Thursday, October 27, 2016

Dkt. Kitima; Bodi ya Ithibati ya Wanahabari haitazuia uhuru wa habari

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Marios cha Mtwara Padre, Dkt. Charles Kitima  akichangia mada katika moja ya Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi za Mwalimu Julius Nyerere.( PICHA KUTOKA MAKTABA)


Na: Frank Shija, MAELEZO

27.10.2016
Uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari kama ilivyoainishwa katika Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 hautaminya uhuru wa kutafuta na kusambaza habari.

Hayo yamebainishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Marios kilichopo Mtwara Dkt. Charles Kitima katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii leo.
Dkt. Kitima amesema kuwa msingi wa haki ya kutafuta taarifa na kusambaza habari unatokana ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo watu wasiwe na hofu ya kuwa Bodi hiyo itawaminya watu kutoa mawazo yao.
“Bodi ya Ithibati ya Wanahabari haiwezi kuwa kizuizi cha watu kutafuta na kusambaza habari kwani haki hiyo ipo kikatiba kupitia ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Alisema Dkt. Kitima
Amesema kuwa haoni sababu yoyote ya kupinga uanzishwaji wake kwa kuwa malengo yake ni kuhakikisha inasimamia kanuni za maadili ya wanahabari hapa nchini na kuijengea heshima tasnia.

Aidha aliongeza kuwa pamoja na kuanzishwa kwa Bodi hiyo hakuna maana kwamba uanzishwaji wake utachukua majukumu ya taasisi zingine za habari zilizopo na kuongeza kuwa waandishi wa habari duniani kote wanafanya kazi kwa kufuata miiko ya maadili ya uandishi wa habari.

Alisema kuwa suala kubwa kwa mwanahabari ni kuzingatia maadili na weledi wa taaluma yake ili kutekeleza majukumu yake pasipo kusababisha usumbufu kwa mtu au kikundi kingine
.
Bodi ya Ithibati ya Wanahabari ipo katika muswada wa huduma za Habari sehemu ya Tatu na kuelezewa kwa kirefu katika kifungu cha 10 hadi 20 katika muswada huo unaopatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.bunge.go.tz.

No comments: