KAMATI YA UTENDAJI YA TAIFA IMEKATAA MAONI NA USHAURI ULIOTOLEWA NA MSAJIRI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI
Jana tarehe 24/9/2016 KAMATI YA UTENDAJI YA TAIFA YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama cha wananchi) imekutana katika kikao chake cha dharura kilichofanyika kwenye Makao Makuu ya Chama, Zanzibar.
Kamati ya Utendaji Taifa imejadili taarifa kuhusiana na MAONI NA USHAURI WA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI pamoja na KITENDO CHA UVAMIZI WA OFISI KUU YA CHAMA BUGURUNI, DAR ES SALAAM kilichofanywa na Ibrahim Lipumba na kundi lake la wahuni na kusababisha uharibifu wa mali za Chama. Kutokana na matukio hayo Kamati ya Utendaji ya Taifa imefikia maamuzi yafuatayo;
1. Baada ya kupitia Maoni na Ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini juu ya malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi yake na Ibrahim Lipumba na wanachama wenzake waliochukuliwa hatua za kinidhamu na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Kamati ya Utendaji ya Taifa inakataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni yaliyopendekezwa na Msajili na badala yake inaendelea kusimamia maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21/8/2016 uliokubali kujiuzulu kwa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa yaliyofikiwa katika kikao chake cha tarehe 28/8/2016 juu ya kuwasimamisha uanachama Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye.
Katiba ya Chama haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya Chama na kubatilisha maamuzi ya vikao hivyo.
2. Kutokana na kitendo cha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni na kusababisha uharibifu wa mali za Chama, Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa mujibu wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka 2014 imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kitakachofanyika tarehe 27/9/2016 siku ya Jumanne, kuanzia saa 4 asubuhi kwenye Makao Makuu ya Chama, Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka 2014, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeandaa ajenda na kumfikisha Ibrahim Lipumba mbele ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa na kutakiwa kujieleza na kujitetea kwa nini Baraza Kuu la Uongozi Taifa lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake aliyoyafanya jana.
Ibara tulizozitaja hapa zinazungumzia;
“ Kulinda heshima ya Chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya katiba ya Chama, kutii kanuni za Chama, kutii sheria na sheria ndogondogo za serikali iliyoundwa kihalali na pia, kwa busara, kukosoa utekelezaji mbaya wa serikali kwa hoja za msingi ili kuendeleza maslahi ya Chama, maslahi yake mwenyewe, maslahi ya wanachama wenzake, maslahi ya nchi na maslahi ya raia wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Ibara 12(6)
“ Kuwa mwaminifu kwa Chama na serikali zilizoundwa kihalali na kwa ridhaa ya wananchi na kuwa tayari kuwatumikia watu kwa juhudi, maarifa na vipaji vyake vyote.” Ibara 12(7)
“ kukilinda kutokana na maadui wa ndani au wa nje wanaokusudia kukihujumu, kukiua, kukigawa au kukidhoofisha.” Ibara 12(16)
HAKI SAWA KWA WOTE
______________________________ ______
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU CUF
No comments:
Post a Comment