Friday, July 22, 2016

KAMATI KUU CHADEMA KUKUTANA KESHO KIKAO CHA DHARURA DAR.,HII NDIYO MADA WATAKAYOJADILI


KIKAO CHA KAMATI KUU YA DHARURA 

Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari kwamba Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), itakutana kwa dharura, jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, ambapo pamoja na masuala mengine, itapokea taarifa na kujadili hali ya siasa nchini. 

Katika siku za hivi karibuni, taifa limekuwa likipitia katika majaribu makubwa, ikiwa ni pamoja na uvunjifu mkubwa wa sheria na taratibu za kuongoza nchi unaofanywa waziwazi na mamlaka za juu/viongozi waandamizi wa nchi kupitia kauli na matendo mbalimbali kiasi cha kuwashtua Watanzania ambao wangependa kuona nchi yao ikiendeshwa katika misingi ya uwajibikaji wa kisheria na demokrasia. 

Katika kikao hicho cha siku mbili, Julai 23-24, mwaka huu, Kamati Kuu pia itapokea taarifa na kujadili kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mipango mbalimbali inayoendelea ya kukipanga chama ili kiendelee kufanya shughuli zake kwa ufanisi hususan kinapokwenda kuimarisha misingi kuanzia ngazi ya kitongoji nchi nzima, kupitia usimamizi wa kanda 10 za chama. 

Imetolewa leo Ijumaa, Julai 22, 2016 na; 

Tumaini Makene 

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari 
CHADEMA

No comments: