ACT WAZALENDO WAPANGA SAFU MPYA YA UONGOZI


WENYEVITI NA MAKATIBU WA KAMATI ZA KITAIFA WA CHAMA CHA WAZALENDO (ACT-WAZALENDO)

Kamati Kuu ya Chama cha Wazalendo (ACT-Wazalendo) imeidhinisha uteuzi wa Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Kitaifa. Wanachama walioteuliwa na wasifu wao ni kama ifuatavyo:


A. WENYEVITI
1.       Mustapha Boay AKONAAY (63)
Mwenyekiti wa Kamati ya Uadilifu,
Ulinzi na Usalama wa Chama
Ndugu Mustapha AKONAAY ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Stashahada ya Sheria kutoka kilichokuwa Chuo cha Maendeleo Mzumbe. Ndugu AKONAAY ana uzoefu wa miaka mingi katika tasnia ya sheria. Aliwahi kuwa Hakimu Mkaazi wa Mahakama za Wilaya na Msingi. Kabla ya kuwa hakimu alianza kazi kama Karani wa Mahakama na kupanda ngazi hadi kuwa Karani Mwandamizi wa Mahakama. Kwa sasa ni Wakili wa Kujitegemea katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Ndugu Akonaay ana uzoefu wa muda mrefu katika uongozi ambapo ameshika nafasi mbalimbali, ikiwemo Katibu Mtendaji wa Chama cha Waendesha Utalii nchini (Tanzania Association of Tour Operators). Ndugu Akonaay alikuwa Mbunge wa Mbulu kati ya mwaka 2010 na 2015.

2.       Yeremiah Kulwa MAGANJA (48)
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa
_________________________________________________________
Ndugu Yeremiah Kulwa Maganja ana Shahada ya Uzamili katika Biashara (MBA) kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na Shahada ya kwanza ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini. Ndugu Maganja pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Ndugu Maganja ana uzoefu wa kazi wa miaka mingi katika maeneo ya biashara, bajeti na uwekezaji na amefanya kazi na Jumuiya ya Ulaya kwa miaka 18. Kwa sasa Ndugu Maganja, anaendesha Kampuni ya Ushauri wa Kitaaluma katika biashara na uwekezaji ya ANDEL Consultants.

3.       Mosses MACHALI (34)
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo na Uchaguzi
Ndugu Moses Machali ana Shahada ya Uzamivu katika Sayansi ya Jamii na Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St. John’s) na Shahada ya kwanza katika Sayansi ya Jamii na Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Mt. Augustine (SAUT). Ndugu Machali alikuwa Mbunge wa Kasulu Mjini kati ya mwaka 2010 na 2015 na kabla ya hapo alikuwa mwalimu katika shule za msingi na sekondari.

4.       Albert MSANDO (36)
Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
Ndugu Albert Msando ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ni Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Ndugu Msando ni mwanzilishi wa Kampuni ya uwakili ya AlbertMsando Legal Consultants na ni moja ya mawakili katika Kampuni ya Mawakili ya Gabriel & Co Attorneys. Ndugu Msando aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Sheria na Katiba katika CHADEMA na alikuwa Diwani wa Kata ya Mabogini kati ya mwaka 2010 na 2015.

5.       Carol Moses NDOSI (32)
Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma
Ndugu Carol Moses Ndosi anajulikana katika tasnia ya habari nchini Tanzania. Amefanya kazi katika tasnia ya habari na masoko. Ndugu Ndosi ana Shahada ya kwanza katika tasnia ya Amani na Utatuzi wa Migogoro kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala. Amewahi kuwa Meneja wa Matukio wa Kampuni ya Excutive Solutions, na mwandishi wa kujitegemea akifanya kazi na kampuni zinazojihusisha na mahusiano ya umma kwa miaka kadhaa. Kwa sasa Ndugu Ndosi ni mmiliki wa Tamasha kubwa lijulikanalo kama Nyama Choma Festival. Chama cha Wazalendo kinafuraha kumkaribisha Carol Ndossi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma na tunaamini atautumia utaalamu na uzoefu wake katika mawasiliano ya umma katika kueneza na kuelimisha umma kuhusu Itikadi ya chama ya Ujamaa wa Kidemokrasia.

6.       Venance MSEBO (32)
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Miradi ya Kujitegemea
Ndugu Venance Msebo ana Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Diploma ya Juu katika Kodi kutoka Chuo cha Kodi. Ndugu Msebo ni Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu ya Tanzania na anaendesha kampuni yake ya uwakili ijulikanayo kama Ms. Austin and Mark Attorneys. Kabla ya uteuzi huu, Ndugu Venance Msebo alikuwa Katibu wa iliyokuwa Kamati ya Mambo ya Nje ya Chama cha Wazalendo (ACT-Wazalendo).

7.       Mhonga Said RUHWANYA (37)
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamaii
Ndugu Mhonga Said Ruhwanya ana Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Jamii na Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, na Shahada ya Kwanza katika Sosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ndugu Ruhwanya alikuwa Mbunge kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Kabla ya kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo, Ndugu Ruhwanya alikuwa mwanachama wa CHADEMA na alishika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu kati ya mwaka 2005 na 2010. Aidha, akiwa Mbunge alikuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani (2006-2008), Maji na Umwagiliaji (2008-2010) na Uchukuzi (2010-2012).

8.       Theopista KUMWENDA (29)
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
Ndugu Theopista Kumwenda ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT). Ndugu Kumwenda ni mwanasheria katika Kampuni ya Unitrans (T) Kilombero na amewahi kuwa mwanasheria msaidizi katika Kampuni ya Sukari ya Kilombero.

B. MAKATIBU

  1. Ado Shaibu (32)
Katibu wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma
Ndugu Ado Shaibu ana Shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyohitimu Mwaka 2015. Kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amewahi kuwa Mwalimu wa Historia na Kiingereza katika shule mbalimbali. Ndugu Shaibu amekuwa kiongozi katika mashirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na: Katibu Mkuu wa Kitabu cha Maendeleo Tanzania; Mkwenyekiti wa Tanzania Sahara Solidarity Committee. Katika uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015, ndugu Shaibu alikuwa mtafiti mkuu wa Mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mama Anna Mghwira.

  1. Dorothy Jonas TEMU (40)
Katibu wa Kamati ya Utafiti, Sera na Mipango
Ndugu Dorothy Jonas TEMU ana Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Fiziotherapi (MSc Physiotherapy) na Shahada ya Kwanza katika eneo hili (BSc Physiotherapy) kutoka katika Chuo Kikuu cha Western Cape nchini Afrika Kusini. Kikazi, Ndugu Temu amewahi kuwa Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Kuzuia Ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa zaidi ya miaka kumi, kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2015. Kwa sasa ndugu Temu ni Mshauri Mwekekezi katika Taasisi ya Fiziotherapy (LTD) iliyopo Jijini Dar es Salaam. Mbali na Kamati hii, Ndugu Temu atakaimu pia nafasi ya Katibu wa Kamati ya Fedha na Miradi hadi Katibu kamili atakapopatikana.

  1. Emmanuel Thomas MSASA (27)
Katibu wa Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
Ndugu Emmanuel Thomas Msasa ana Shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, na ni Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Ndugu Msasa pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Uongozi na Menejimenti katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Ndugu Msasa ni moja wa wanachama saba (7) waanzilishi wa Chama cha ACT-Wazalendo.

  1. Eng. Mohamed Mshamu NGULANGWA (44)
Katibu wa Kamati ya Uadilifu, Ulinzi na Usalama wa Chama
Ndugu Ngulangwa ni Mhandisi kitaaluma mwenye Shahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Uhandisi na Shahada ya Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ndugu Ngulangwa pia ana Shahada ya Uzamili (MBA) katika Biashara kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Kikazi, Mhandisi Ngulangwa amewahi kuwa Mhandisi Mwandamizi katika Shirika la TANESCO kati ya mwaka 2013 na 2015 na aliwahi kuwa Meneja wa Miliki katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kati ya mwaka 2008 na 2011. Mhandisi Ngulangwa ni mjumbe wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi Tanzania (ERB) na ni Mjumbe wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (MIET). Kwa sasa Mhandisi Ngulangwa ni Katibu wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam. 

  1. Mchange HABIBU (30)
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa
Kabla ya uteuzi huu, Ndugu Habibu Mchange alikuwa Katibu wa Mipango na Mikakati wa Chama cha ACT-Wazalendo na alihusika kuratibu ziara za kukitambulisha chama baada ya kuzinduliwa rasmi Mwezi Machi 2015. Ndugu Mchange ana Shahada ya Kwanza katika Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

  1. Mohammed MASSAGA (42)
Katibu Kamati ya Mafunzo na Uchaguzi
Kabla ya uteuzi huu, Ndugu Massaga alikuwa Katibu wa Kamati ya Chaguzi na Kampeni ya ACT-Wazalendo. Kabla ya kujiunga na ACT-Wazalendo, Ndugu Massaga alikuwa mwanachama wa CUF ambapo alishika nafasi mbalimbali katika ngazi ya Wilaya na Taifa. Ndugu Massaga ana Stashahada ya Uandishi wa Habari kutoka Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

  1. Janeth Joel RITHE (42)
Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (Bara)
Ndugu Janeth Joel Rithe ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Maendeleo Kunduchi. Ndugu Rithe ana Stashahada katika Theolojia na Maarifa ya Biblia. Ndugu Rithe alikuwa Diwani wa Kata ya Kunduchi kati ya mwaka 2010 na 2015, na aligombea ubunge katika Jimbo la Kawe katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

  1. Seif Hamad SULEIMAN (25)
Katibu Msaidizi Itikadi, Mawasiliano na Uenezi (Zanzibar)
Ndugu Seif Hamad Suleiman ana Stashahada katika Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka kutoka Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Zanzibar, na ni mwanafunzi wa Stashahada katika Menejimenti ya Raslimali Watu katika chuo hicho hicho.
Msafiri Abrahman Mtemelwa,
      NAIBU KATIBU MKUU.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.