Saturday, November 28, 2015

CHANZO CHA MAJI CHA RUVU CHINI KUWATUA AKINA MAMA NDOO ZA MAJI.

ru1Meneja Mradi Ruvu chini Mhandisi Emmanuel Makasa akiwaonesha waandishi wa habari sehemu ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini kwenda jijini Dar es salaam.
ru2Sehemu ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini kwenda jijini Dar es salaam lilivyozamishwa chini tayari kwa kusafirisha maji ambayo yatawanufaisha wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kwa matumizi mbalimbali.
ru3Baadhi ya mitambo ya kusafisha maji ambayo yamesafishwa tayari kwa matumizi ya wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
ru4Baadhi ya waandishi wa habari na viongozi kutoka Wizara ya Maji wakiwa eneo la chanzo cha maji cha Ruvu Chini.
ru5Fundi akiendelea na kazi ya kuunganisha na kuchomelea bomba la maji ambalo litasafirisha maji kutoka Ruvu Chini kwenda jijini Dar es salaam.
ru6Muonekano wa maji yakiwa mtoni kabla ya kuanza kusafishwa kupitia hatua mbalimbali  kwa matumizi.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
…………………………………………………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ya maji ili kuwanufaisha wakazi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kupata maji kwa mahitaji yao ya kila siku.
Mioundombinu  hiyo inayoboreshwa ni pamoja na bomba la Ruvu Chini lenye urefu wa Jumla ya km 55 ambapo hadi sasa km 52.6 zimekamilika na zimebaki km 2.4 ili kukamilisha  mradi huo ambao utasaidia kusimamia moja ya sentensi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  ya “Kuwatua akina mama ndoo za maji kichwani” 

Ili kufikia azma hiyo ya kuwapatia maji safi na salama wakazi wa mikoa hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo alisema kuwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kabla ya waandishi hao kwenda kujionea hatua iliyofikiwa, Mwang’ingo alisema kuwa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo  Februari 2016 na kuondoa adha ya maji kwa wananchi na kuwaunganishia wengine ambao hawakuwa na huduma ya maji.
“Tumelazimika kufikia hatua ya kupanua huduma ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya Dar es salaa na Pwani kutokana na ongezeko la watu kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2012, mkoa wa Dar es salaam una jumla ya zaidi ya watu milioni 5 ambao watatumia maji zaidi ya lita milioni 5 kwa siku”,

“Katika upanuzi huo, kumekuwa na changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 katika mahakama mbalimbali katika maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi, hadi sasa DAWASA imeshinda kesi 13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo kukamilisha upanuzi wa mradi” alisema Mwang’ingo.
Kwa mujibu wa Mwang’ing’o kesi nne bado zipo mahamani na ambazo zimefikia hatua mbalimbali kulingana na taratibu za kimahakama.
Lengo la mradi huu ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 182 hadi 270 kwa siku. Mradi ambapo awamu itakayofuata ni lita milioni 360 kwa siku.
Chanzo cha maji cha Ruvu Chini ndiyo chenye kiwango kikubwa ambacho kina wapatia maji wakazi wa Dar es salaam kwa zaidi ya asilimia 75 ikilinganishwa na asilimia 25 kutoka Ruvu Juu.

Mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini unalenga kuongeza uzalishaji maji na kuwahudumia wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani
Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo, Vingunguti, Buguruni, Kariakoo na Ilala.

No comments: