Wednesday, October 12, 2016

MKUTANO WA KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM SIMON SIRRO KWA WANANCHI WA KATA YA MBWENI ILIYOFANYIKA TAREHE 11.10.2016 MAJIRA YA JIONI.



Kamishna Sirro alizungumza na wakazi wa Mbweni maswala ya Ulinzi na usalama kuwa ni jukumu la kila mwananchi katika mtaa wao na kusisitiza raia wema waendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa za uhakika kuhusu uhalifu unaotokea, unaoendelea kutokea na unaotarajia kutokea.

Wakati huo huo alipata fursa ya kuongelea suala la magendo katika bandari bubu ya Mbweni ambayo imekaa katika fikra za wananchi wa maeneo hayo na kuwataka watafute kazi nyingine za halali ili kujipatia kipato badala ya kufanya kazi ambazo ni kinyume cha sheria za nchi yetu. 

Aliwaambia kukwepa kodi ni kosa la jinai na Jeshi la Polisi litashirikiana na TRA kuwakamata wale ambao hawatatii sheria.


Pia aliomba wananchi kushirikiana na jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu katika maeneo ya mbweni na kushirikiana katika suala la ulinzi katika mitaa yao kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya kata ya Mbweni ili kuzuia vitendo vya uhalifu na uhalifu unaoweza kutokea.

Aidha kamishna Sirro aliwaomba wananchi kushirikiana ili kumalizia kituo cha Polisi cha kata ya Mbweni ili kuondokana na kufuata huduma mbali katika kituo kikuu cha polisi wazo Hill.

Pia alizungumzia kuhusu vikundi vinavyotokea katika makanisa na misikiti kuwafundisha vijana mambo ya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwafundisha mafunzo kama ya JUDO, KARETI NA TAIKHONDO na kuwaachisha shule. Wenye tabia kama hizo waache mara moja, polisi wanafuatilia suala hilo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watakaobainika .

Kamishna wa kanda maalum Dsm pia alipokea kero mbalimbali kuhusiana na askari ambao sio waaminifu wamekuwa wakiwabambikizia wananchi kesi na kudai rushwa amesema atafuatilia suala hilo na watakaobainika atawachukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Mwisho mkutano uliahirishwa na kamishna alitoa namba za simu za dharura(111 na 112) ili wananchi waweze kutoa malalamiko yao kupitia namba hizo na kutoa taarifa za kihalifu na uhalifu katika maeneo yao.

S.N.SIRRO - CP
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM


No comments: