NIDA YAANZA KUTOA VITAMBULISHO VYENYE SAINI

1Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bi. Rose Mdami akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu zoezi la utoaji wa vitambulisho vipya vyenye saini ya mwenye kitambulisho. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji Vitambulisho Bw. Alphonce Malibicha na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mifumo ya Kompyuta Bw. Mohamed Khamis.
2Kaimu Mkurugenzi Mifumo ya Kompyuta Bw. Mohamed Khamis akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu faida za vitambulisho vya taifa leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji Vitambulisho Bw. Alphonce Malibicha na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Rose Mdami.
3Baadhi ya waandishi wa habari wakiangalia video ya faida za vitambulisho vya Taifa iliyoandaliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa ajili ya kuelimisha umma kwenye mkutano wa Mamlaka hiyo na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Fatma Salum (MAELEZO)

………………………………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kutoa vitambulisho vya Taifa vyenye saini ya mwombaji kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Mamlaka hiyo Bi. Rose Mdami wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Mdami alisema kuwa lengo la Mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata vitambulisho vya Taifa ambapo katika hatua ya kwanza mamlaka hiyo inachakata taarifa za wananchi walizotoa wakati wa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Utoaji wa vitambulisho hivi vyenye saini ya mwombaji utasaidia kuwatambua wahusika pale wanapohitaji huduma mbalimbali za kijamii.
“Upatikanaji wa vitambulisho vyaTaifa utasaidia Serikali kuondokana na tatizo la Watumishi hewa kwa kuwa mfumo wetu utaunganishwa na mifumo mingine inayosimamia utumishi wa umma” alisisitizaMdami.
Utoaji huo wa vitambulisho utaanza kwa kutoa namba za utambulisho kwa wananchi ilizisaidie katika upatikanaji wa huduma mbalimbali wakati mchakato wa kuzalisha vitambulisho hivyo ukiendelea.
Mdami alifafanua kuwa baada ya kuchakata taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi zitarudishwa kwenye mitaa na vijiji husika kwa ajili ya uhakiki wa taarifa hizo.
Lengo la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba mwaka huu wananchi wote wawe wamepatiwa namba ya utambulisho .

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.