Tuesday, August 11, 2015

TAIFA STARS YAANZA MAZOEZI



Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimeanza mazoezi katika uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.

Wachezaji wa Taifa Stars chini ya kocha wake mkuu Charles Mkwasa watakua wakijifua mara mbili kwa siku asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume katika kujiweka fit na maandalizi ya mchezo huo.


Kufuatia baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu na timu zao kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 22, Mkwasa amewaongeza wachezji wengine kumi (10) kutoka katika orodha yake ya akiba.

Lengo la kambi hii ya awali ya siku tano, ni kocha mkuu pamoja na benchi lake la ufundi kupata nafasi ya kuwaona wachezaji katika mazoezi hayo kabla ya safari ya kuelekea nchini Uturuki Agosti 23 mwaka huu kwa kambi ya siku kumi.

Wachezaji walioitwa na kuanza mazoezi leo ni Said Mohamed, Vicent Andrew (Mtibwa Sugar), Mohamed Hussein, Ibrajim Hajibu (Simba SC), Hamis Ali, Juma Mbwana (KMKM), Tumba Sued (Coastal Unioni), Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), Ibrahim Hilka (Zimamoto– Zanzibar) na Mohamed Yusuf (Prisons).

Wachezaji wengine waliopo kambini ni Said Ndemla, Hassan Isihaka, Abdi Banda(Simba SC), Rashid Mandawa (Mwadui FC), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Orgeness Mollel (Aspire Academy) na Abdulhaman Mbambi (Mafunzo).


TWIGA STARS KUIVAA HARAMBEE STARLETS
Timu ya Taifa ya  Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini kisiwani Zanzibar, inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Wanawake kutoka Kenya (Harambee Starlets) Agosti 23, 2015.

Mchezo huo wa kirafiki utachezwa katika uwanja wa Aman Kisiwani Zanzibar, ikiwa ni sehmu ya maandalizi ya kikosi hicho kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofayika nchini Congo-Brazzavile kuanzia Septemba 4 – 19, 2015.

Twiga Stars inaendelea na mazoezi kutwa mara mbili katika viwanja vya Aman na Fuoni chini ya kocha wake mkuu Rogasian Kaijage kujiandaa na fainali hizo za michezo ya afrika, wachezaji wote waliopo kambini wapo katika hali nzuri wakiendelea kujifua na michezo ya Afrika.


USAJILI                                                                                         Dirisha la usajili limeongezwa toka tarehe 06 Agosti hadi tarehe 20 Septemba, baada ya muda huo klabu itakayochelewesha kuleta usajili wake itatozwa kiasi cha shilingi laki tano (Tsh 500,000) kwa kila mchezaji itakayemsajili mpaka siku ya tarehe 30 Agosti.
Mwisho wa kufanya uhamisho wa kimataifa wa wachezaji kwa njia ya mtandao TMS ni tarehe 6 Septemba.
Kikao cha kamati ya sheria kitakaa tarehe 28 kwa ajili ya kuupitisha usajili na kitakaa tena tarehe 8/9/2015 kwa ajili ya kupitisha usajili.
Kuanzia tarehe 21 hadi 27 itakuwa ni wiki ya pingamizi, ambapo majina yatabandikwa TFF Karume na kuwekwa kwenye mtandao ili kuwezesha vilabu vyenye pingamizi kuwawekea wachezaji mapingamizi.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza tarehe 12 Septemba 2015, Daraja la kwanza (FDL) ikitarajiwa kuanza Septemba 17 na Ligi Daraja la pili inatarajiwa kuanza Oktoba 16 mwaka huu.


MICHUANO YA COPA COCA-COLA 2015
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bado linaendelea na mazungumzo na wadhamini wa michuano hiyo (Coca-Cola). Kutokana na mazungumzo hayo, ratiba ya michuano hiyo itachelewa kutoka.

Hivyo, tunawaomba kuwa na uvumilivu wakati mchakato wa mazungumzo hayo yanayokaribia ukingoni ukiendelea.



UAMUZI WA KAMATI YA RUFAA YA TFF JUU YA RUFAA YA DR. DEVOTA JOHN MARWA,YA MAAMUZI YA KAMATI YA UCHAGUZI WA SOKA LA WANAWAKE (TFF)

Mwomba rufani, Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiamini kwamba anakidhi vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho.

Maombi hayo yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na wakereketwa wawili wa soka la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za ugombea wa nafasi ya Mwenyekiti.

Waleta mapingamizi walidai kuwa Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.

Aidha Ibara ya 28 (ishirini na nane) kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo miaka 2 (miwili) katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.  Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo na kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya Uchaguzi uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.

Kwa ujumla, sababu za kupinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni iliyojikita juu ya hitilafu katika kuamua kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu katika uongozi wa soka kwa muda ulioainishwa. Sabau nyingine ni kwamba Kamati ya Uchaguzi illibua sababu ambayo haikuwa katika Hati ya pingamizi iliyoletwa na Mleta pingamizi.

 Wakati ambapo Mleta pingamizi alijikita katika kipengele cha 28(3), Kamati iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA kinachomtaka mgombea awe ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho hakikuwemo katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.

Katika kufikia uamuzi wake, Kamati ya Rufani ilizipitia sababu za Mrufani kama zilivyoletwa, na baada ya kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward Augustino, na imeamua kama ifuatavyo. Tutaanza na hoja ya mwisho.

Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua kipengele ambacho hakikuletwa katika hati ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua kipengele hicho endapo kwa kufanya hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema ya maslahi ya suala linalozungumziwa.

Sharti jingine ni kwamba hoja hiyo inyoibuliwa isiwe na athari hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili hata hivyo, hoja iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha 28 (3), imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.

Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu wa miaka 3 hadi 4, bado angekwama kutokana na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa vyovyote ingekuwa ni athari hasi (negative impact) katika harakati za Mrufani. Ni vema

Kamati zinazosikiliza malalamiko zikajikita kwenye malalamiko yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama pigamizi lingekuwa liko juu ya kipengele hicho tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii ya rufani. Hata hivyo, takwa la uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara ya 9 (3), ambayo ilikuwa ni sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya mapingamizi.

Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani haioni kama hoja hiyo ina mashiko. Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa hii ni je, Kamati ya Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa uongozi ulioainishwa na Katiba?

Mrufani ameieleza Kamati ya Rufani mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi katika taaluma. Miongoni mwa shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa kuendeleza soka la wanawake. Mpango huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira Duniani, yaani FIFA.

Maelezo mengine ni kushiriki katika kuongoza timu mbali mbali kule Chuo Kikuu, zingine zikiwa za watoto wadogo ambao baadhi ya matunda yake ni wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon Msuva. Alisema zaidi kuwa alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya FIFA na TFF.

Aidha. Alisema kuwa amekuwa kiongozi tangu akiwa bado kwenye vyuo vya ualimu, na baadaye alipohitimu na kufanya kazi kama Mwalimu, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka sasa. Akasema, hata alipokuwa Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na programu za maendeleo ya soka la wanawake.

Wakili msomi wa TFF akijibu hoja hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha popote kwamba amewahi kuongoza soka, akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi, jambo linaloweza kufanywa na msomi yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya Rufani za Uchaguzi kuitupilia mbali rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.

Tofauti na Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi mapana ya mchezo wa soka katika ujumla wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide interpretation) juu ya sifa zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri finyu (restricted/narrow interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya Uchaguzi.

Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana na Mrufani, Kamati imeona kuwa ana sifa zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa, na vielelezo vyake, Kamati ya Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu mbali mbali sio katika soka tu, bali pamoja na michezo katika ujumla wake.

Tumeshuhudia katika maelezo yake kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua mbali mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa, sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake. Maelezo

yake kuwa aliaandaa programu ya maendeleo ya soka la wanawake, hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi ingeangalia namna ambavyo “visheni” iliyomo katika programu ile ambavyo ingeweza kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo, katika hoja hii, Kamati inakubaliana kuwa Mrufani

anazo sifa stahiki, na kukatwa kwa sababu hii, Kamati ya Uchaguzi haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda rufaa yake? Kamati ya Rufani inachelea kujibu swali hili moja kwa moja. Utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki.  Chini ya Ibara ya 13 (1) cha Kanuni ya
Uchaguzi (Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.

Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo.  Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28 Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni, na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.

Japo katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia. Kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya Uchaguzi.

Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza Mrufani kwa jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa hatokata tama, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la akina mama lililo na changamoto lukuki.

Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: