Monday, February 13, 2017

VITA YA MADAWA YAHAMIA SHINYANGA-TIZAMA HII


Kamanda Muliro akionesha dawa za kulevya zilizokamatwa na jeshi hilo -Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limemfukuza kazi askari wake mwenye namba F9899 PC Hassan Mavindi kwa fedheha kutokana kujihusisha na dawa za kulevya kwa makosa ya kukosa uadilifu wakati wa vita dhidi ya dawa za kulevya.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema jeshi hilo linahitaji vita hiyo ifanyike kwa kiwango kikubwa cha uadilifu na umakini mkubwa unaotakiwa kwa askari wakati wa ufuatiliaji wa taarifa.

“Kwa maskitiko makubwa kuanzia Februari 12,2017 jeshi la polisi limeamua kumfukuza kazi askari namba F 9899 PC Hassan kwa fedheha baada ya mfumo wote wa kisheria kuuzingatia,mfumo wa haki”,amesema Muliro.

“Askari huyu alifanyiwa mashtaka ya kijeshi na ushahidi wa kutosha dhidi yake ukatolewa ikabainika hana uadilifu katika zoezi hili ambalo sisi tunaona ni vita kubwa”,ameeleza Muliro.

Amesema jeshi hilo litamfikisha mahakamani askari huyo na kwamba halitavumilia askari yeyote atakayebainika kujihusisha na kutumia dawa za kulevya.

Hata hivyo kamanda Muliro hakuweka wazi kama askari huyo alikamatwa akisafirisha,akiuza au kutumia dawa za kulevya ambapo alisisitiza kuwa wamemfukuza kazi kwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa fedheha kwa makosa ya kukosa uadilifu wakati wa vita dhidi ya dawa za kulevya.

Kamanda Muliro amesema pia watu wengine 33 wamekamatwa kwa kusafirisha,kuuza na kutumia dawa za kulevya. 

Amesema watuhumiwa hao 33 wamekamatwa wakati wa operesheni kali ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya wiki mbili iliyoanza Januari 30,2017 ambayo wiki ya kwanza walijikita katika kuzifuatilia kwa siri za umakini wa hali ya juu taarifa zote za kiintelijensia zinazohusiana na dawa za kulevya.

Amesema baada ya kuzichuja vizuri taarifa hizo kwa lengo la kuepuka ubambikizaji wa kesi walifanya operesheni kwa vitendo kwa upekuzi na ukamataji wa watuhumiwa kuanzia Februari 6,2017.

“Tulikamata gramu 480 za heroine na cocaine,bangi kilo 81,kete za bangi 1,370,misokoto 1,230 ya bangi,mirungi kilo 3 na gramu 1,027 pamoja na vifaa saidizi vya kujidungia dawa za kulevya ikiwemo sindano na bomba za sindano 8 zenye ujazo wa CC 0.5”,ameeleza Muliro.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

No comments: