Sunday, February 19, 2017

ACT WAZALENDO WAIBUKA NA USHAHIDI JINSI HALI YA CHAKULA ILIVYO MBAYA NCHINI KWA SASA


HALI YA CHAKULA NCHINI BADO NI MBAYA! SERIKALI ICHUKUE HATUA

Jana Jumamosi, Februari 18, 2017, Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Sektetarieti ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA CHAKULA NCHINI kama inavyotolewa hapa chini.

1.       Mtakumbuka Januari 6 mwaka huu, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Nkome mkoani Geita, chama chetu kilieleza kwa undani juu ya tishio kubwa la baa la njaa linaloendelea kuinyemelea nchi yetu. Msingi mkuu wa taarifa yetu ile ulikuwa ni taarifa na takwimu mbalimbali za Serikali yenyewe juu ya hali ya chakula nchini. Baada ya Chama chetu kutoa taarifa husika, tuliiona Serikali kwa kila namna ikihaha kujikita katika kukanusha zaidi taarifa tulizozitoa, badala ya kujikita katika kutatua hali mbaya ya Chakula nchini katika wilaya mbalimbali zaidi ya 50 nchi nzima. Bahati mbaya hali ya chakula nchini haijatengamaa na Chama chetu bado hakijaridhishwa na hatua ambazo Serikali imechukua katika kuzuia tishio hili la baa la njaa nchini.


2.       ACT Wazalendo tumeshtushwa na taarifa mpya za Serikali yenyewe juu ya hali ya Chakula nchini, hasa juu ya uhaba wa vyakula, tishio la baa la njaa na mfumuko mkubwa wa bei za vyakula mbalimbali nchini na hali ya ukuaji wa kiuchumi wa wananchi kwa ujumla.Taarifa mpya za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake juu ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na Monthly Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna mfumuko mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania - Mahindi, ambapo Mfumuko wa bei (Inflation) umekua kwa zaidi ya 30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.

3.       Aidha, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita Sektretariati ya Chama cha ACT Wazalendo imekusanya takwimu kuhusu bei ya vyakula mbalimbali hapa nchini. Takwimu zetu zinaonyesha kuwa bei ya unga, maharage na vyakula vingine muhimu kwa wananchi walio wengi imependa kwa wastani wa kutoka shilingi 900/= kwa kilo katika miezi mitatu iliyopita hadi kufikia shilingi 2000/= katika mikoa mingi katika mwezi wa pili. Katika jedwali hapa chini tunaonyesha wastani wa bei za unga na maharage kwa wiki mbili za mwezi wa Februari kwa mikoa mbalimbali tuliyokusanya takwimu:


Jedwali: Bei ya Unga wa Mahindi na Maharage katika Mikoa Nane nchini+
NA.
MKOA
MAZAO
BEI YA KILA ZAO (Tsh.)
01.
ARUSHA
Unga wa mahindi
1700


Maharage
2200
02.
DAR ES SALAAM
Unga wa Mahindi
2000


Maharage
3000
03.
DODOMA
Unga wa mahindi
1600


Maharage
2200
04.
IRINGA
Unga wa mahindi
1700


Maharage
2200
05.
KILIMANJARO
Unga wa mahindi
1000


Maharage
2200
06.
MWANZA
Unga wa mahindi
1500


Maharage
2000
07.
MOROGORO
Unga wa mahindi
1800


Maharage
1800
08.
TABORA
Unga wa mahindi
1500


Maharage
1700

4. Kutokana na hali ya chakula nchini, na hali ya maisha kwa wananchi kwa ujumla, Chama cha ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali ya CCM kuchukua hatua za haraka kurekebisha mambo, ikiwemo:
(a). Serikali ichochee Tija kwenye Kilimo: Uamuzi wa Serikali ya CCM kupunguza bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka shilingi bilioni 78 mwaka 2015/16 mpaka bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa uamuzi sahihi na umechangia katika kuwapunguzia wananchi uwezo wa kuzalisha. Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinatumia mbolea kwa kiwango kidogo zaidi ulimwenguni.Hivyo, hatua yoyote ya kupunguza bajeti ya mbolea ya ruzuku ina lengo la kupunguza tija ya kilimo chetu na ni hujuma kwa jitihada za kuwakwamua watanzania kutoka kwenye umasikini. Ni kwa sababu hii takwimu za Serikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2016 kasi ya ukuaji wa Kilimo imeshuka kutoka 2.5% mpaka 0.6%. Tunaitaka serikali irekebishe hali hii katika bajeti ijayo ili kuhakikisha kuwa inatenga pesa za kutosha kwa ajili ya kununua mbolea.
(b). Serikali itenge pesa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua ambazo zinazidi kutokutabirika
(c). Serikali ijenge maghala ya kutosha na Bunge liongeze bajeti ya hifadhi ya Chakula ya Taifa
(d). Kutokana na hali ya ukame katika mikoa mingi nchini, na hali ya chakula kuendelea kudorora, tunamshauri Rais atumie mamlaka yake kikatiba kutangaza rasmi janga la ukame nchini na hali mbaya ya chakula.
 5. Hitimisho:
Sisi kama chama cha siasa, kwa kuzingatia falsafa ya chama chetu ya Siasa ni Maendeleo, tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa vyakula nchini, kuhakikisha kuwa vyakula husika vinapatikana katika bei ambayo watanzania wanaimudu, na kuwa hakuna mtanzania anayekufa kwa njaa nchini.


Janeth Rithe
Katibu, Kamati ya Maendeleo ya Jamii - ACT Wazalendo
Dar Es salaam
Jumapili, 19 Februari 2017

No comments: