Saturday, August 15, 2015

Za kimichezo kutoka Tanzania leo



MALINZI AMPONGEZA  NDIKURIYO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Burundi (FBF) Reverien Ndikuriyo kwa kuchaguliwa kuwa spika wa bunge la Seneta nchini humo.

Katika salam hizo za pongezi kwa Rais wa FBF na nakala zake kwenda CECAFA, CAF na FIFA, Malinzi ameelezea imani yake kwa Seneta Ndikuriyo na amemtakia kila la kheri na mafanikio katika nafasi hiyo mpya aliyochaguliwa.

TWIGA STARS YAENDELEA KUJIFUA ZANZIBAR
Kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kilichoweka kambi kisiwani Zanzibar, kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) kimeendelea kujifua kutwa mara mbili katika viwanja wa Aman na Fuoni kabla ya safari ya kuelekea nchini Congo – Brazzavile mwezi ujao.

Twiga Stars chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Starlets) Agosti 23  katika uwanja wa Amani kisiwani Zanzibari ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michezo ya hiyo ya Afrika (All Africa Games).

Kaijage amesema anashukru vijana wake wanafanya mazoezi kwa morali ya hali ya juu, wachezaji wanaonekana kuyashika vizuri mafunzo yake na kumpa imani kuwa sasa kikosi chake kimeiva na anachosubiri ni mchezo wa kirafiki dhidi ya Kenya ili kuweza kuona uwezo wa kikosi chake kabla ya safari ya kuelekea nchini Congo-Brazzavile.

Akiongeleaa maendeleo ya kambi ya Twiga Stars, Mkuu wa Msafara Blassy Kiondo amesema timu ipo katika hali nzuri, wachezaji wanafanya mazoezi  kwa morali ya hali ya juu, hakuna majeruhi kikubwa wanachosubiri kwa sasa ni huo mchezo wa kirafiki dhidi ya Kenya mwishoni mwa wiki ijayo.

TFF YAIRUHUSU  DRFA KUENDELEA NA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA TEFA,KAMA ULIVYOPANGWA KUFANYIKA KESHO.
Shirikisho la mpira wa miguu nchini Tff imekiruhusu chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa chama cha soka wilaya ya Temeke (TEFA) kama ulivyopangwa na kamati ya uchaguzi ya  chama hicho.

Baada ya ruhusa hiyo Uongozi wa DRFA umemuandikia barua katibu wa TEFA Kasim Mustapha ili aijulishe kamati ya uchaguzi ya chama hicho kuendelea na mchakato huo kama kawaida.

Awali TFF iliiandikia barua DRFA kushauri kusimamishwa kwa uchaguzi huo,kutokana na kile kinachoonekana kuwepo na malalamiko kuhusu mchakato wake lakini maada ya mashauriano kati ya pande hizo mbili,sasa ni ruksa kwa uchaguzi huo kufanyika kesho jumapili Agosti 16,2015 kama ulivyopangwa.

Aidha DRFA imewaomba wapiga kura wote kujitokeza kwenye uchaguzi,huku ikisisitiza amani na utulivu itawale katika zoezi hilo muhimu la kuwapata viongozi watakaokiongoza chama cha soka Temeke,ili kuleta maendeleo ya mpira wa miguu mkoa wa Dar es salaam

No comments: