Friday, September 11, 2015

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAAM LAHIMIZA AMANI NA MSHIKAMANO KATIKA MCHAKATO WA UCHAGUZI MKUU WA 25.10.2015




        Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam Suleiman Kova amewakumbusha watanzania hususani wananchi wanaoishi jijini Dar es Salaam kukumbuka wajibu wao wa kudumisha amani wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu.

mchakato huo ni pamoja na wakati wa kampeni, siku ya kupiga kura tarehe 25.10.2015 na baada ya kutangazwa kwa matokeo  mablimbali katika ngazi za udiwani, ubunge na urais.

Kamishna ameyasema hayo katika uwanja wa mpira wa karume jijini dsm alipoenda kukaguwa mazoezi ya pamoja yanayowashirikisha viongozi wa dini mbalimbali wakiwemo Masheikh, Maaskofu, mapadre wachungaji na mabalozi wa nchi mbalimbali.

Mabalozi na wawakilishi wa Nchi zao walioshiriki mazoezi hayo ni pamoja na Ujerumani, Uholanzi, Urusi, na Denmark ambao Kamishna aliwashukuru kwa ushiriki wao ulilenga kudumisha amani ya Tanzania.
Aidha watanzania wamekumbushwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki  

kuelekea uchaguzi mkuu  kwani muda huu ni mfupi sana ukilinganisha  na muda mrefu  ambapo Tanzania imekuwa na amani. Wanatakiwa washirikiane bila kujali itikadi zao au tofauti zozote zile kwa madhumini ya kudumisha amani iliyopo.

Jeshi la Polisi limejiandaa kikamilifu katika kulinda amani na usalama wa Nchi na kutoa onyo kwa wale watu wachache watakaovuruga amani na usalama kwani wakibainika watashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria.

Katika zoezi hilo hapo uwanja wa karume Kamishna Kova alikabidhi mipira mitano kwa Mwenyekiti wa timu ya Amani na mshikamano Sheikh Alhad Mussa Salum ambaye pia ni Sheilk wa Mkoa wa Dar es Salaam akisaidiwa na Mchungaji FUPE -Makamu Mwenyekiti, na Katibu wa timu PADRE JOHN SOLOMONI ili kuwapa hamasa katika kazi yao ya pamoja iliyo nzuri na muhimu kwa taifa hili. Aidha Kamishna alipata fursa ya kupuliza filimbi katikati ya uwanja ikiashiria kuanzisha mazoezi kwa madhumuni ya kuhamasisha amani na mshikamano.

Kamishna Kova amewambia watanzania kupitia shughuli hiyo kwamba katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu "kipaumbele cha kwanza ni  amani cha pili ni amani na cha tatu ni amani"


SULEIMAN H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments: