Wednesday, November 2, 2016

MUSWADA WA HABARI WAELEZEWA KUWA MUAROBANI DHIDI YA KASHFA NA UCHOCHEZI.


Na: Mwandishi Wetu.
MUSWADA wa huduma za Habari wa mwaka 2016 umeelezewa kuwa muarubani wa uandishi wa habari za kughushi na uchochezi kutokana na kuwa na vifungu vyenye kumlinda mwandishi na kumuweka hatiani pindi anapoenda kinyume na matakwa ya sheria.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Kurgenzi ya Mawasiliano wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Bernard James wakati wa  mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii leo Jijini Dar es Salaam.

“Baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa na tabia za kandika habari za kughushi na mara nyingine zenye lengo la kumkashfu mtu, ni imani yangu kwamba muswada huu ni muafaka kwa watu kama hao”. Alisema Bernard.


Bernard alivitaja vifungu hivyo kuwa ni Sehemu ya Tano ya muswada huo kuanzia kifungu cha 32 hadi 39 ambavyo vinahusu mambo ya kashfa ambapo mwandishi ana anayo haki yake,  hali kadharika anao wajibu wa kuzingatia misingi ya sheria na mipaka yake.

Huku sehemu ya saba ikihusisha makosa mbalimbali yakiwemo uchochezi,habari za kuchochea uasi, makosa yanayohusu utangazaji, vyombo vya habari na kosa la habari za kutia hofu kwa jamii.

Alisema kuwa ni vyema wanahabari wakatambua kwamba Serikali imeleta muswada huo si kwa nia ya kukandamiza uhuru wa habari bali ni nia yake yakutaka kuona kunakuwa na maboresho katika tasnia  ya hii na siyo kama ambavyo wengi wao wamekuwa wakipotosha.

Aidha Bernard aliongeza kuwa muswada huo ukipitishwa utapelekea kuanzishwa kwa chombo kitakachosimamia waandishi wa habari kwa kuwapa Vitambulisho, kusimamia  maadili na mienendo ya taaluma za waandishi wa habari na kuongeza kuwa tasni itaheshimika kwani wale makanjanja hawatakuwa na nafasi tena.

“Binafsi naunga mkono muswada huu upitishwe ili tasnia ya habari iheshimike kama taaluma nyingine zinavyoheshimika”.Aliongeza.

Amewaomba wanahabari wenzake kuunga mkono Muswada huu unaotarajiwa kusomwa Bungeni kwa mara ya pili siku ya Ijumaa ya tarehe 4 Novemba ambapo utajadiliwa na kupitihwa.

MWISHO

No comments: