Kituo cha sheria na Haki za Binadamu kimeendelea
kufuatilia kwa ukaribu masuala ya haki za binadamu hususani haki za kisiasa na
kiraia ambazo ni miongoni mwa haki muhimu kwa binadamu. Katika kuifuatilia haki
hii na kuitetea, Kituo kimeendelea kuona umuhimu wa kuwepo kwa Katiba ya
wananchi, kwani masuala mengi ambayo yamelalamikiwa na wananchi na viongozi na
hata juhudi za Rais John Pombe Magufuli za Kupambana na ufisadi kuirudisha
heshima ya watendaji serikaliniyangeweza kupata suluhisho kwa kufufua mchakato
wa Katiba Mpya ulioahirishwa bila tarehe maalum za kuurejesha .
Ikumbukwe
kuwa toka mchakato wa kuandikwa kwa
Katiba Mpya ulipoanza mwaka 2011, ni zaidi ya shilingi Bilioni moja za
Kitanzania zimekwisha kutumika. Matumizi haya makubwa ya kodi ya watanzania
bila kupata matokeo ambayo ni kupatikana kwa Katiba Mpya ya wananchi ni sawa na
ubadhirifu wa fedha hizo.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinasikitishwa sana na ukimya wa Serikali juu ya
kuuendeleza mchakato huu. Awali, alipokuwa akisoma bajeti ya Wizara ya Katiba
na Sheria aliyekuwa waziri wa Sheria na Katiba Mheshimiwa Harrison Mwakyembe alieleza
nia ya Serikali kuukamilisha mchakato huu. Hata hivyo, tulishangazwa kutokujumuishwa
kwa suala hili katika bajeti ya mwaka 2016/2017.Pia Mheshimiwa Rais alipokuwa
akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza alieleza pia nia ya Serikali ya kurejea
kwenye mchakato na kutanabaisha kwamba nafasi iko wazi kwa maoni yotote
kuboresha Katiba Pendekezwa kabla haijapigiwa kura ya maoni.
Kutokana
na hali hiyo Kituo kilihamasika kuufuatilia kwa ukaribu zaidi mchakato huu ili
kuhakikisha upatikanaji wa katiba ambayo imehusisha asilimia kubwa ya maoni ya
watanzania.
Kuwepo
kwa kauli mbalimbali za viongozi ambazo zinakatisha tamaa, bado hakujarudisha
nyuma jitihada za wananchi kudai mchakato huu kurejeshwa.
Kukosekana
kwa taarifa rasmi kumeendelea kusababisha wananchi kukata tamaa ya kupata
katiba mpya ambayo ingeweza kutatua changamoto zao kwa kiwango kikubwa. Kama
serikali ilivyo na mipango mingi, ni muda muafaka serikali ikaleta mpango
mkakati wa kumalizia mchakato wa katiba ili wanahabari wajiandae vema kushiriki
kwenye hatua zitakazofuata wakiwa na taarifa za kutosha.
Pamoja
na hatua iliyokwisha kufikiwa, Kituo kinaamini kwamba bado kuna fursa kubwa na
wajibu mkubwa wa kufanikisha kufufua Muafaka wa Kitaifa juu ya Mchakato wa
Katiba ambao ulitetereka katika ngazi ya Bunge Maalum la Katiba na hatimaye
kuweka mazingira mabaya kwa umoja wa Taifa letu na kufifisha uhakika wa kukidhi
lengo la awali la upatikanaji wa Katiba ya wananchi yenye misingi mizuri kwa
Taifa la Tanzania.
Mapendekezo;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadmu kinapenda
kuainisha mapendekezo yake kama ifuatavyo;
1.
Serikali
iboreshe Sheria zinazoongoza Mchakato wa Katiba yaani Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba Na. 83/2011 na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013 ili ziruhusu mwelekeo
mpya wa mchakato wa Katiba wenye tija na kujenga mazingira
yenye kuzingatia muafaka wa Kitaifa katika upatikanaji wa Katiba Mpya.
Maboresho haya ya Sheria ni vema yakazingatia kuondoa vifungu vibovu vya Sheria
hizo ambavyo vimekua kivuli cha kuvurugika kwa muafaka katika hatua zilizopita
za utungaji wa katiba mpya ikiwemo kupunguza uwezekano wa wanasiasa na vyama
vya siasa kuuteka mchakato wa Katiba.
2.
Wananchi
wote tudai kurudishwa mjadala wa kitaifa juu ya haja ya kufufua mchakato wa
mabadiliko ya katiba, kwa mrengo wa maoni ya wananchi na usitishwaji
wa hatua inayofuata ya Kura ya Maoni kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni Na.
11/2013 ili kutoa fursa kwa wadau kujenga muafaka mpya wa kitaifa na kuamua
namna bora ya kuelekeza Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
3.
Serikali
itenge bajeti kwa mwaka 2017/2018 kuwezesha mchakato huu wa
Katiba Mpya kuendelea.
4.
Serikali
itekeleze maagizo ya Hukumu inayohusiana na Kura ya Maoni iliyo
tolewa tarehe 3 Februari 2017 Kuweza kuifanyia mabadiliko sheria ya Kura ya
Maoni No. 11 ya mwaka 2013 itakayo toa
muongozo wa kuendelea na mchakato wa katiba.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu tunandelea kuwa sehemu ya uhamasishaji wa Katiba
ya wananchi pasipo kukata tamaa kwa kuzingatia Mabadiliko yanayojitokeza na muelekeo
wa taifa kwa ujumla.
Imetolewa na,
Dr.
Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi
Mtendaji
No comments:
Post a Comment