Thursday, June 30, 2016

WAFANYAKAZI WA ABANA WAANDAMANA KUDAI MIL 400 WANAZODAI

ma1Wafanyakazi wa kiwanda cha kuchapisha vitabu cha ABANA Printers ltd,kilichopo kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani,wakiandamana kudai mishahara na mafao yao wanayodai kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ambayo yamefikia mil 400 .
(Picha na Mwamvua Mwinyi) 

———————————————————–

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
WAFANYAKAZI wa kiwanda cha uchapishaji vitabu(ABANA Printers Ltd) kilichopo kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ,wanadai fedha za mishahara na mafao yao kiasi cha sh.mil.400 tangu mwaka 2014 bila mafanikio.
Aidha wafanyakazi hao waiomba serikali ya awamu ya tano kuingilia kati tatizo hilo kwani wameshapigania haki zao kupitia mahakamani ,wizara,idara na vyama vinavyojishughulisha kutetea haki za wafanyakazi lakini hakuna msaada walioupata.
Wameeleza kuwa hadi sasa wanaishi katika maisha magumu  huku wengine wakiwa wamefukuzwa kwenye nyumba walizopanga  na wenzao watatu wamefariki kutokana na ugonjwa wa moyo.
Hayo yamejiri jana baada ya wafanyakazi hao kuchukua hatua ya kufanya maandamano nje ya kiwanda hicho na kisha kumfikishia kilio chao mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi (CCM)Bagamoyo,alhaj Abdul Sharif ili aweze kuwasaidia kulipwa haki zao.
Mwenyekiti wa tawi la chama cha wafanyakazi tawi la ABANA printers Wilbard Ikigo ,alidai kuwa mmiliki wa kampuni hiyo anajigamba kwa kusema serikali ipo mkononi mwake hivyo hawezi kuchukuliwa hatua yoyote.
Alisema ni miaka miwili na nusu sasa tangu watelekezwe na mwajiri wao hali iliyosababisha kuingia katika mgogoro na mmiliki huyo.
Hata hivyo Ikigo alisema wameshachukua hatua mbalimbali ikiwemo kufikisha kero yao CMA ambapo walishinda kesi na kuamuriwa walipwe haki zao .
‘Lakini mwajiri huyu bado aligomea amri anazopewa tuliamua kwenda kufungua kesi mahakama kuu ambako tulishinda na iliamuriwa  mitambo iliyopo kiwandani ipigwe mnada ili tuweze kulipwa haki zetu lakini alikiuka tena amri za mahakama”
“Siku mbili kabla ya mnada ,madalali walijitoa na kushindikana kufanyika mnada huo huku mwajiri huyo akiendelea kujinadi kuwa serikali iko mkononi mwake na twende kokote hakuna atakachofanywa”alisema Ikigo.
Alielezea kuwa hawajui wamiliki wa kiwanda hicho wana nguvu gani hadi idara,wizara na mahakama zikakiukwa kwa hatua zinazochukuliwa na kushindwa kuchukuliwa hatua zinazostaki .
Nae fundi mitambo kiwandani hapo Ally Abdallah alisema walishaandika barua ya kukutana na waajiri wao ambapo walipokutana nao walikana kuwa hawawatambui na hawadaiwi na mfanyakazi yoyote.
“Baada ya hapo tukaenda kwa Paul Makonda wakati alipokuwa mkuu wa wilaya ya Kindondoni ambako ofisi kuu ya kampuni hii ipo Kinondoni ambapo alimwandikia barua ya kumpa agizo hadi ikifikia mwezi wa 30,desemba 2015 awe ameshalipa lakini hakulipa.”alisema Abdallah.
Abdallah alisema hatua nyingine waliyochukua ni kwenda kwa kamishna wa kazi ambapo aliitwa na kuahidi mwenyewe kuwa atalipa lakini hajalipa hadi sasa hivyo kamishna huyo aliamua kumshtaki katika mahakama ya kiraia.
Steven Bituro alimuomba Rais Magufuli kuingilia kati kwa kuwaagiza watendaji wake kuchukua hatua zinazostahili ili wapate haki zao.
Alisema kiwanda hicho kwasasa kimefungwa ,badala ya kuendelea kufanya kazi kwa maslahi ya mtu binafsi na kudidimiza utekelezaji wa kukuza sekta ya viwanda nchini.
Bituro alieleza kuwa kiwanda hicho ni muhimu nchini kutokana na kuchapisha vitabu mbalimbali na ni kiwanda kinachotegemewa kuchapisha vitabu mashuleni na mitambo yake ni mikubwa lakini kimefungwa kwa maslahi ya mtu mmoja.
Kwa upande wake msimamizi wa uzalishaji kiwandani humo, Venance Mbamba alikiri ni kweli hawajalipwa madai yao kwa muda mrefu .
Mbamba alisema ni hatua mbalimbali zimechukuliwa za kisheria pasipo ufumbuzi na mwajiri ameamua kufunga makufuli kwenye kiwanda hivyo uzalishaji umesimama kwa mwezi mmoja sasa.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilayani Bagamoyo ,alhaj Abdul Sharifu alifika kiwandani hapo  na ameahidi kushirikiana nao bega kwa bega kutatua kero hiyo.
Alieleza kuwa kilio hicho kimemgusa kwani dhamira kuu ya rais Magufuli ni kuinua ajira kwa jamii lakini inashangaza kuona baadhi ya waajiri wanakuwa wakandamizaji na hawathamini wafanyakazi wao.
Alhaj Sharif aliziomba taasisi za haki za binadamu na serikali kusimamia suala hilo ambalo linawaumiza waajiri na familia zao.
Alisema ifikie hatua sasa ya kuwachukulia hatua wawekezaji na waajiri wababaishaji ambao wamekuwa wakijali matumbo yao na kuwatumia watumishi wao pasipo kuwatahamini.
Juhudi za kuwatafuta wamiliki wa kampuni hiyo ili waweze kujibu malalamiko hayo hazikuzaa matunda licha ya kupiga simu zao mara kadhaa.
Kampuni hiyo ya ABANA printers ltd,ilianza mwaka 2010,ina jumla ya wafanyakazi 45 na inamilikiwa na wamiliki akiwemo Micael Edler na mkewe Cristina Edler kutoka nchini Sweden pamoja na mmiliki mzawa Richard Kimwaga Stika .

No comments: