Monday, February 6, 2017

HABARI KUHUSU KUSHUSHWA DARAJA KEMONDO SUPER FC,RAUNDI YA SITA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017,KOCHA MOROCCO AFUNGIWA MECHI TATU


KUSHUSHWA DARAJA KEMONDO SUPER FC


Timu ya Kimondo Super SC imeshushwa madaraja mawili (hadi Ligi ya Mkoa), na matokeo ya mechi zake zote ilizocheza katika kundi la B yamefutwa kwa kushindwa kufika uwanjani kucheza mechi dhidi ya JKT Mlale bila sababu za msingi.


Mechi hiyo namba 47 (JKT Mlale vs Kimondo Super SC), ilitakiwa kuchezwa Januari 28, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, lakini Kimondo Super SC haikutokea uwanjani wala kutoa taarifa yoyote hadi Februari 1, 2017 ilipotuma taarifa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), na kutoa sababu ambazo hazikukubaliwa na Kamati.

Pia Kimondo Super SC imetozwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo kati ya hizo sh. 1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na TPLB, na sh. 1,000,000 (milioni moja) italipwa JKT Mlale. Adhabu dhidi ya Kimondo Super SC ni utekelezaji wa Kanuni ya 28(1) na (2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

RAUNDI YA SITA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017

Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 24, 2017 kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu ya Pwani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam na Mtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu ya Mbao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Jumatano Machi 1, 2017 Simba SC itacheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam wakati Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

KOCHA MOROCCO AFUNGIWA MECHI TATU

Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), imemfungia Kocha wa Stand United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kushiriki michezo mitatu uwanjani na faini ya Sh 500,000 (laki tano).


Katika mechi Na. 160 ya Ligi Kuu ya Vodacom uliozikutanisha timu za JKT Ruvu na Stand United iliyochezwa Januari 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Morocco aliondolewa kwenye benchi (Ordered off) kwa kosa la kupiga maamuzi ya mwamuzi na kutoa lugha chafu.

Kamati hiyo ya Saa 72 imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 40 (11) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Makocha. Morocco hata kama atakuwa amemaliza mechi tatu nje ya benchi, hataruhusiwa kukaa kwenye benchi hadi awe amelipa faini hiyo.

Adhabu hiyo ya Morocco itaendelea kumhusu hata kama utakuwa umehamia kwenye timu nyingine na katika msimu mwingine wowote.

..…………………………………………………………………………........................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: