KAULI YA ACT WAZALENDO KWA OLE SENDEKA NA CCM


TAARIFA KWA UMMA

CHAMA  cha ACT Wazalendo kimeshtushwa na tuhuma, kashfa, porojo na matusi mbalimbali yaliyotolewa jana na msemaji wa chama cha Mapinduzi(CCM), Ndugu Christopher Ole Sendeka dhidi ya Kiongozi wa chama chetu, ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto.
 Kutokana na hayo chama kina masuala yafuatayo ya kusema kwa wanachama wetu na umma wa Watanzania kwa ujumla:

• Chama chetu kinakaribisha uchunguzi juu ya mali na madeni ya Kiongozi wetu, ndugu Zitto. Tutafurahi uchunguzi huo ukihusisha akaunti zake za benki pamoja na mfumo wa maisha yake binafsi (Life Style). 
Tunavitaka vyombo vya uchunguzi vianze kazi hiyo mara moja kwani tunaamini kuwa  Kama kuna Kiongozi ambaye Mali, Madeni, Maslahi na Akaunti zake viko wazi basi ni ndugu Zitto. 
Ikumbukwe kuwa Katiba na Kanuni za chama chetu huwataka Viongozi wote wa chama kuweka hadharani tamko la mali zao na madeni, ndugu Zitto alitekeleza matakwa hayo ya kisheria, na mali pamoja na madeni yake yako hadharani na mtandaoni. Tunatambua chama tawala kinaweweseka na tunataka kiondokane na ugonjwa huo wa  kuweweseka,badala yake  wachukue hatua za uchunguzi dhidi ya ndugu Zitto.

• ACT Wazalendo tunayo taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG. Kupitia taarifa husika CAG ametoa Hati safi Kwa Shirika la NSSF Kwa hesabu za mwaka 2014/15. Hajaona ufisadi wowote ule. 
Sijui msemaji wa CCM anatumia taarifa ipi ya CAG kusema kuwa NSSF ilinunua Ardhi Kwa bei ya Shilingi Milioni 800 aliyomhusisha nayo Kiongozi wetu.
 Kwa mujibu wa barua ya CAG Kwa Uongozi wa NSSF (Management letter), Shirika hilo halijanunua ardhi yoyote Kigamboni, bali Shirika limeingia ubia wa Ardhi Kwa Hisa (Land for Equity). 
Hivyo ni vizuri mbwatukaji huyo wa Chama tawala akaeleza kwa undani Ufisadi anaousema juu ya manunuzi ya ardhi kwa kunukuu ripoti ya CAG kaitoa ukurasa namba ngapi katika ripoti husika. 
Labda chama chake kina taarifa nyengine ya CAG tofauti na iliyowasilishwa kwenye Kamati ya PAC.

Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa chama  tawala, amemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kuwa Balozi. Kauli za Msemaji wa chama tawala alizozitoa jana zikiaminiwa zina maana kuwa Rais na Mwenyekiti wa chama chake anateua mafisadi kuwa mabalozi. Ni vizuri nyie wanahabari muulize juu ya hili jambo.

• Ni wajibu wa Viongozi wa chama cha ACT Wazalendo kuupinga ujinga popote pale ulipo, Kiongozi wa Chama chetu, ndugu Zitto, anatekeleza wajibu huo kwa Uzalendo mkubwa kwa Taifa lake.
 Chama chetu kiko pamoja naye katika kupinga Ufisadi mkubwa wa ESCROW ambao chama tawala kimeukalia kimya, ufisadi wa Mabilioni ya HATI FUNGANI na hata sasa anapowapigania Waandishi wa Habari nchini katika Kampeni yake ya kupinga MSWADA MBAYA wa Habari. 
Tunajua kuwa kampeni hii ya kupinga Mswada mbaya wa Habari ndiyo ambayo imezua ubwatukaji huu wa msemaji wa chama tawala.
 Ni muhimu Serikali na chama tawala wajue kuwa chama chetu kitaupinga mswada huo ambao utakwenda kuua tasnia ya habari nchini mpaka pale utakaporekebishwa. Porojo, kashfa na matusi havitaturudisha nyuma, tutaisimamia hoja hii mpaka mwisho.

• Tunamtaka msemaji wa chama tawala aache porojo, kashfa, vijembe na matusi. Ni muhimu ajikite katika kukishauri chama chake kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Sasa ni mwaka mmoja tangu wachaguliwe, lakini hakuna madawa hospitalini, hakuna mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hakuna ajira mpya, hakuna kupanda mishahara kwa watumishi wa umma, hakuna hata jiwe la msingi la Kiwanda kipya lililowekwa tokea Serikali ya awamu ya tano iapishwe, mzigo imepungua bandarini, magari makubwa ya mizigo yameamuriwa yapaki tu kwa kuwa sekta ya Usafirishaji imeuliwa, na maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu.

Hayo ndiyo mambo ya msingi ya Watanzania, chama chetu kitaendelea kuisimamia serikali katika mambo hayo Bungeni kama anavyofanya mbunge na Kiongozi wetu wa Chama.
Mwisho kabisa, tunapenda kujua kama haya aliyoyasema Ole Sendeka ndiyo msimamo rasmi wa Chama chake au ni maneno yake mwenyewe,maana kama ni msimamo wa chama chake,tutakuwa na mengine ya kusema.

"Taifa Kwanza, Leo na Kesho"

Habibu Mchange
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa
 ACT Wazalendo

Oktoba 29, 2016

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.