Friday, December 16, 2016

WAZIRI MWAKYEMBE ATEMBELEA UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA KIGAMBONI

Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga mahakama za mwanzo katika kila kata nchini ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo alipotembelea ujenzi wa Mahakama ya kisasa ya Wilaya Kigamboni inayojengwa kwa kutumia teknolojia ya Moladi ambayo inapunguza muda na gharama za ujenzi ambayo inagharimu kiasi cha shilingi milioni 572 na  ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2017.
Waziri Mwakyembe amesema moja ya kipaumbele cha Wizara yake ni kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi hivyo huduma za kimahakama zitaendelea kuboreshwa na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema anaishukuru Serikali kwa kujenga Mahakama ya kisasa Kigamboni na hivyo kusogeza huduma kwa wananchi na pia ameipongeza Serikali kwa kuanzisha mchakato wa kutunga Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ambayo itasaidia sana wananchi wa kipato cha chini.


Aidha, Mhe. Ndugulile ameomba changamoto za ucheleweshwaji wa kesi Mahakamani na rushwa ziweze kutafutiwa ufumbuzi maana ni miongoni mwa kero zinazowakabili wananchi.

No comments: