi wa habari juu ya afya ya Mhe. Mbowe, Daktari Bingwa Magonjwa ya Moyo, Shem Tulizo Sanga amesema Mhe. Mbowe anaonekana kuchoka sana kufuatia shughuli ambazo amekuwa akizifanya mfululizo hivyo anahitaji kupumzika ili kurejea katika hali yake ya afya ya kawaida.



Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili, anakopatiwa matibabu, mh Mbowe, amesema anaendelea vizuri na kwamba bado anaendelea kupumzika hospitalini hapo, kama alivyopangiwa na madaktari wanaoangalia hali yake.

''Hali yangu imeendelea kuimarika na kilichonipata jana kwa mujibu wa uchunguzi wa madaktari ni uchovu wa muda mrefu, uliobainishwa kutokana na shughuli za muda mrefu bila kupumzika katika shughuli zangu za kisiasa'' amesema Mbowe.

Mh Mbowe ameongeza kwamba, madaktari wamemtaka kuendelea kuwa chini ya uangalizi wao mpaka hapo watakapo mruhusu kuendelea na shughuli zake za kwawaida.

Mmoja kati ya madaktari wanaoangalia afya ya mh Mbowe, Dr Tulizo Sanga(daktari bingwa wa magonjwa ya moyo) ,amewaambia waandishi wa habari hospitalini hapo kwamba, mh Mbowe alipokelewa jana akitokea Hospitali ya Doctors Plaza ya Kinondoni,jijini Dar Es Salaam, kwa ajili ya uangalizi na uchunguzi zaidi kutokana na kuugua ghafla wakati akiwa katika msafara wa mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa.


Nae James Mbatia mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa UKAWA, amefika hospitalini hapo kumjulia hali mh Mbowe, na amesema pamoja na hali ya kuumwa ya mh Mbowe, wao bado wanaendelea kufanya kazi na kwamba ratiba mbalimbali za vikao vya UKAWA ziko palepale, na amewaomba watanzania kuwa watulivu na kuendelea kumuombea mh Mbowe, apone haraka.

No comments: