Monday, January 2, 2017

ZAHOR: ASANTE PRESIDENT, ILA….


untitled-k
KIUNGO mshambuliaji mpya  wa Mbeya City fc , Zahor Pazzy  amemshukuru rais wa shirikisho la kabumbu nchini Jamal Malinzi kwa kufanikisha  kupatikana kwa hati yake ya uhamisho (ITC)  iliyokuwa imekwama  nchini DR Congo kwa miaka  miwili.
Akizungumza na mbeyacityfc.com mara baada ya kumalizika kwa mazoezi asubuhi ya leo kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, Zahor amesema kuwa anafuraha kubwa kuona amerudi rasmi kwenye  ulimwengu wa soka baada ya kukaa nje  kwa miaka miwili,  licha ya jitihada kubwa alizokuwa akizifanya.

Namshukuru Mwenyezi Mungu, hakika natanguliza sifa kwake, nimekuwa nje ya soka la ushindani kwa miaka miwili sasa, mara kadhaa nimejaribu kufanya jitihada za kuhakikisha naokoa kipaji changu lakini sikufanikiwa, namshukuru rais wa TFF amefanikisha  ndoto zangu za kuendelea kucheza mpira, niseme wazi  kuna wakati nilikata tamaa kabisa, ingawa pia niliendelea kujipa moyo na kumuomba Mungu, nashukuru sasa niko huru na naweza kuitumikia timu yangu mpya, alisema.
Akiendelea  zaidi Zahor alisema  anawashukuru viongozi wa Mbeya City  Fc kwa kumpa nafasi ya kuitumikia timu hii licha ya kutokuwa kwenye soka la ushindani kwa muda mrefu.
Nawashuruku viongozi wa mbeya city, wameniamini na  wamenipa nafasi  ya kujiunga na timu licha ya kutokucheza kwa muda mrefu, najua sitakuwa na miujiza ila nitajitahidi kutumia uwezo wangu wote niliojaaliwa na Mwenyezi muMungu na kwa kushirikiana na wenzangu naamini tutaifikisha mbali timu yetu, alisema Zahor na kuongeza kuwa anaimani kubwa City itaibuka na ushindi dhidi ya Mbao Fc  jumamosi kufuatia mazoezi mazuri yaliyofanyia leo.  Aidha Zahor  ametoa  wito kwa wachezaji wenzake kuwa makini katika hatua zote zinazohusu  usajili na uhamisho  pale wanapohitaji  kutoka timu moja kwenda nyingine.
Kwa wachezaji wenzangu kikubwa tuwe makini, nafahamu kuwa mara nyingi huwa tuna kiu kubwa ya kucheza nje, kila mmoja ana ndoto hizo  ni vyema kuangalia na kufanya mambo kwa makini, yaliyonikuta mimi  sikuyapanga ila kuna njia ambazo zilitumika ndivyo sivyo mpaka ikafika hapo ilipofika  hivyo ni vyema kuwa na watu makini na madhubuti ambao wanaosiamamia mambo yetu, alimaliza. 

No comments: