Wednesday, November 11, 2015

JESHI LA POLISI LAKAMATA SILAHA 8 NA RISASI 62

Na. Lilian Lundo – Maelezo
Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es salaam imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 7 wakiwa na  silaha 8  na risasi 62 kwenye msako uliofanyika jijini  Dar es salaam katika  kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akiongea na waandishi wa habari leo , katika ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova amesema  wahalifu walidhani kuwa Jeshi la Polisi limeweka nguvu katika uchaguzi mkuu na kusahau kufanya misako yake iliyokuwa ikifanya mara kwa mara kama moja ya majukumu yake.
“Ukweli ni kwamba Jeshi la Polisi lilijipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na misako mingine inaendelea kufanyika kama kawaida kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na mikoa ya jirani” Alisema kamanda Kova.

Kamanda Kova aliongezea kwa kusema kuwa, Jeshi la Polisi kanda maalum inashirikiana na mikoa ya jirani kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao hawapati fursa ya kukwepa mkondo wa sheria.
Aidha alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni SMG moja (1), Bastola sita (6) na Mark 4 riffle moja (1)   na risasi 62 ambapo mpaka sasa jumla ya majambazi 74 wamekamatwa ikiwa ni pamoja na silaha 51 na risasi 890 za silaha mbalimbali
Kamanda Kova amezidi kufafanua kuwa kutakuwa na msako mwingine mkali kuelekea sikukuu za x-mass na mwaka mpya 2016, utakayofanyika katika mikoa ya kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke wakisaidiwa na vikosi maalum vilivyopo Kanda ya Dar es Salaam.
Msako huo utajikita katika kuwakamata majambazi, magaidi, wanaojihusisha na madawa ya kulevya, vibaka, wapiga debe, wanaouza pombe haramu, madanguru yote ambayo pia huhifadhi wahalifu.

No comments: