Sunday, April 2, 2017

NI SERENGETI BOYS NA BLACK STARLETS KESHO UWANJA WA TAIFA


Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, kesho Jumatatu itapambana na Black Starlets ya Ghana kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni, Serengeti Boys itautumia kama ni ishara ya kuwaaga mamilioni ya Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.

Lakini kabla ya kutua Gabon, Serengeti Boys itakwenda Rabat, Morocco kufanya kambi ya takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji morocco na timu nyingine ya jirani ama Tunisia au Misri. Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu itasafiri hadi Cameroon.

Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.

Vipimo vya mechi dhidi ya Ghana kadhalika hapo baadaye Cameroon, vitakuwa mwafaka kwenye kufanya tathmini ya uwezo wa Serengeti Boys kwani wapinzani hao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye soka la vijana na kwa kipindi hiki zimepangwa kundi A pamoja na wenyeweji Gabon na Guinea.

Kila la kheri Serengeti Boys katika mapambano ya kuwania ubingwa wa Afrika kadhalika kucheza fainali za Kombe la Dunia hapo Novemba, mwaka huu zitakazofanyika India. Serengeti Boys inaweza na Mtanzania tunakuomba kuichangia timu hii kwa namna ya 223344 kupitia mitandao yote ya simu.

……………………………………………………………………………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: