Friday, February 19, 2016

Nape Nnauye atengua uteuzi wa Katibu Mtendaji Baraza la Michezo Tanzania(BMT).

 
BT1
Waziri wa habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye(katikati) akizungumza na waandishi wa Habari leo hii katika ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kutengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu  Mtendaji  mkuu wa baraza ilo Bw. Henry Lihaya (wa kwanza kushoto)  leo jijini Dar es Salaam kutokana utendaji usiolizisha.Picha na Daudi Manongi.
BT2
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa  Bw.Dionis Malinzi(kulia) akiongea jambo na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo mhe Nape Nnauye.
BT3
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akisaini kitabu cha wageni wakati   alipotembelea  ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) leo hii kuona utendaji  wa  Baraza hilo.
……………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye  ametengua uteuzi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania Henry Lihaya baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wake.
Mhe. Nnauye alitengua uteuzi huo katika ziara yake aliyoifanya leo mapema katika ofisi za BMT kuona miundo mbinu ya ofisi hizo na kujua  changamoto walizonazo.
“Baraza likirekebishwa vyama vya michezo navyo vitakuwa mguu sawa na kuleta chachu na maendeleo katika michezo,”alisema Mhe. Nnauye.
Aliongeza kwa kusema kuwa, miaka saba ambayo Lihaya amekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza imetosha kwani hakuna mabadiliko yoyote aliyoyafanya katika sekta ya michezo tangu alipoteuliwa mwaka 2009.
Kutokana na utenguzi huo Mhe. Nnauye amemtaka Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi kupendekeza jina la Katibu Mtendaji mpya wa BMT ambaye anampendekeza kwa mujibu wa sheria ya BMT kifungu cha 5(1) baada ya kupata idhini ya waziri mwenye dhamana.
Vilevile, Mhe. Nnauye amemtaka mwenyekiti kuteua Katibu Mtendaji ambaye atakuwa ni mchapa kazi na mwenye mipango ambayo itaibadilisha BMT na kuleta chachu katika michezo nchini.
Aidha, Mhe. Nnauye amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara ya habari, utamaduni sanaa na michezo kumpangia Lihaya kazi nyingine wizarani.

No comments: