Tuesday, June 14, 2016

LIPUMBA AZIDI KUKATALIWA-MTATIRO AELEZA MAZITO,YAKO HAPA


Kama mzee wetu anao washauri, wamwambie kuwa “DALILI ZA MVUA NI MAWINGU”. Na kwamba, NGOMA ivumapo sana hupasuka na tena ajulishwe kuwa VITANI hakuna michezo ya KUJIFICHA na KUONEKANA baadaye, jana niliwaambia kuwa najua CUF inao watu makini wanaojua nini haki ya PROFESA LIPUMBA na nini haki ya CUF kama chama. Kwa wale ambao hawakuelewa ujumbe wangu wa jana nilikuwa namaanisha viongozi wa CUF watakuwa upande wa chama, hawatafuata matakwa ya mtu, na dalili zimeanza kuwa hivyo. Mwisho wa siku mshindi wa mchezo huu ni CHAMA na WANACHAMA wenye UTII na COMMITMENT kwa chama chao, na siyo MTU!



Kuna watu nasikia wanasema WATAGAWANA MBAO, ukweli ni kuwa CUF ni taasisi imara na haiwezi kuwa na MBAO za kugawana. Kutakuwa na machaguo mawili tu, aidha kuondoka na mtu au kubaki na chama, wale watakaobaki na chama watabaki na mbao zote, na wale watakaoondoka na mtu hawatandoka na hata kipande cha ubao – kwa sababu mchezo huu hautahitaji hasira. Siasa ni maisha halisi ya watu, vyama vikiruhusu zigeuke kuwa mchezo wa KOMBOLELA, zitakosa maana na hapa lazima ieleweke, kwamba kuna mambo ambayo vyama vya upinzani vikiyaruhusu yaendelee kutendeka, vitakuwa vinafanya ujinga wa kiwango cha PhD na Uwendawazimu wa Kiwango cha MWENDOKASI!
Profesa Lipumba ambaye kila mtu anamheshimu sana, apishe kwenye uongozi ili chama kijiandalie ZAMA mpya. Nawarejesha kwenye nukuu yangu ya mwaka jana wakati anajiuzulu, kwamba “Kamanda wa vita akiuawa katikati ya vita, siyo muda wa kuanza kulia na kuomboleza, siyo muda wa kulaumiana, anatafutwa askari mwingine na kutwaa bunduki yake, mapambano yanaendelea mbele”.
Ninaamini kuwa, CUF inao watu wenye sifa za kuwa wenyeviti wa chama na tena kisiasa wapo watu bora sana. Chama kisiogope kufanya maamuzi sahihi kwa ajili yake na siyo kwa ajili ya mtu. Na iwe fundisho kwa wanasiasa kuwa HISIA za wafuasi wa vyama hazichezewi, na iwe FUNDISHO kwa viongozi wa kisiasa kwamba MISIMAMO na KUTOYUMBA ni wajibu wao usiokwepeka.
Katika mgogoro huu wa kutengenezwa makusudi, wanachama imara wanajua wajibu wao, wasimame upande wa chama, wasimame upande wa taasisi, maana taasisi itakuwepo siku zote. Mtu na watu watapita haraka na kunyauka kama maua.
Namshauri Prof. Lipumba, kwa namna yoyote ile, asikubali kutumikia matakwa ya kundi lolote lile, iwe ndani ya chama au nje ya chama. Asikubali kuwa sehemu ya kuanzisha mgogoro na vurumai kubwa ndani ya chama, asikubali kuwa chanzo cha kuleta sintofahamu kama hii, namtambua Mwenyekiti wangu kama mtu makini na muumini safi wa dini ya kiislamu na huu ni mwezi mtukufu wa Ramadhani, hebu na ajitafakari upya ikiwa NIA yake ni salama kwa ajili ya wanachama wa CUF na nchi yetu.
Binafsi nisingelipenda kuona mgogoro mwingine mkubwa CUF, ambao matokeo yake sote tunayajua, kwamba chama ndicho kitashinda na kitabaki salama salmini, na kwamba watu wachache ndiyo wataumia na kufedheheka, akiwemo mtu anayeheshimiwa sana na aliyewahi kushiriki kukijenga chama hiki kwa nguvu zake na akili zake zote.

No comments: