Thursday, November 10, 2016

VIJANA WATANO WACHAGULIWA MAJARIBIO YA AZAM FC U-17 ZANZIBAR


KAMA ulimisi taarifa ya majaribio ya wazi ya mwisho ya Azam FC kwenye msako wa kusaka vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) yaliyofanyika Visiwani Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa rasmi ni kuwa tulifanikiwa kuwachagua vijana watano kutoka visiwani humo, ambao wameingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika mwezi ujao makao makuu wa Azam Complex, yatakayohusisha vijana wote waliochaguliwa kwenye mikoa mbalimbali.
Vijana hao watano wanaungana na wengine 37 waliochaguliwa kwenye maeneo tofauti nchini katika mikoa ya Morogoro (12), Dar es Salaam (13), Tanga (12) na kufikisha idadi ya vijana 42 waliochaguliwa mpaka sasa kati ya vipaji 2,143 waliofanyiwa usaili.

Uongozi wa Azam FC kwa kushirikiana na idara ya ufundi ya timu hiyo, una nia dhati ya kuboresha mfumo wa kituo chake cha kukuza vipaji 'Azam FC Academy' ili kihusishe vijana wa umri tofauti kwa ajili ya kuvuna vipaji vingi zaidi kwa manufaa ya baadaye ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla.


Hadi sasa Azam FC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye uleaji wa vipaji katika kituo hicho, ikivuna vijana kadhaa wanaotamba sehemu tofauti katika timu mbalimbali nchini, wengine wakiwa wanaing'arisha timu kubwa ya kituo hicho.
Baadhi ya waliopandishwa kwenye timu kubwa ni makipa Aishi Manula, Metacha Mnata, mabeki Ismail Gambo, Gadiel Michael, Abdallah Kheri (mkopo Ndanda), viungo Mudathir Yahya, Masoud Abdallah, Bryson Raphael (mkopo Ndanda).

Wengine ni Joseph Kimwaga (mkopo Mwadui), Farid Mussa (aliye mbioni kujiunga na CD Tenerife - Hispania), wshambuliaji Kelvin Friday (mkopo Mtibwa Sugar) na Shaaban Idd.

Wanaotamba na timu nyingine baadhi yao ni Simon Msuva (Yanga), Mohamed Hussein (Simba), Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Joseph Mahundi (Mbeya City), Jamal Mnyate (Simba).

FURSA YA MWISHO ADIMU KWA VIJANA U-17 DAR, SASA KUJARIBIWA KESHOKUTWA

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuendelea na mpango wake wa Kitaifa wa kusaka wachezaji chini ya umri wa miaka 17 (U-17) Jumamosi ijayo Novemba 12 mwaka huu kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 9.00 alasiri ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Baada ya wikiendi iliyopita kufanya majaribio ya wazi visiwani Zanzibar, ambako walichaguliwa wachezaji watano, sasa tunarudisha mkazo wetu Tanzania Bara na kufanya majaribio ya mwisho katika jiji la Dar es Salaam.
Kwa majaribio mengine ya wazi katika maeneo mengine kuzunguka Tanzania yatatangazwa hivi karibuni.






No comments: