Thursday, April 20, 2017

LOWASA AIBUKA BUNGENI KIVINGINE,NASARI AMSHUKIA MWAKYEMBE


Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe jana walichafua hali ya hewa bungeni na kusababisha mzozo mkubwa katika mjadala uliokuwa ukiendelea.

Wawili hao walihamisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais Tamisemi na kurudisha suala la Richmond lililotokea mwaka 2008, huku Nasari akimtuhumu Dk Mwakyembe kuwa hakutenda haki katika ripoti yake na kumuondoa bila kumpa nafasi ya kujitetea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

“Huyu Mwakyembe ndiye aliyeongoza ripoti ya Richmond na hakumpa nafasi mheshimiwa Lowasa ajitetee, leo tena kapewa dhamana ya kuongoza Wizara ya Habari, Nape (Nnauye) ameondolewa lakini hakuna nafasi ya kumhoji Mkuu wa Mkoa... hakuna haki hapo,” alisema.

Kauli za Nasari zilimfanya Dk Mwakyembe kuomba mwongozo na aliposimama alisema: “Nilikuwa naongoza kamati na utaratibu mzuri wa kisheria ni kuwa, kama utaona kuna ushahidi wa kutosha hakuna sababu ya kumuita mtu, unaleta taarifa bungeni halafu Bunge linakuja kuamua.”

Dk Mwakyembe alisema katika taarifa yao, waliona hakuna sababu ya kumuita Lowassa kuhojiwa kwani ushahidi ulikuwa wazi na ndiyo maana hakutakiwa kuitwa mbele ya kamati badala yake walikuja kumshtaki bungeni.

“Huyu mtu wanayekuwa na mahaba naye kwa sasa, nasema wamlete hata leo waone kama hatutamnyoa kwa chupa, kanuni za kibunge zinaruhusu anaweza kuirudisha tena taarifa ya Richmond na ikaanza upya,” alisema Dk Mwakyembe.

No comments: