Friday, October 30, 2015

Janet Mbene Ashukuru wapiga kura na wana CCM kwa kumchagua

MBUNGE mteule katika Jimbo la Ileje mkoani Songwe ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Janet Mbene (CCM) amewashukuru wananchi
wa jimbo hilo kwa kumpa kura za kishindo, madiwani na  Dkt. Jonh
Magufuli anayewania urais.



Akizungumza na wakazi wa Ileje, Mbene alisema ushindi wa kura 27,583
aliopewa na wana Ileje dhidi ya Emmanuel Mbuba wa NCCR Mageuzi
aliyepata kura 14,578 atahakikisha anawapa wananchi hao kupitia
ushirikiano, usimamizi na utatuzi wa changamoto mbalimbali
zinazowakalibi.


“Awali ya yote niwashukuru wana Ileje kwa kuonesha imani kubwa kwangu,
madiwani na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Jonh
Magufuli. Wana Ileje wametupa kura za kishindo nami ninawahaidi
sitawaangusha katika utekelezaji wa ahadi nilizozitoa kwenu wakati wa
kampeni,” alisema Mbene.


Mbunge huyo mteule alisema kuwa, kipaumbele chake cha kwanza  kitakuwa
mindombinu ya barabara na kuwajengea uwezo wajasiriamali  ili
kuzalisha bidhaa bora ikiwemo kuongeza thamani na mauzo.
Mbene alisema, hatua hiyo itasaidia kuondoa umaskini wa kipato na
msisitizo utakuwa kwenye ufugaji wa samaki, kuku, nyuki na mifugo ya
kisasa.


Pia alisema, kilimo nacho atakipa kipaumbele hususani cha alizeti,
kunde, choroko, dengu, mbaazi,  soya , karanga  zikiwemo njugu mawe
kwa wingi  kama mazao ya biashara.


“Nitahakikisha pia kilimo cha nafaka  ambacho kitahusisha mahidi,
mpunga, ulezi , mtama na kilimo cha matunda aina mbalimbali yakiwemo
mananasi , maembe, maparachichi, mapera zikiwemo mbogamboga ili
kuwainua wana Ileje kupitia kilimo chenye tija,” alisema Mbene.


Mbali na hayo alisema, kwa kushirikiana na wananchi ataibua vyanzo vya
asili ambavyo ni vivutio vya watalii wilayani Ileje ili viweze
kuwavutia watalii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya
kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Pia alisema, atahakikisha anashirikiana na wananchi ili kuhakikisha
wanatatua kero mbalimbali katika sekta ya elimu, afya na miundombinu
hatua ambayo itasaidia kuinua vipato vyao, jimbo na taifa kwa ujumla.
********



No comments: