Sunday, January 22, 2017

TAARIFA MPYA KUHUSU UFAFANUZI WA ALIPO ZITTO KABWE SASA

Kiongozi wa ACT Wazalendo hajakamatwa na Polisi Kahama


Taarifa kwa Wanachama na wananchi wote

Tunawajulisha kuwa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe, Mb hajakamatwa na polisi na yupo salama hapa hapa nchini.
Jana tarehe 21/1/2017 Polisi wilayani Kahama wakiwa na magari 7 Kati Yao 4 ya FFU na mabomu ya machozi walivamia Mkutano wa Kampeni wa Chama katika kata ya Isagehe, Halmashauri ya Mji wa Kahama.

 Kiongozi wa Chama alikuwa jukwaani wakati polisi wanafika na aliendelea na hotuba yake mpaka mwisho na kumnadi Mgombea ndg Ibrahim Masele.
 Baada ya kushuka jukwaani, Kama kawaida yake KC alipeana mikono na wananchi na baadaye alipotea katika eneo Hilo.

Polisi waliingia mkutanoni na kuanza kumtafuta KC lakini hawakuweza kumpata na hivyo kumkamata dereva wa gari alilokuwa anatumia KC ndg Patrick Muhidin pamoja na katibu wa Chama Wa jimbo la Kahama.


Wote walipelekwa kituo cha polisi Kahama na kuandikishwa maelezo, gari hiyo Landacruiser V8 imeshikiliwa na polisi mpaka sasa.

Mnamo saa mbili na dakika 2 usiku Polisi walivamia makao makuu ya kampeni ya Chama na kufanya upekuzi mkubwa wakimtafuta KC bila mafanikio. Baadaye waliweka mazuio ya njia zote za kutoka Kahama wakiamini kuwa KC atakuwa anapanga kutoroka na kutoka nje ya Kahama.

Tunapenda kuwajulisha kuwa KC yupo salama na yupo Kahama anasimamia ushindi wa kura. Amewaeleza viongozi wa Chama kuwa Polisi wataweza kumkamata iwapo yeye atataka kukamatwa na sio kwa kuvamiwa bali kwa kuitwa rasmi polisi na kuelezwa makosa aliyoyafanya.

Chama kimefuatilia kujua ni kwanini polisi wanamtafuta KC. Tumejulishwa na polisi kwamba KC Ana mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi katika hotuba zake za kampeni katika kata ya Isagehe Jimbo la Kahama Mjini. Polisi wanasema KC amemchonganisha Rais na wananchi kwa kusema kuwa Rais anakula bure na kulala bure Ndio maana hajali hali ngumu ya Maisha ya wananchi wakati huu wa balaa la njaa.

Chama kinalitaka jeshi la polisi kufuata taratibu za kukamata raia kwa mujibu wa sheria na pia protokali za kuwaita polisi viongozi wa Kitaifa Kama ilivyo kwa ndg Zitto. Chama kinajiandaa na wanasheria wake ili kwenda na KC kituo chochote cha polisi nchini Mara watakapopata wito wa kwenda polisi.

Chama chetu kitaendelea kukosoa vitendo vya serikali vinavyoenda kinyume na sheria na desturi ya demokrasia ya Tanzania. Wito wetu ni kwa Serikali kuachia vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani kufanya kazi zao bila bugudha na kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu.

Kiongozi wa Chama anawataka wanachama wote wa ACT Wazalendo kuishi kwa mujibu wa Ahadi 5 za mwana ACT Wazalendo na kusimama kidete kulinda demokrasia ya vyama vingi nchini ambayo ipo hatarini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwaka 2015.

Msafiri A Mtemelwa
Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo

No comments: