Wakati msimu mpya wa korosho 2016/17 kufunguliwa
rasmi Septemba mosi mwaka huu bado baadhi ya wakulima wameendelea
kulalamika kutolipwa malipo yao ya korosho kwa msimu uliopita 2015/16.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na
mbunge wa jimbo la Ndanda,Cecil Mwambe katika kata ya Chikukwe kwaajili
ya kuwashukuru wapiga kura wake baadhi ya wakulima walidai kuwa bado
wanadai malipo yao ya tatu kwa msimu uliopita hali inayowavunja moyo.
Akiuliza swali Hashim Abdullah alidai msimu mpya wa ununuzi
wa korosho umeanza rasmi lakini bado hawajalipwa pesa zao hali
inayowatia hofu.
"Tunataka kufahamu tunapokuwa na matatizo yetu
tuyawasilishe wapi , kuna matatizo mengine hatujui pa kuyapeleka mfano
malipo ya tatu ya korosho kwa msimu uliopita mpaka sasa kuna watu ambao
bado hawajalipwa na hawajui hatima yao na msimu mpya umeanza tayari
tunapata hofu je zitalipwa kwasababu bodi nyingine za vyama vyama msingi
zilivunjwa ,"alihoji Abdullah
Akizungumzia madai hayo mbunge wa jimbo la Ndanda, Cecil
Mwambe alisema madai ya baadhi ya wakulima kutolipwa malipo yao
anayafahamu na kwasasa unafanyika ukanguzi ili watakaobainika kudhulumu
pesa za wakulima waweze kuchukuliwa hatua.
"Haya madai yapo hata waziri alipokuja aliagiza wakulima
walipwe haki zao, na haikuishia hapo aliagiza ufanyike ukaguzi katika
vyama vyote vya msingi na wale watakaobainika kudhulumu jasho la mkulima
wachukuliwe hatua,"alisema Mwambe
Hata hivyo alimtaka rais kuichukulia hatua bodi ya korosho
nchini (Cbt) kwa kile alichiokidai ni kuwa na matumizi mabaya ya ofisi
na kuomba wafanyiwe ukaguzi wa mahesabu.
"Kama bodi ya korosho ingekuwa inatekeleza majukumu yake
ipasavyo hata malalamiko ya wakulima yangepungua lakini bodi ambayo
iliundwa kwa lengo la kusaidia wakulima wanajijali wao zaidi kuliko
mkulima ambaye amesababisha iundwe..haiwezekani wakulima mpaka leo
wanadai madai yao ya miaka ya nyuma lakini bodi wanakaa vikao vya wadau
wa korosho na kulipana 1.5 milioni kama posho, "alisema Mwambe
Aidha alisema viwanda vingi vya kubangulia korosho vimeuzwa
kwa watu wanaovitumia kama maghala ya kuhifadhia mazao hasa korosho
jambo ambalo linakosesha ajira.
Naye kaimu mtendaji wa chama cha msingi Chamwali,Omary
Mkudile alipotakiwa kueleza juu ya uwepo wa madai ya wakulima katika
chama chake alikiri ni kweli chama chake kinadaiwa pesa za wakulima
kiasi cha 51 milioni zikiwa ni malipo ya tatu.
"Ni kweli katika chama chetu bado tunadaiwa kiasi cha Sh 51
milioni ambazo ni malipo ya tatu ya wakulima kwa msimu wa mwaka 2015/16
,"alisema Mkudile
Hivi karibuni naibu waziri wa kilimo, Uvuvi na
Mifugo,William Ole Nasha alifanya ziara katika wilaya ya Masasi na
kueleza kuwa pesa za wakulima zaidi ya Sh 4 bilioni zimepotea huku
asilimia hamsini ya pesa hizo zikiwa ni za wilaya ya Masasi pekee.
No comments:
Post a Comment