Friday, August 19, 2016

LIGI KUU YA VODACOM YAANZA, TFF YATOA ANGALIZO

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17 inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Agosti 20, 2016 kwa michezo mitano huku Bingwa Mtetezi wa Kombe hilo 2015/16, Young Africans ya Dar es Salaam ikisubiri hadi Agosti 31, 2016 kuanza kutetea taji lake.

Young Africans inatarajiwa kusafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kucheza na TP Mazembe kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Michezo itakayochezwa kesho ni pamoja na Simba SC itakayoikaribisha Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, ulioko Chang’ombe Dar es Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni wakati Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji.
Kadhalika Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga sawa na Mtibwa Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya Mbeya itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC ya huko.
Wakati ligi ikianza, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF. Vilevile tumeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba. Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
TFF linapenda kuzikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.

No comments: