WAKATI ikiwa imebakia siku nne ili kuanza Bunge la kujadili na kupitisha Bajeti ya serikali ya mwaka 2016-2017,Tayari Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Hakielimu imewataka wabunge kuondoa itikadi zao za vyama na kuungana pamoja ili kuishinikiza serikali kupunguza fedha za matumizi ya kawaida katika bajeti ya wizara ya elimu,
Ili fedha hizo za matumizi ya kawaida zielekezwa kwenye mipango ya Maendeleo ya elimu.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji-HakiElimu,John Kalage amesema wanawataka Wabunge kuuungana na kuishinikiza serikali kutekeleza mpango wa miaka mitano (2015-2020) unayoitaka bajeti ya kawaida na ya maendeleo kuwa na uwiano wa asilimia 60 na 40.
Amesema Bajeti iliyopo haikizi hali halisi ya Elimu na imechangia kurudisha maendeleo ya elimu kutokana bajeti ya elimu kuwa ndogo,
Kalage ametolea mfano Bajeti ya Fedha ya mwaka 2015/2016 bajeti nzima ya elimu ilikuwa Bilioni 3,887.kati ya hivyo Bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu ilikuwa bilioni 604 tu sawa na (16%) ya sekta nzima,huku bajeti ya matumizi ya kawaida ikiwa ni bilioni 3,282 sawa na (84%) ya Bajeti nzima jambo analodai ni vigumu elimu yetu kukuwa.
Hata hivyo Kalage ameonesha masikitiko yake katika Bajeti hiyo kwa kusema licha upangaji huo wa fedha inayodaiwa kuwa ni fedha ya maendeleo katika sekta ya elimu huelekezwa katika kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,
“Kwa mfano Bajeti ya 2015/16 bajeti ya maendeleo ilitengwa bilioni 604,lakini nusu ya fedha hizo bilioni 306 ilitengwa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu,hivyo bajeti ya maendeleo ya elimu ilikuwa Bilioni 298,sasa kwa hali hii elimu yetu haitaweza kukuwa “amesema Kalage.
Kalage ametumia nafasi hiyo kuishauri serikali kuondoa fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu katika bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu na badala yake amesema fedha hizo zipangwe katika matumizi ya kawaida ,kwa madai kuwa itasaidia kutoa picha halisi ya matumizi ya maendeleo katika sekta ya elimu.
Katika hatua nyengine,HakiElimu pia wamewataka Wabunge kuitazama kwa umakini dhana ya elimu bure iliotengwa na Rais John Magufuli kwa kuangalia bajeti husika inayokwenda kutekeleza elimu bure kwa madai kuwa Bajeti iliyopo ni ndogo kabisa na hakikizi maitaji halisi.
No comments:
Post a Comment