Friday, December 4, 2015

Mkusanyiko wa Story Tatu kutoka TFF leo


MKUTANO MKUU WA BARAZA LA TPLB
Mkutano Mkuu wa Pili wa Kawaida wa Baraza Kuu (Ordinary Governing Council) la Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Jumapili, Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mkutano wa Kawaida ambao wajumbe wake ni klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza utafanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Uwanja wa Taifa kuanzia saa 4 kamili asubuhi.

Ajenda za Mkutano huo ni Kufungua mkutano, Kuhakiki akidi, Kuthibitisha ajenda, Kuthibitisha Muhtasari wa Mkutano uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya Mwenyekiti, Kupokea Taarifa za Utekelezaji kutoka kwa Wanachama, Kuthibitisha Taarifa ya Utekelezaji ya Kamati ya Uongozi, Kuthibitisha Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu, na Kupitisha Bajeti ya 2016.
Mkutano huo utakuwa chini ya Mwenyekiti wake Hamad Yahya Juma

SDL WIKIENDI HII
Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa timu 24 za makundi A, B, C na D kucheza katika viwanja 12 mbalimbali nchini, kusaka nafasi nne za kupanda Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao (StarTime First League).
Kesho Jumamosi Kundi A, Singida United watakua wenyeji wa Mvuvuma FC katika uwanja wa Namfua mkoani Singida, Green Warriors watacheza dhidi ya Mirambo FC uwanja wa Mabatini Mlandizi - Pwani, huku maafande wa Trasnit Camp wakiwakaribisha Abajalo FC ya Tabora katika uwanja Kambarage Shinyanga.
Kundi B, jijini Mwanza timu ya Alliance FC itawakaribisha ndugu zao Pamba FC katika uwanja wa CCM Kirumba, Madini FC ya mkoani Arusha ikiwakaribisha Bulyanhulu FC uwanja wa Mbulu, huku AFC wakicheza dhidi ya JKT Rwamkoma katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kundi C, Abajalo FC ya jijini Dar es salaam watawakaribisha Changanyikeni FC katika uwanja wa Karume, huku kundi D, Mbeya Warriors watakua wenyeji wa Wenda FC uwanja wa Sokoine – Mbeya, Sabasaba FC dhidi ya Mkamba Rangers uwanja wa Jamhuri Morogoro, na The Mighty Elephant watakuwa wakicheza dhidi ya African Wanderes kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Jumapili kutakua na mchezo mmoja kati ya  Vill Squad dhidi ya Karikaoo ya Lindi kwenye uwanja wa Karume, Jumatatu Cosmopolitan FC watawakaribisha Mshikamano FC katika uwanja wa Karume yote ikiwa michezo ya Kundi C.
TAARIFA KWA UMMA
Juma lililopita Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliaga timu ya Taifa ya Vijana Chini ya umri wa miaka 15 (U15) ikianza ziara yake ya Afrika Mashariki kuanzia kucheza na Burundi mjini Kigoma na baadaye Kigali, Rwanda, Kampala, Uganda na mwisho Nairobi Kenya.
Bahati mbaya ziara hiyo itaishia Mwanza na Kigoma kufuatia Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA) mkoa wa Ilala kuzuia fedha kwenye akaunti zote za Shirikisho kwa madai ya kulipwa kiasi cha Shilingi 1,637,334,000 (bilioni 1.6 tshs) ikiwa ni kodi kwa kipindi cha 2010 – 2013 sehemu kubwa ikiwa ni makato kwenye mishahara (PAYE) ya walimu wa kigeni, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen na vilevile kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazili uliofanyika mwaka 2010.
Walimu wa Timu za Taifa wamekuwa wakilipiwa mishahara na Serikali na hivyo TFF haikuwajibika kuwakata kodi. Aidha, mchezo kati ya Tanzania na Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya Serikali na fedha zake hazikuingizwa katika akaunti za TFF.
Kutokana na hatua hii ya TRA shughuli nyingine za mpira zitakazohathirika nazo ni:
1. Kulipia madeni ya usafiri, chakula na posho za Timu za Taifa zilizoshiriki mtoano wa kombe la Dunia na mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Challenge Cup)
2. Program za mpira wa Wanawake na vijana zitalazimika kusimama.
3. Mashindano ya kombe la Shirikisho raundi ya pili iko kwenye hatihati kwani hakuna fedha za kugharimia michezo hiyo.
4. Mashindano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoendelea yatalazimika kusimama vilevile. Mashindano haya TFF imekuwa ikiyaendesha bila mdhamini.
5. Vifaa vya michezo (Mipira) kwa ajili ya shule za msingi na vituo vya maendeleo (Regional Football Development Centres) vinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote na TFF haitakuwa na uwezo wa kulipia usafirishaji na ushuru wake.
6. Malipo ya gharama za kambi na karo kwa ajili ya vijana wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 13 walioko shule ya Alliance Academy ya jijini Mwanza.
7. Huduma za kiutawala ikiwa ni pamoja na utunzaji viwanja na majengo, maji, umeme, ulinzi pamoja na mishahara na stahiki nyingine za wafanyakazi
8. Mwelekeo na mwitikio mzuri wa wadhamini uko kwenye hatari ya kupotea pindi mashindano na shughuli wanazozidhamini zitakapofubaa au kusimama kabisa.
9. Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) wa Mwaka 2015 uliopangwa kufanyika Tanga 19-20 Desemba 2015 sasa una hatihati ya kuweza kufanyika.
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ulipaji kodi na wajibu wa Mamlaka ya Mapato katika kuhakikisha kodi inakusanywa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa,TFF ipo katika mawasiliano na TRA katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwa ni pamoja na kupitia upya mahesabu ili kujua wajibu halisi (net liability) wa TFF na namna ya kulipa au kulipwa kutegemea ulali wa mahesabu.
Hii si mara ya kwanza hili kujitokeza, lilijitokeza Oktoba 2012 na shilingi 157,407,968 iliyokuwa mgawo wa vilabu kuchukuliwa na TRA. Kufuatia tukio hilo, yalifanyika mazungumzo kati ya TFF na serikali ambamo ilikubaliwa kwamba fedha hizo zitarudishwa TFF na mpaka sasa TFF inafuatilia fedha hizo.
Kwa taarifa hii TFF inaomba utulivu kwa wanamichezo wote pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka katika vyombo vyote husika ikiwemo TRA na wadau wengine ili jambo hili lipate ufumbuzi wa kudumu utakaoleta tija kwa serikali ya awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla wake.

No comments: