Monday, May 15, 2017

EXIM BANK TANZANIA YATOA FURSA YA ZIARA KWA WANAFUNZI WA HARVARD

Wanafunzi kutoka chuo kikuu maarufu cha biashara cha Marekani - Harvard Business School wafanya mahojiano na wadau wa Dar es salaam ili kupata taarifa zaidi juu ya mtazamo wao wa sekta ya kibenki nchini Tanzania. Benki ya Exim Tanzania hivi karibuni ilipata fursa ya kuwa mwenyeji wa wanafunzi hawa, kwa wiki moja, kuwapatia uzoefu na ujuzi wa kufanya kazi katika mazingira mageni.

Benki ya Exim Tanzania hivi karibuni ilipata fursa ya kuwa mwenyeji wa wanafunzi waliokuwa wanafanya ziara ya kimasomo kutoka chuo kikuu maarufu cha biashara cha Marekani - Harvard Business School. Wanafunzi hao walikuja katika benki hiyo jijini Dar es Salaam kwa wiki moja kama sehemu ya mafunzo yao ya mwaka wa kwanza kupitia mpango unaoitwa ‘FIELD Global Immersion’ ambayo Exim ni mmoja wa wanachama.

“Tunajivunia kufanya kazi pamoja na chuo cha Biashara cha Harvard kwa kuwapatia wanafunzi uzoefu wa kihalisia wa kufanya kazi katika nchi kama Tanzania” alisema Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu Fredrick Kanga. “Tuna uhakika kupitia ziara hii wanafunzi hawa waliweza kupata ujuzi ambao wasingeweza kupata katika majadiliano ya darasani pekee.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Tanzania, Bwana Dinesh Arora [wa kwanza kulia] na Mkuu wa huduma za rejareja za kibenki, Mr Rahul Singh [mwisho kushoto] wakiwa pamoja  na wanafunzi wa chuo cha Harvard Business School, katika makao Makuu ya  Exim Dar es Salaam. Kama mmoja wa washirika wa kimataifa wa chuo hicho, Benki ya Exim ilikuwa mwenyeji wa wanafunzi hawa kwa wiki moja na kuwapatia elimu na ujuzi juu ya sekta ya kibenki nchini Tanzania.

Mpango huo wa FIELD Global Immersion ni programu iliyoundwa kuwaimarisha wanafunzi na kuwajengea uwezo wao wa kumudu na kuweza kufanya kazi kiufanisi katika tamaduni mbalimbali ulimwenguni. Benki ya Exim ilianza kufanya kazi na wanafunzi hao kwa miezi kadhaa kabla ya kuwasili nchini. Wakiwa nchini wanafunzi hao walitoa mawazo yao kwa uongozi, walishiriki katika utafiti na wateja jijini Dar es Salaam na mwishowe kutoa mapendekezo yao kwa uongozi wa benki. Kusudio la zoezi hili ni kutoa fursa kwa wanafunzi kupata uzoefu wa kufanya kazi katika mradi wa uvumbuzi katika mazingira mageni.

Harvard inakiri pia kuwa ziara hii ya kimasomo isingewezekana bila kuwepo na washirika wa kimataifa.

“Tunaishukuru sana Exim Bank Tanzania na washirika wengine wote wa FIELD Global Partner kwa yale wanayofanya kwa niaba ya wanafunzi wetu,” alisema Profesa Juan Alcacer, mkuu wa kitengo cha FIELD. “Wanafunzi wetu wanafaidika kupita kiasi kupitia ziara hizi na tunategemea kuwa washirika wetu wanafaidika pia.”

No comments: