Kampuni ya nishati ya jua ya jijini Dar es Salaam inayojulikana kama Paraa
Mwanga Limited imezindua rasmi kampeni ya “Kuangaza Afrika.” Paraa Mwanga
imezindua kampeni hiyo yenye lengo la kuleta mwanga katika nyumba za vijijini
kupitia vifaa vya ubora wa juu vya nishati ya jua ikishirikiana na kampuni ya
Indian Electronic na kampuni ya USA Electro mechanical.
Kampeni hiyo ambayo iko wazi kwa umma itawezesha familia nyingi kuweza
kushinda vifaa vya ubora wa juu vinavyotumia nishati ya jua zikiwemo taa za
mfumo wa LED, redio za FM, chaja za simu za mkononi na betri, vifaa vya kutengeneza
umeme jua (solar panels), televisheni, ving’amuzi, majiko ya kutumia gesi na
bima za afya ya jamii kila wiki.
Bi. Neela Krishnamurthy, Mkurugenzi mkuu wa Paraa Mwanga akionyesha Baadhi ya Solar zao wanazosambaza ambazo zina Ubora wa aina yake |
Shindano hili litafanyika kuanzia Novemba 2016 hadi Februari 2017 na
linategemewa kufikia vijiji zaidi ya 6,000 katika kampeni hii itakayopita
katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Lindi, Mbeya, Iringa, Mwanza
na Arusha. Watakaovutiwa kushiriki wanashauriwa kujiandikisha kwa kutuma TZS
500, kwenda kwenye namba ya Airtel
money 28668.
Bw. Said A. Shamo, Mwenyekiti wa Paraa Mwanga na Mwakilishi wa Baraza la Djibouti nchini Tanzania akizungumza wakati wa Uzinduzi huo Jijini Dar es salaam
|
Akizungumza katika mkutano na waandishi, Bi. Neela Krishnamurthy, Mkurugenzi
mkuu wa Paraa Mwanga, alisema, “Tunajivunia kuweza kufanya promosheni ya vifaa
vya LED na umeme jua katika vijiji vya Tanzania. Mahitaji ya nishati ya umeme
ni makubwa kuliko uzalishaji na hivyo kupelekea asilimia kubwa ya vijiji
kutokuwa na umeme. Bado kuna njia ndefu katika kufikia wale ambao hawafikiwi na
mtambo wa nchi wa umeme. Ni lengo letu kuwa katika miaka miwili ParaaMwanga
itaweza kuleta mwanga katika nyumba milioni moja nchini Tanzania.”
Bi. Krishnamurthy aliendelea kusisitiza kuwa katika mikoa mingi nchini
shughuli za kibishara nyakati za usiku zinakuwa hazipo. Wanaume na wanawake
wanashindwa kutumia muda wao kujiendeleza kiuchumi na watoto wanashindwa
kujisomea wakati wa usiku. Vilevile, matumizi ya taa za mafuta ya taa na
mishumaa ni gharama na sio salama kwa afya. “Nishati ya jua ndio suluhisho ya
changamoto hizi na kupitia kampeni hii tutapatia nyumba, vijiji, shule na vituo
vya afya vilivyopo vijijini fursa ya kuweza kupata vifaa bora kabisa vya
nishati jua kutoka India ambavyo wanaweza kuvitumia katika maisha yao yote,”
aliongeza Bi. Krishnamurthy.
Mteja wa kwanza kabisa Kutumia Bidhaa za Paraa Mwanga Bwana Colonel Mkami kutoka Jeshi la wokovu Tanzania akitia ushughuda Kuhusu ubora wa Bidhaa hizo leo Jijini Dar es salaam |
Shindano hili ambalo limeshaanza litakuwa na droo za aina mbili kwa
wiki, katika droo moja ya kawaida washindi kumi watazawadiwa vifaa vya nishati
jua vya nyumbani vikiwemo, paneli za nishati jua (solar panels), betri na
kidhibiti chake, taa za aina ya LED 3, redio ya FM na chaja ya simu. Kila wiki
washindi kumi watazawadiwa ushindi wa draw hii.
Droo ya aina ya pili mshindi mmoja atapatiwa zawadi yenye taa za aina
ya LED 4, redio ya sola inayotumia remote control na kifaa cha kusomea (flash
reader), chaja ya simu na betri. Washindi hawa pia watapata televisheni ya
inchi 24 ya aina ya LED, king’amuzi kilichounganishwa mwaka mmoja, jiko la
gesi, feni na bima ya afya ya jamii. Kila wiki mshindi mmoja atajipatia zawadi
ya draw ya pili.
Baadhi ya Solar zinazosambazwa na Para Mwanga na jinsi zinavyoweza kufanya kazi mbalimbali ikiwembo kuwasha Televission,Radio,Kucharge Simu,na huduma mbalimbali. |
Pamoja na washindi wa wiki ambao watapatiwa vifaa vya nishati jua, pia
makusanyo yatakayopatikana katika kampeni hii yatatumika katika kuweka mwanga
katika vijiji vitakavyochaguliwa bure.
“Kutokana na mafanikio yatakayopatikana katika kampeni hii, asilimia
kadhaa ya makusanyo yatapelekwa katika vijiji katika mikoa ya Kigoma, Katavi,
Kagera na Rukwa. Hii ni mikoa ambayo ina tatizo kubwa la kutokuwa na nishati ya
umeme. Kwa kushiriki katika kampeni hii wote tutakuwa tunachangia katika kuleta
mwanga na matumaini katika familia maeneo ya vijijini Tanzania,” alimalizia Bw.
Said A. Shamo, Mwenyekiti wa Paraa Mwanga na Mwakilishi wa Baraza la Djibouti nchini
Tanzania.
Wadau katika uzinduzi huo |
No comments:
Post a Comment