Thursday, August 11, 2016

TAARIFA YA SERIKALI KULIFUNGA GAZETI LA MSETO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifungia kwa miezi 36  gazeti la “MSETO”. Amri ya kulifungia  Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 242 lililotolewa tarehe 10 Agosti, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25(1).
Kifungu hicho kinasema “Waziri akiona kwamba kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya kudumisha amani na usalama inafaa afanye hivyo aweza kutoa amri na kuitangaza kwenye Gazeti la Serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litakoma kutolewa tangu siku (ambayo katika fungu hili itaitwa ”tarehe ya kuanza kutumika”) itakayotajwa katika amri hiyo”
Uamuzi huo unazuia gazeti la Mseto kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.

Aidha, hatua hii ya kulifungia gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Septemba, 2012 hadi Agosti,  2016  kumtaka Mhariri wa gazeti kuacha kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari bila mafanikio.
Kutokana na hali hiyo, Serikali kwa masikitiko makubwa, imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wa Serikali kwa lengo kutaka  kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na matarajio makubwa kwa uongozi wa Awamu ya Tano.
Pamoja na makosa mengine, hivi karibuni gazeti lao katika toleo Na. 480 la tarehe 4 hadi 10 Agosti, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua ya kugushi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yenye kichwa cha habari kisemacho  “Waziri Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.
Kwa mujibu wa vyombo vya uchunguzi vya Serikali, imebainika kwamba nyaraka hiyo imeghushiwa na wahariri na walipotakiwa kuleta uthibitisho wa nyaraka waliotumia katika gazeti lao, walishindwa kuleta vithibitisho huo.
Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ambayo ukizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo
Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha uhuru na mipaka ya habari kama vile Tamko la Kimataifa la haki za Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu 1981.
Mikataba na matamko hayo kwa pamoja licha ya kuanisha uhuru wa habari ambao Tanzania imeruhusu kwa kiwango kikubwa pia, imeweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uongo, uzushi na uchochezi.
Ninapenda  kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kujenga uhusiano mzuri na wa kirafiki kati yake na wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza tena wadau wa sekta hii kuzingatia Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kujenga heshima ya tasnia ya habari na kulinda amani ya nchi yetu.
Mhe. Nape M. Nnauye (Mb,)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

No comments: