Tuesday, March 14, 2017

WAZIRI NAPE ATISHIA KUWATUMBUA MAAFISA HABARI WASIO WAJIBIKA IPASAVYO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amemtaka Mkurugenzi wa Habari maelezo kufuatilia utendaji kazi wa maafisa habari na mawasilano wote ili kuona utendaji kazi wao kama unaleta maendeleo kwa jamii.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na maafisa habari na mawasiliano wakati akifungua kikao kazi cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo Mkoani Dodoma.

Amesema kuwa wao ndiyo chanzo cha kuwafanya viongozi wao kukimbia vyombo vya habari kutokana na maafisa hao kushindwa kuwaandaa vyema badala ya kutoa habari zinazotakiwa kwa jamii.

Amesema kuwa maafisa habari na viongozi wa umma nchini wanapaswa kutekeleza sheria hasa zinazowataka kutoa habari na taarifa kwa kuhakikisha vyombo vya habari na wananchi wanapata habari kwa wakati bila urasimu.

“Nataka niiagize ofisi ya mkurugenzi wa habari maelezo kuhakikisha kuwa mnafuatilia utendaji kazi wa kila afisa habari na mawasiliano ili kujiridhisha kama wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria au la na kama tutabaini kuna afisa habari ambaye hatekelezi majukumu yake ipasavyo tumuombe atupishe”. Alisema Nape

Aidha Waziri huyo aliwasisitizia maafisa hao kutoa ushirikiano mzuri kwa waandishi wa habari pindi wanapofika katika ofisi zao kuwapa taarifa sahihi na kwa wakati ili jamii iweze kupata ufumbuzi ya matatizo yao.

No comments: