ZINGATIA HAYA ILI KUREJESHA ARI YA KUFANYA KAZI BAADA YA LIKIZO

Na Jumia Travel Tanzania

IWAPO unazitambua vizuri barabara za jiji la Dar es Salaam, basi utagundua kwamba kuna tofauti kubwa kwenye msongamano wa magari ukilinganisha na kipindi cha sikukuu. Hali hiyo imetokana na idadi kubwa ya watu kurejea jijini kuendelea na shughuli za kazi, ambapo wengi walikuwa kwenye likizo na mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Mwezi Januari ni mgumu sana miongoni mwa watu wengi wanaorudi maofisini kutokana na uchovu uliotokana na mapumziko ya kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka. Hivyo huwawia ugumu wengi wao kuendana na mazingira ya kazi ambayo huyaona ni mapya kutokana na kulewa starehe za mapumziko.

Zifuatazo ni mbinu chache ambazo Jumia Travel (www.travel.jumia.com) inakushauri kuzifuata ili kuhakikisha unarudisha mawazo na ari yako kazini kama ilivyokuwa awali.

Tegesha ‘kengele kwenye saa’ ya kukuamsha mapema asubuhi

Najua kwamba kipindi cha mapumziko watu huamka muda wanaoutaka bila ya wasiwasi wa kuwahi ofisini. Kutokana na sababu hiyo huwa hakuna haja ya kutegesha kengele kwenye saa ya kukuamsha asubuhi, basi kama ulifanya hivyo sasa huna budi kuirudisha ili uweze kuwahi shughuli zako.

Anza kwa kumalizia ‘viporo’ ulivyovibakisha

Sio watu wote wanaoenda likizo wanakuwa wamemaliza kazi zao za ofisini, kwani huwa haziishi hata hivyo. Kwa hiyo, pindi unaporudi ofisini kitu cha kwanza ni kuhakikisha kwamba unamalizia viporo vya kazi vyote ulivyoviacha ili kuuanza mwaka na majukumu mapya. 

Ulizia kwa wafanyakazi wenzako kazi zilizofanyika wakati wewe hukuwepo

Haimaanishi wewe ukiwa mapumzikoni kwamba kazi haziendelei ofisini. Ni muhimu kuulizia kazi zilizofanyika wakati wewe haupo ili uende sawa na wenzako au kufahamu yapi ni majukumu yako.

Fanya mazoezi ili kuweka mwili na akili yako katika hali nzuri

Mazoezi ni tiba kubwa sana kwa afya ya mwili na akili, hii itakufanya urudi katika hali yako ya kawaida ili kufanya kazi kama kawaida. Unaweza kufanya mazoezi asubuhi au baada ya kumaliza shughuli zako jioni pindi unaporudi nyumbani. Mazoezi yanaweza kufanyika katika vituo maalumu vilivyowekwa au kwa kukimbia au kutembea pembezoni mwa barabara.
  
Jifanyie tathimini kwa uliyoyatimiza mwaka uliopita

Kipindi unachotoka mapumzikoni kinafaa kutumika kwa kufanya tathimini juu ya yale uliyoyatimiza mwaka uliopita. Kwa kufanya hivyo utajua kama ulifanikisha malengo uliyojiwekea au kutoyatimiza ili kuweka mikakati thabiti kwa mwaka huu unaoanza.

Omba ushauri 
Wakati mwingine inakuwa ni vigumu kwa uwezo na utaalamu tulionao katika kukabiliana na mabadiliko katika miili yetu. Hivyo tunashauriwa kuomba msaada kutoka kwa wakuu wetu wa kazi kutokana na uzoefu walionao, kwa sababu wao pia walipitia na wanaifahamu hali hiyo. Lakini pia kuwaona wataalamu wa afya kwa ajili ya ushauri zaidi ni muhimu.

Zipo mbinu kadhaa za kukabiliana na hali ya uchovu au kutokujisikia kufanya kazi baada ya kurudi kutoka mapumzikoni. Jumia Travel (www.travel.jumia.com) inakushauri kuzifuatilia hizo chache kwani zitakusaidia sana ili usiharibu kazi kwani ndio msingi wa maisha na Taifa lolote katika kuleta maendeleo. 

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.