DK. Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema), amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya nchi kuongozwa na kauli za viongozi, anaandika Happiness Lidwino.
Kutokana na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba matakwa yao katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa Chadema hakitashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.
Badala yake, Chadema kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya na bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipoukaribisha ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Dkt. Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku akisisitiza kuwa Chadema kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki, demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.
“Suala la Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa kwenye rasimu ya pili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ni agenda muhimu kwa Watanzania wapenda nchi yao na sisi ni kipaumbele kwa mwaka huu na kuendelea hadi hapo nchi yetu itakapopata Katiba Mpya ya Wananchi.
Amesema “Jana na leo tumewasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakisema kuwa wanajiandaa kuitisha kura ya maoni…hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunajua Watanzania wengi wanataka Katiba Mpya iliyotokana na maoni yao, si ile iliyochakachuliwa bungeni.
Aliongeza kuwa “Katiba Mpya iliweka masuala kuhusu haki za wananchi, kuimarisha misingi na kuweka mifumo ya demokrasia na uongozi bora, walau kwa kuanzia. Hatuwezi kusema sasa tutatumia mikakati gani kuwahamasisha Watanzania kuidai Katiba Mpya…tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni,”
Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Mashinji amesisitiza kuwa suala la nchi kuwa na misingi na mifumo imara ya demokrasia na uongozi bora ni muhimu kwa Tanzania, katika wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi mkubwa wa nishati ya gesi na mafuta, akisema vinginevyo ni hatari iwapo taifa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, litaendelea kuwa na wananchi waliokata tamaa kutokana na mfumo mbovu uliopo.
Kwa upande wake ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Centre Party, Knut Olsen, umesema kuwa chama hicho kinashukuru kwa mradi huo kuingia katika hatua ya pili kuanzia mwaka 2016-2019 huku hatua ya kwanza ikiwa na mafanikio makubwa katika jamii ya wananchi wa maeneo ya pembezoni.
“Kama unavyojua, mradi huu kupitia TCD unahusisha vyama vyote vyenye uwakilishi ndani ya bunge, na lengo letu ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama hasa wanawake na vijana katika ngazi ya jamii kwenye vitongoji, vijiji, kata na bunge ili waweze kushiriki mchakato wa maamuzi. Tunatarajia kuendelea kupata ushirikiano katika hatua ya pili,” amesema Inger Bigum, ambaye ni Meneja wa Mradi hapa nchini.
Wengine waliokuwa katika ujumbe huo wa Centre Party ni pamoja na Vijana Sara Hamre Katibu Mkuu wa, Katibu Mkuu wa Wanawake, Eline Stokstad-Oslan na Kristin Madsen Katibu Mkuu wa Wazee, Mradi huo wa Elimu ya Demokrasia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini unaohusisha vyama vyenye uwakilishi bungeni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) chini ya ufadhili wa chama hicho, katika awamu ya kwanza ulihusisha kata za Msangamkuu, Nanyamba, Ziwani na Mbembaleo na katika sasa awamu ya pili utakuwa katika kata za Mkunwa, Tangazo, Mayanga na Madimbwa
No comments:
Post a Comment