ZITTO KABWE ATANGAZA KUMSHAKI RAIS JPM ENDAPO MTANZANIA HATA MMOJA ATAKUFA KWA NJAA

Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha ACT WAZALENDO na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akiwasili katika kata ya Kijichi ambapo kulikuwa na Kampeni ya kumnadi mgombea wa chama hicho kwenye kata hiyo Bwana Edga  Mkosamali anayewania kiti cha Udiwani katika kata hiyo kwa Tiketi ya ACT WAZALENDO ukiwa ni uchaguzi Mdogo baada ya Diwani wa chama hicho Kutoka chama cha mapinduzi Kufariki Dunia.Zitto Kabwe ametumia Hadhara Hiyo kuzungumza na watanzania maswala mbalimbali yanayoendelea nchini .Unaweza kufwatilia Hotuba yake hapo chini
Watanzania wakifa njaa tutamwajibisha Rais kwa mujibu wa Katiba ibara ya 46A

(Sehemu ya Hotuba ya Kiongozi wa Chama katika Mkutano wa Kampeni za Udiwani - Kijichi) 15/1/2017
Pamoja na masuala haya ya uchaguzi mdogo hapa Kijichi ninaomba nizungumzie masuala machache ya kitaifa. Nafanya hivi kwa sababu baada ya siku saba hatutakuwa tena na nafasi ya kuzungumza majukwaani kama viongozi wa vyama vya siasa kwa sababu ya zuio lisilo la kikatiba ambalo limewekwa na Rais dhidi ya mikutano ya hadhara. Hivyo, sisi tuliamua kutumia majukwaa haya ya kampeni za uchaguzi mdogo kuzungumzia mambo ya kitaifa pia. Hatujui chaguzi ndogo nyengine zitakuja lini.

Tulitumia mikutano hii ya kampeni kuelezea hatari ya njaa ambayo inaikabili nchi yetu hivi sasa. Nikiwa katika kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro nilieleza kuhusu kupanda kwa bei za vyakula na kiwango kidogo cha akiba ya chakula kwenye maghala ya Taifa (NFRA).
Tunashukuru kwamba suala hili limekuwa ni ajenda ya Taifa hivi sasa na tunawapongeza sana viongozi wetu wa dini kwa kutoa matamko ya kuhamasisha watanzania kuliombea Taifa kuepukana na adha ya njaa. Viongozi wa dini wameonyesha utu na uwezo mkubwa wa uongozi wa kutafuta jawabu la mwenyezi mungu kuhusu adha hii.

Serikali kupitia kwa Rais imewaambia watanzania kuwa hali ni shwari kabisa na kwamba Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa sababu "Mzee Bure" ameshatoka madarakani. Lakini Rais pia alituhumu wanasiasa na wafanyabiashara kwamba ndio wanachochea hali ya njaa kwa kupitia vyombo vya habari kadhaa. Na akaenda mbali zaidi kwa kufikia hatua ya kutisha vyombo vya habari na kusema siku zao zinahesabika, kosa lao kubwa likiwa ni kuandika yale ambayo yeye hayapendi.
Sisi ACT Wazalendo tunamsihi Rais awe msikivu. Hii ni nchi ya kidemokrasia na watu wana uhuru wa mawazo. Haiwezekani kila mwenye mawazo tofauti awe ni mtu anayehongwa au mpiga dili. Kazi yetu sisi kama chama cha upinzani ni pamoja na kuikosoa Serikali iliyopo madarakani na kuonyesha sera mbadala kwa wananchi.
Tutaendelea kuichokonoa Serikali mpaka ianguke, maana ndio kazi yetu ili kuondoa sera mbovu zilizopo na kuweka sera bora.
Tumesema hili la njaa katika kutekeleza wajibu wetu, Rais na Serikali wamejibu na kufunga mjadala. Wakati utaamua na kuonyesha mkweli nani na mpiga propaganda nani.

Jambo moja ni muhimu sana, Rais anapaswa kujua kuwa anafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Na Katiba imetoa wajibu wa lazima kwa Serikali kulinda watu. Ndio kazi ya Serikali – kulinda wananchi pale ambapo yanatokea majanga ambayo yanazidi kimo wananchi hao.
Tunamwambia Rais kwamba, Mtanzania yeyote akifa kwa njaa kwa sababu Serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake Watanzania tutapaswa kuchukua hatua, Katiba inatulazimisha kumtoa Rais madarakani ikiwa yeye na Serikali yake watashindwa kutimiza wajibu wake wa kulinda uhai wa raia wake.
Tunamkumbusha Rais kuwa yeye sio mungu mtu. Yupo chini ya Katiba na kwa idadi ya wabunge wa upinzani waliopo Bungeni, na wakiamua kusimama na wananchi na kulinda Katiba, Rais wa sasa atakuwa Rais wa kwanza wa nchi yetu kutolewa hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni. Katiba inahitaji asilimia 20 tu ya wabunge kuwasilisha hoja hiyo bungeni.

Ninatoa wito kwa Watanzania wote nchini, bila kujali vyama vyao, kuweka rekodi ya hali ya chakula popote walipo na kuweka takwimu ya maafa yeyote yanayotokana na njaa. Mtanzania yeyote akifa kwa njaa ni lazima tuchukue jukumu la kumwajibisha Rais kwa kusema waziwazi kwamba hajatimiza wajibu wake kama Mkuu wa Serikali kulinda wananchi wake.
Tunamkumbusha Rais kwamba kwa mujibu wa ibara ya 46A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yeye amekula kiapo kuilinda, kuihifadhi na kuitetea, Bunge laweza kumshataki yeye Rais kwa kosa la mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais.
Wananchi wanaona lugha za ubabe, vitisho, kuonea watu, kudhihaki waliopatwa na majanga kwamba ni mambo yanayodhalilisha kiti cha Rais. Hivyo Rais achague maneno ya kusema mbele ya wananchi wake, atumie lugha ya kujenga matumaini badala ya kujenga hofu kwenye jamii, aache kuonea watu kwa kutumia madaraka yake, na akumbuke cheo ni dhamana.

Tunayasema haya kwa Uzalendo mkubwa kwa nchi, sisi kama chama, ACT Wazalendo, tulimwunga mkono Rais toka mwanzo wa utawala wake na kumkabidhi Ilani ya uchaguzi ya chama chetu kama ishara ya kwamba uchaguzi umekwisha na sasa tujenge nchi yetu. Hatujutii kumwunga mkono kwa sababu kuna mambo mazuri amefanya kuhusu nchi yetu.
Rais amefanya kazi nzuri ya kupambana na rushwa na ufisadi nchini. ameondoa hali ya ‘impunity’ iliyokuwa imeshika mizizi nchini. Hatua kubwa alizochukua za kuwajibisha watendaji na Waziri aliyekiuka maadili ya kazi tunaziunga mkono.
Hata hivyo, nchi huendeshwa kwa zaidi ya kutumbua majipu. Kuna uchumi unapaswa kuendeshwa ili watu waweze kujenga maisha yao. Rais anaelekea kushindwa kwenye eneo hili la 'Menejimenti' ya Uchumi kutokana na matamko yake ambayo yanakimbiza uwekezaji na hata mahusiano yetu na mataifa mengine duniani.
Rais bado anahutubia kana kwamba bado tupo kwenye kampeni. Huu ni mwaka 2017, ni muhimu, ajielekeze katika kujenga uchumi wetu ili kutengeneza ajira kwa wananchi wake.

Vile vile, sisi tunaona Rais anahangaika na majipu madogo na kuacha majipu makubwa yanayoathiri uchumi wetu na kupoteza fedha nyingi sana za nchi yetu. Kwa mfano, Rais ameacha kabisa kushughulika na ufisadi mkubwa wa IPTL ambapo kila mwezi TANESCO inalipa shilingi bilioni 8 kwa kampuni ya kitapeli ya PAP. Moja ya sababu za TANESCO kutaka kupandisha bei ya umeme ni kwa ajili ya kupata fedha za kulipa PAP.
Rais amemfukuza kazi Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO akijua kuwa Mkurugenzi huyo alikuwa anatekeleza mpango wa Serikali. Barua ya Waziri wa Nishati na Madini kwenda kwa Waziri wa Fedha kuhusu kupandisha bei ya Umeme imenukuliwa kwa Rais. Hivyo Rais alikuwa anajua kuwa bei ya umeme itapanda na Serikali imeijulisha hivyo IMF katika barua yake ya Disemba 20, 2016, siku 10 kabla ya Tamko la EWURA la kupandisha bei ya umeme.
Jambo hili kubwa la IPTL ambalo lilihusisha mabilioni ya fedha kuchotwa Benki Kuu Rais analiacha na hataki kabisa kulizungumzia, maana yake ni kwamba Rais anaogopa wakubwa na kuonea wadogo, amemtumbua Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kwa sababu tu EWURA imetangaza bei mpya ya umeme ambayo Serikali yenyewe iliagiza kupandishwa toka mwezi Septemba mwaka 2016.

Lakini Rais huyu huyu anaendelea kutetea mkataba unaowalipa matapeli shilingi bilioni 8 kila mwezi. Rais wa wanyonge anawalinda matapeli wanaoiba fedha za umma.
Lingine ambalo Rais anaonyesha woga kwa wakubwa ni lile la mkopo wa Hati Fungani kutoka Benki ya Standard ya Uingereza. Serikali ilikopa dola milioni 600 mwaka 2013 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Licha ya mkopo ule kugubikwa na ufisadi katika upatikanaji wake, Serikali imeanza kuulipa na deni litakapokwisha baada ya miaka 6 itakuwa imelipa dola milioni 983.
Lakini sheria zote za kimataifa zinaibeba Tanzania kwamba kama mkataba na kampuni za kimataifa umepatikana kwa rushwa, nchi inaweza kukataa kulipa deni. Niliiambia serikali Bungeni kuhusu jambo hili na nimepeleka maswali kama manne bungeni kuhusu jambo hili lakini Serikali inaogopa hata kujibu maswali husika. Kwa sababu gani? Serikali inaogopa makampuni ya kigeni.
Najua kuna kesi mahakamani na sitaki kuingilia kesi hiyo. Lakini hiyo kesi iliyopo mahakamani na hao waliopo rumande ndio wangekuwa mashahidi wa Serikali kwamba Benki ya Standard ya Uingereza ilitoa rushwa kupata biashara nchini na hivyo Serikali ingeishitaki Benki hiyo na kukataa kulipa mkopo huo. Rais na Serikali yake hata kujibu maswali ya bunge wanaogopa. Sisi tunamtaka Rais ahangaike na mambo haya makubwa na aachane na watu wadogo. Rais ni mtu kubwa sana na akitumia ujasiri wake vizuri anaweza kuokoa nchi dhidi ya deni kubwa la kifisadi la Standard Bank ya Uingereza.
Lingine nataka kuongea nanyi ni suala la Bajeti ya Serikali na Utekelezwaji wake. Serikali ilileta Bungeni Bajeti ya matumizi ya shilingi 29.5 trilioni mwaka 2016/17. Katika hiyo, ilitarajia kupata mikopo na misaada kutoka nje pamoja na mikopo ya kibiashara ya shilingi 5.7 trilioni. Kutokana na mahusiano mabaya kati ya Serikali na nchi marafiki, mpaka sasa nusu ya mwaka wa Bajeti imekatika na Serikali haijaweza kupata hata thumni katika matarajio hayo. Vile vile Serikali imeanza kukusanya chini ya matarajio kwenye kodi na mapato yasiyo ya kikodi.
Miradi ya Maendeleo imechelewa kutekelezwa kwa sababu Serikali inafanya kazi ya kulipa mishahara na kulipa madeni tu. Ndio maana miradi mingi inayozinduliwa hivi sasa hakuna mradi mpya bali ni miradi iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Nne. Serikali hii inahitaji kurekebisha mahusiano yake na nchi marafiki zetu ili uchumi wetu usisimame. Masuala haya Rais hawezi kuambiwa na Mawaziri wake kwa sababu amejenga hulka ya kuogopwa. Sisi wa Upinzani ni lazima tumwambie maana ni wajibu wetu.
Katika Barua (letter of intent) ambayo Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu wameandika kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Serikali inasema inataka kukopa mikopo ya kibiashara (syndicated loans and Eurobond) ili kupata fedha. Hata hivyo Mabanki ya Dunia yanataka kujua 'Credit Rating' ya Serikali yetu.
Hiyo pekee itachukua miezi mingi iwapo mfumo wa kawaida wa zabuni utapaswa kufuatwa. Hata hivyo IMF wameiambia Serikali kuwa soko la mikopo ya dunia hivi sasa ni baya maana Serikali itakopa kwa gharama kubwa, mpaka riba ya 9% kwenye fedha za kigeni.
Serikali inataka kuiingiza nchini kwenye madeni ghali kwa sababu tu ya kutaka kufanikisha Bajeti isiyotekelezeka, iliyotungwa kwa sifa bila kuzingatia uhalisia wa nchi yetu. Kwa maoni yetu sisi ACT Wazalendo, Bajeti ya Serikali haikupaswa kuzidi shilingi 24 trilioni. Ushauri wetu kwa Serikali ni kuitaka ikae chini na kuleta Bajeti ndogo Bungeni ili kurekebisha Bajeti iliyoko kulingana na uwezo wetu kama Taifa ili kujiepusha na mikopo ghali itakayoumiza wananchi.
Serikali ilitangaza kuwa ujenzi wa Reli ya Kati ya kisasa utaanza mwezi Disemba mwaka huu kwa msaada kutoka nchi ya China. Leo ni mwezi Januari hata zabuni ya kampuni iliyoshinda kutekeleza mradi huo Serikali haijatangaza. Hata hivyo tumesikia kuwa kampuni kutoka Uturuki imeshinda zabuni hiyo na China (ambao ndio watoa mkopo wa mradi husika) wamekasirika na wamegoma kutoka fedha zao.
Tumesoma kwenye vyombo vya habari kuwa Rais wa Uturuki anakuja nchini wiki ijayo. Hatukatai kuimarisha mahusiano na Uturuki, lakini ni muhimu Serikali ijitazame upya kuhusu mahusiano yake na China. China ni rafiki wa Tanzania wa misimu yote. Tanzania imekuwa na China muda wote na China imekuwa na Tanzania muda wote. Maamuzi ya Serikali ya kutozingatia taratibu za China katika masuala ya mikopo yanaweza kugharimu sana mahusiano yetu ya zaidi ya miaka 50.
Tunamsihi Rais awe makini sana na mwenendo wake wa kutojali misingi imara ya Sera yetu ya mambo ya nje. Serikali ikae chini na China kutazama upya suala la Reli ya Kati vinginevyo hatutajenga Reli hiyo, ama itachukua miaka mingi sana kuijenga Reli hiyo. Madhara ya kuchelewa kujenga Reli ya Kati ni makubwa mno kwani washindani wetu wa kibiashara, Kenya, wanamaliza Reli yao sasa kuunganisha na nchi za Rwanda na Mashariki ya Kongo.
Namkumbusha Rais na Serikali namna ndani ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani walivyovunja misingi yetu kadhaa ya Sera ya Mambo ya Nje, hasa kuhusu Sahara Magharibi na Mashariki ya Kati. Tumeikumbatia Moroko kwa ahadi ya viwanja vya mipira na misikiti na kuwaacha wananchi wa Sahara Magharibi ambao Mwalimu Nyerere aliwalinda kwa gharama zote. Juzi juzi kwa mara ya kwanza tumewasaidia Israel kwenye Umoja wa Mataifa bila ya kujali msimamo wetu wa 'Two States Solution' kati ya Palestine na Israel.
Sasa tunakwenda kuweka nyufa kwenye mahusiano yetu na China. Serikali ijitazame upya. Tanzania haikuanza na awamu ya Tano, nchi hii imekuwapo na itaendelea kuwapo. Hatuwezi kukaa kimya tukiendelea kuona misingi ya nchi yetu inavunjwa vunjwa. Lazima tukemee.
Mwisho ni haya masuala ya Demokrasia. Juzi nilipokuwa Kahama nimezungumzia suala la ubinywaji wa demokrasia na kuwaweka ndani wawakilishi wa wananchi kwa makosa yanayodhaminika. Nilionya kuhusu tabia ambayo imeanza ya kuitumia mahakama kutekeleza matakwa ya kisiasa ya Serikali.
Wakati mbunge wa Arusha Mjini bado angali kizuizini, Mbunge wa Kilombero amehukumiwa kwenda jela miezi 6 kwa kosa ambalo lina adhabu ya faini. Kuna maamuzi ya mahakama ya rufaa kuhusu kwamba kosa lenye faini, faini ndio adhabu stahili na sio kifungo. Lakini kwa kuwa lengo ni kukomoa wanasiasa wa upinzani Mbunge wa Kilombero ameswekwa jela.
Narudia kutoa wito kwa Serikali kuwa makini sana na chuki inazozijenga kwa wananchi kutokana na uonevu huu. Ninaamini kuwa vyama vya siasa vyenye wabunge hao pamoja na taasisi za kutetea haki zitashiriki kikamilifu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya matendo yanayoendelea nchini mwetu hivi sasa.
Tusiache kuinua mikono yetu kupinga uonevu kwa sababu uonevu wa dola ni mtego wa panya. Tukemee kabla hatujafikiwa pia.
Watu wa Kijichi, ninawatakia Uchaguzi mwema hapo Januari 22, 2017. Nina imani kwamba mwaka 2017 tutaweza kupata haki yetu ya kikatiba ya kufanya mikutano ya hadhara ili tuendelee kuwaelimisha wananchi ubaya wa Sera za CCM na ubora wa sera zetu za ACT Wazalendo. Tunawaomba wanaKijichi mumchague ndugu Edgar Mkosamali awe Diwani wenu ifikapo jumapili ijayo. Na tunawaomba WanaKijichi pamoja na Watanzania wote waichague ACT Wazalendo, ifikapo mwaka 2019 watupe mitaa mingi na mwaka 2020 watupe Serikali ili tuweze kuwaongoza kwa kuzingatia Utu, Uadilifu na Uzalendo.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo
Kijichi - Dar es salaam 
Januari 15, 2015

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.