Friday, April 15, 2016

Ofisi ya Bunge yatoa ufafanuzi kamili juu ya utata unaoendelea wa mkataba wa LUGUMI.

Kumekuwa na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na baadhi ya vyombo vya Habari kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikitekeleza majukumu yake tarehe 5 Aprili, 2016 ililitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha Mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa Alama za Vidole AFIS (Automated Fingerprint Identification System).

 Ofisi ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili kwamba, taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha umma kutokana na kile kilicho amuliwa na kamati hiyo.
 
Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba tarehe 5 Aprili, 2016, kamati hiyo ilikutana na kujadili Taarifa ya Ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa za fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2014 ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika utekelezaji wa mkataba huo.  

Kutokana na dosari hizo, kamati iliomba Afisa Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mabo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge ili kamati iweze kuchambua na kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua. Kufuatia agizo hilo, kamati ilimwandikia pia Katibu wa Bunge taarifa kuhusu agizo hilo tarehe 12 Aprili, 2016 ili kupatiwa maelezo hayo kutoka kwa Afisa Masuhuli.
  
Aidha, Ofisi ya Bunge  ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 12 Aprili, 2016 kuwasiilsha Taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotokana na kikao hicho cha tarehe 5 Aprili 2016 kabla ya tarehe 18 Aprili, 2018 kama ilivyoshauriwa na kamati . Hivyo ni vyema Umma ukafahamu kuwa kilichoombwa na Kamati ni Maelezo ya utekelezaji wa Mkataba huo na sio Mkataba kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya Habari ambapo Ofisi ya Bunge iliomba maelezo hayo yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.
 
Imetolewa na: 
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge DAR ES SALAAM 

15 Aprili, 2016.

No comments: