Tuesday, October 25, 2016

SERIKALI KUZIBA PENGO LA WAHADHIRI WAANDAMIZI NCHINI

mkan3
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia kwenye kilele cha Maadhiisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam  kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Waziri Mkuu ataka vyuo viweke utaratibu bayana wa kurithishana kazi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha
za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba
pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa lakini pia amevitaka
vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi
(succession plan).

Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na
masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na
maprofesa kuwa miaka 70.

mkan4
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha  Kitabu Kiitwacho  From Lumumba  Street to the Hill and Beyond baada ya kukizindua katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es salaa baada ya kuhutubia kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa CHuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Rwekaza Mukanda  na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt Leonard Akwilapo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga
kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K.
Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa
wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa
taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu
nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba
kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za
kutosha kwa ajili ya mafunzo,” amesema.

“Lakini vyuo vya elimu navyo havina budi kuweka taratibu na mipango
endelevu ya kurithishana (kuachiana nafasi) ‘Succession Plan’. Jambo
hii ni muhimu sana kwani bila hivyo, wakati wote kutakuwa na pengo
kubwa katika utoaji wa taaluma,” amesisitiza.

mkan2Amesema Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa
mipango hii ya kuwa na watalaamu wa kutosha katika vyuo huku
ikiendelea kutekeleza majukumu ya kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi
wapya pale wanapohitajika.

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi
wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za
kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.

“Hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa,
limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya
zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa
Serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.

“Ninafahamu kuwa yapo madai mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya
mishahara kwa watumishi hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja
wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma. Serikali inaendelea na
maboresho na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia
bodi ya mishahara na motisha; na mara tutakapokamilisha, tutapanga
upya mishahara na motisha kwa watumishi,” amesema.

Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu
amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa
mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo
wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya
mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh.
bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.

Mapema, akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55,

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho
kinakabliwa na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani
mbalimbali.

“Chimbuko la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za
umma kwenye miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa
miaka mingi, kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana
uzoefu baina ya wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua
nafasi zao,” amesema.

“Hali hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu
wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi
karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na
hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika
ngazi za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.

Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kuwadhamini
wahadhiri chipukizi ambao wako sehemu mbalimbali wakipata mafunzo. Pia
amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga
hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,800 na hivyo
kutarajiwa kupunguza tatizo la malazi.

Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi
cha sh. bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye
chuo hicho zikiwemo maabara.

No comments: