Thursday, February 23, 2017

RAIS MALINZI AELEZA MIKAKATI, NAPE AIPONGEZA TFF




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameelezea mikakati mbalimbali ya maendeleo ya soka nchini akisema hiyo ndiyo sababu ya Kamati ya Utendaji kubuni na kuunda Mfuko wa Maendeleo ya soka.

Katika Risala yake aliyoitoa jana mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye katika uzinduzi wa mfuko huo, Rais Malinzi alisema wamefanya hivyo kwa lengo la kutimiza ndoto za Tanzania kushiriki michuano mbalimbali ya soka.

“Kwa kipindi kirefu Tanzania hatujafanikiwa kucheza fainali kubwa za mpira Barani Afrika. Mara ya mwisho kupata mafanikio makubwa kwa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ilikuwa ni mwaka 1980 Tanzania ilipofuzu kucheza fainali za Afrika (AFCON) nchini Nigeria,” amesema Rais Malinzi na kuongeza:


“Ila kuhakikisha Tanzania inang’ara tena Kimataifa katika mpira wa miguu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linania thabiti ya kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza fainali za kombe la Dunia mwaka 2026 kwa upande wa wanaume (Taifa Stars) na kufuzu kucheza fainali za Dunia kwa mpira wanawake (Twiga Stars) nchini Ufaransa mwaka 2019.


“Msingi mkubwa wa mafanikio ya Timu za Taifa duniani kote ni kuwekeza katika mpira wa vijana ili kuhakikisha vijana wanafundishwa mpira kwa kiwango cha Kimataifa kuanzia wakiwa wadogo. Wakilelewa pamoja na kufundishwa mpira pamoja ukubwani wanaunda Timu ya Taifa imara yenye uwezo wa kushindana na timu yoyote duniani. Hakuna njia ya mkato,” alisisitiza Rais Malinzi ambaye mbali ya Risala hii kupatikana kwenye Mtandao wa TFF wa www.tff.or.tz pia inasomeka hapa chini neno kwa neno.

Kabla ya kuzindua mfuko huo, Waziri Nape alisema:

“Kwanza, napenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kuandaa hafla hii na kunialika mimi kuja kuzindua mfuko huu.

“Pili, niwapongeze TFF kwa kubuni Mfuko huu. Wakati sisi Serikali tunahangaika kuona namna gani tutasaidia, tayari wenzetu wa TFF umekuja na ubunifu na leo nawazindulia mfuko wenu. Hongereni sana. Tunawapongeza.

“Kinachohitajika kwa sasa ni kuunga mkono jitihada hizi za TFF. Ni matumaini yangu kwamba mfuko huu utatimiza wajibu wenu kwa uaminifu na uadilifu.

“Watu wanaweza kusita kama mtapata fedha na mkazitumia visivyo. Kama mtapata fedha mkazitumia inavyokusudiwa basi naamini tutafanikiwa. Na wito wangu kwa viongozi wa mfuko na TFF kuwa wawazi mna kutoa taarifa kila inapobidi.

“Sisi Serikali, kama wadau wakubwa wa mpira wa miguu hatutasita kuonyoosha mkono kama mambo yatakuwa hayaendi sawa, lakini kwa watu walioko kwenye mfuko huu sitatajii kama kunaweza kuibuka malalamiko yoyote.”


Pamoja na hayo, Waziri Nape alitumia fursa hiyo kutoa onyo kwa mashabiki wa mpira wa miguu ambao wana lengo la kufanya fujo kwenye mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaozikutanisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments: