Mfanyabiashara wa nguo za mitumba ya kike katika Soko la Ilala Boma jijini Dar es Salaam, Daud Omary (kushoto), akitoa maelezo Dar es Salaa jana ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa na baadhi ya askari polisi wa Kituo cha Pangani kwa Mwezeshaji wa kisheria katika soko hilo (kulia) kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG), wakati wa uhamsishaji wa kufungua klabu za mabadiliko ya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni unaofanywa na Shirika hilo kwa kusimamiwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) kupitia kampeni ya miezi miwili ya Tunaweza. Katikati ni mfanyabiashara Seleman Adam.
Fundi ushonaji nguo katika Soko la Ilala Boma, Abdallah Omari (kulia), akitoa maelezo kwa mwezeshaji sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga na klabu ya mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Fundi ushonaji nguo katika Soko la Ilala Boma, Hamisi Bweni (kulia), akitoa maelezo kwa mwezeshaji sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga na klabu ya mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Mama Lishe, Zaina Amri (kushoto), akijieleza kwa mwezeshaji wa sheria, Irene Daniel, wakati akijiunga na klabu hiyo.
Wafanyabiashara katika soko hilo wakijiunga na klabu hiyo. Kutoka kulia ni Fatuma Bayuni, Ibrahim Said na kushoto ni mwezeshaji wa kisheria Irene Daniel kutoka EfG.
Mama Lishe Sauda Mwinyi akisoma kipeperushi kabla ya
kujiunga na klabu ya mabadiliko.
Mama Lishe Wanamabadiliko wakiweka bango la kupinga ukatili huo. Kulia ni Fatuma Bayuni na Zaina Amri.
Mwezeshaji wa Kisheria masokoni, Irene Daniel (kulia), pamoja na wanamabadiliko wa Soko la Ilala Boma, wakionesha vipeperushi vya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni. Kutoka kushoto ni Zaina Amri, Ibrahim Saidi na Fatuma Bayuni.
Na Dotto Mwaibale
WAFANYABIASHARA katika Soko la Ilala Boma jijini Dar es Salaam wamelipongeza Shirika la Equality for Growth (EfG) kwa kuwahamasisha kufungua klabu za kupinga ukatili wa kijinsia masokoni.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, walisema kufunguliwa kwa klabu hizo kutawasaidia kwa karibu kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika katika soko hilo na mengine.
"Binafsi nalipongeza shirika hili kwa hatua hii nzuri waliofikia ya kutuhamasisha kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutusogezea huduma hii karibu ambayo itapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo vya ukatili masokoni" alisema Abdallah Omari ambaye ni mshonaji nguo katika soko hilo.
Omari alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo ni wapi walipaswa kutoa taarifa za ukatili huo wa kijinsia kwani wengi wao walikuwa hawajui lakini kwa kuanzishwa klabu hizo na kuwa na namba za wawezeshaji wa kisheria kwao milango ya utoaji wa taarifa hizo sasa imefunguliwa.
Mfanyabiashara wa kuuza nguo za mitumba za kike katika soko hilo, Daud Omari alisema kuna baadhi ya polisi kutoka kituo cha Pangani wamekuwa wakiwafanyia ukatili wa kijinsia pale wanapoenda kuwakamata na kuanza kuwapiga na kibaya zaidi wanakuwa hawajitambulishi mpaka wanapofika kituoni.
"Unajua hapa sokoni kunakuwa na mambo mengi hasa pale tunapopishana na wenzetu na kwenda kushitaki polisi wakifika wao uanza kupiga watu bila ya kujitambulisha na ukifika polisi ndipo wanajitambulisha kuwa wao ni polisi kitendo hicho kwetu tunahesabu kuwa ni ukatili wa kijinsia tunaofanyiwa na askari hao" alisema Omari.
Omari Lubuva mfanya biashara katika eneo hilo alisema mtu anapotoa oda ya chakula kwa mama lishe akipelekewa anapo muambia mama lishe husika kuwa ondoka na chakula chako umekichelewesha nimemuagiza mwingine aniletee huo ni ukatili wa kijinsia dhidi ya mama lishe.
Aliwaomba wafanyabiashara wenzake wenye tabia hiyo kuacha kufanya hivyo kwani jambo hilo ni ukatili mbaya kwa mama lishe hao.
Seleman Adam aliwapongeza EfG kwa hatua walioifikia ya kuwasogezea huduma hiyo kwa mara nyingine hivyo akayaomba mashirika mengine kujitokeza kusaidia wananchi katika maeneo mengine kwani katika jamii kuna changamoto nyingi.
Mwanasheria wa Shirika hilo, Muna Abdallah alisema muitikio wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko waliyoyatembelea ni mkubwa mno.
"Kwa kweli watu wengi wameonesha kuchoshwa na vitendo hivyo na wamepokea kwa mikono miwili mradi huu tuliouanzisha wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili wa kijinsia masokono" alisema Abdallah.
Mratibu wa mradi huo ambaye pia ni Mwanasheria wa Shirika hilo, Mussa Mlawa alisema msimamizi mkuu wa mradi huo kupitia kampeni ya Tunaweza ni Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) lakini EfG wao wanaiendesha kampeni hiyo ya miezi miwili katika masoko matano yaliyopo jijini Dar es Salaam ambayo ni Ilala Boma, Ferry, Mchikichini, Temeke Sterio na Buguruni.
Alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuwa na wanamabadiliko masokoni ambao watasaidia kupambana na vitendo hivyo si katika maeneo ya masoko pekee bali hata majumbani kwa jamii.
No comments:
Post a Comment