Wednesday, April 27, 2016

MGOMO WA KISIASA UNAOENDELEA KISIWANI PEMBA WACHELEWESHA MAZISHI

maxresdefaultNa Masanja Mabula –Pemba
MGOMO wa  kisiasa  unaoendelea Kisiwani  Pemba juzi ulichelewesha kwa muda wa saa kadhaa  mazishi ya  marehemu Bi  Achia Khatib wa Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni , baada ya msikiti uliokuwa utumike kuswalia mwili wa marehemu kufungwa kwa kufuli .
Mbali na kitendo cha kufungwa kwa msikiti huo , pia baadhi ya vifaa vilivyokuwa vitumike katika mazishi hayo  kufichwa ikiwemo kitanda (jeneza) pamoja na mitaimbo ya kuchimbia kaburi kwani sehemu hiyo ni ya mawe .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa wanafamilia , Said Omar Said alisema kuwa hali hiyo ya sintofahamu  ni imetokea ikimhusisha  mtoto mkubwa wa marehemu Abdalla Kombo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kijijini hapo .
Alifahamisha kwamba wananchi waligoma na kusababisha kufungwa kwa msikiti , wakidai kwamba hawako tayari kushiriki mazishi , hadi pale mtoto wa marehemu (Mwenyekiti wa CCM) atakapoondoka katika msiba huo .
“Unajua mzee wetu alikuwa ni mfuasi wa CUF , lakini sasa mtoto wake mkubwa  ni mwanaCCM , hivyo alitaka aondoke ili washiriki mazishi hayo ”alieleza Said Omar Said kwa maskitiko .
Sheha wa Shehia ya Mjini Wingwi Shehe Yussuf Hamad aliiambia gazeti hili kwamba , wananchi hao walitaka pia kuzuia makaburi yasitumike kumzika marehemu , lakini serikali ya kijiji ililazimika kutumia nguvu kutumika kwa makaburi hayo .
Alisema kwamba visa vingi vya maajabu vilitokea katika msiba huo , kwani hata sindano ya kushinea sanda ilichukuliwa na mtoto mdogo wa marehemu Hamad Kombo na kuifichwa wakati kazi ya ushinaji wa sanda ikiendelea.
Hali hiyo iliwafanya ndugu na jamaa wa karibu kuomba msaada kutoka vijiji jirani ikiwemo Micheweni na  Majenzi , ambapo wakaazi wa vijiji hivyo ndio waliosaidia kupatikana sanda na kitanda cha kubebea mwili wa marehemu .
Imamu wa msikiti wa Ijumaa katika Shehia hiyo  Bakar Abdalla alipotafutwa kwa njia ya simu  alikana kuhusika na kitendo cha kufungwa msikiti , na kusema hata taarifa za kuvunjwa kufuli hajazipata .
Aidha alifahamisha taarifa za kifo cha bibi huyoa anazo , lakini taarifa za wapi swala ya kumswalia maiti  itafanyika katika msikiti huo hakuwa na taarifa .
“Taarifa ya kifo nilizipata lakini sehemu ambayo swala itafanyika sikuwa na naelewa , mimi nafahamu kwamba ulikotokea msiba kuna msikiti mwengine mdogo na ndio uliotumika kumuswalia maiti ”alieleza.
 Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mwenyekiti wake Abeid Juma Ali ilifika katika eneo la tukio na baada ya mazungumzo na baadhi ya wazee katika shehia hiyo  yaliyochukua muda wa saa mbili , walilazimika kuvunja kufuli katika msikiti huo .
Akizungumza na baada ya tukio la kuvunja kufuli , Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo alilaani kitendo hicho na kuwataka wananchi kushirikiana na pamoja katika shughuli za kijamii .
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alikemea nyumba za ibada kutumika kwa masuala ya siasa na kuahidi kulitafutie ufumbuzi suala hilo kwa kukutana na mashekhe wote na maimamu wa misikiti yote Wilayani hapa .
“Hichi kitendo kwa kweli si cha kiungwana huwezi kumsusia maiti kwa misingi ya kisiasa , nimepanga kukutana na mashekhe wote wa wilaya tulizungumzie ikiwezekana kuweka maazimio lengo ni kudumisha upendo “ alieleza.
Mazishi hayo ambayo yalipangwa kufanyika majira ya saa saba za mchana , yalifanyika saa kumi na moja za jioni baada ya wanaccm kutoka shehia na vijiji jirani kufika na kusaidia shughuli za kuustiri mwili wa marehemu .

No comments: