Tuesday, February 14, 2017

KINACHOENDELEA JUU YA YUSUPH MANJI ALIKOLAZWA


Hali ya ulinzi imeimarishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikolazwa mfanyabiashara Yusuf Manji baada ya kuugua ghafla akiwa polisi alikokuwa akihojiwa.


Manji aliyekuwa akihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es salaam alipelekwa hospitalini hapo juzi jioni akiwa ndani ya gari la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser lenye nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) huku gari lake aina ya Range Rover likifuata kwa nyuma.

Askari wenye sare na wengine wakiwa na mavazi ya kiraia nje ya wodi aliyolazwa mwenyekiti huyo wa klabu maarufu nchini ya Yanga walionekana wakiimarisha ulinzi.

Ilipofika saa 4:13 asubuhi mfanyabiashara huyo alitoka kwenye chumba hicho na kuongozwa kuelekea upande mwingine wa jengo hilo.

Akiwa amevalia nguo za wagonjwa zenye rangi ya kijani, Manji alitembea taratibu kuelekea upande aliokuwa akielekezwa.

Alipoulizwa kuhusu uwapo wa Manji hospitalini hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema hawezi kuzungumzia taarifa za mgonjwa.

Februari 8, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitoa orodha ya watu 65, akiwamo Manji ambao aliwataka wafike Polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu masuala ya dawa za kulevya.

No comments: