Sunday, May 7, 2017

HOTUBA YA ZITTO KABWE NA HALI YA KISIASA NCHINI 07/05/2017

HALI YA KISIASA NCHI NA NAFASI YA ACT WAZALENDO KWENYE SIASA ZA TANZANIA - 2
(Maelezo ya Kiongozi wa Chama katika kikao cha Kamati kuu ya Chama kilichoketi Mjini Kahama wakati wa Miaka Mitatu ya Chama -  7/5/2017)

1.      Utangulizi
Juzi Mei 5, 2017 Chama chetu cha ACT Wazalendo kilitimiza miaka 3 tangu kuzaliwa kwake mwaka 2014. Kwa umri wa vyama vya siasa mbaimbali nchini, miaka mitatu unaweza usiwe umri wenye maana yoyote, lakini kwa umri wa chama cha siasa cha Kijamaa na kinachopata ufuasi na kupitia vikwazo vingi  kama  chama chetu, basi miaka mitatu ina maana kubwa sana. Ni miaka inayoonyesha safari ndefu ya mapambano ya kurudisha misingi iliyoasisi Taifa, kusimika Demokrasia ya kweli na kuleta sera mbadala za Kijamaa zinazosimamia masuala ya wanyonge wa Taifa hili na Watanzania wote kwa ujumla.

Napenda kuwapongeza Viongozi wote wa Kitaifa, pamoja na wale wa Mikoa na Wilaya mbalimbali nchini walioshiriki kwa njia mbalimbali katika maazimisho ya miaka hii mitatu ya Chama chetu. Ukiondoa chama tawala, CCM, sisi ndio chama pekee nchini ambcho kila mwaka kinafanya maazimisho ya kuongezeka kwa umri na uhai wa chama, ndio maana tuko hapa Kahama, kuazimisha miaka mitatu ya uhai wa chama chetu.

Lakini pia, Mei 5 hiyo hiyo, ulitimia mwaka mmoja na nusu sasa tangu Rais wa Awamu ya Tano ale kiapo cha kusimikwa kwa Serikali yake, Novemba 5, 2015. Hivyo basi, wakati chama chetu kikitimiza miaka hii mitatu tangu kuzaliwa kwake, Serikali ya awamu ya tano nayo imetimiza mwaka mmoja na nusu  tangu kusimikwa kwake. Nimeonelea basi, leo, katika kikao hiki cha Kamati Kuu, nitoe waraka wangu huu wangu wa pili kwa Kamati Kuu ya chama chetu juu ya ‘Hali ya Kisiasa Nchini na Nafasi ya Chama chetu cha ACT Wazalendo katika Siasa za Tanzania’, katika waraka huu nitajikita katika kuangazia hali ya kisiasa ya nchini, nikizieleza changamoto zetu, fursa zilizoko, hali ya kiuchumi ya nchi, changamoto za uongozi na kushauri juu ya namna njema ya kuenenda ili kuondoa vikwazo vilivyoko na kufaidika na fursa mbalimbali kuelekea 2020.

Na mwisho kabisa, nimefanya tathmini ndogo, ili iwe mwongozo wa msingi wa maamuzi mbalimbali ya chama wakati wa kutatua changamoto na kutumia fursa.
2.     MKONO WA CHUMA: Hali ya Kisiasa Nchini na Changamoto Kuu ya Demokrasia Yetu
Waraka wangu wa kwanza kwa Kamati kuu juu ya hali ya kisiasa ya nchi yetu na nafasi ya ACT Wazalendo katika siasa za Tanzania nilioutoa Septemba 5, 2016 jijini Dar es salaam  ulijikita katika kuelezea kwa upana juu ya changamoto kadhaa ambazo zimezikumba siasa zetu tangu Utawala wa Serikali ya awamu ya Tano uingie madarakani. 

Nilieleza kuwa utawala huu chini ya Rais Magufuli, kwa sehemu kubwa, umebadilisha utamaduni wa uendeshaji wa siasa nchini na kuleta matokeo ya namna mbalimbali kwa vyama vya siasa ikiwemo ACT Wazalendo. Niliieleza changamoto za kuzuiwa kwa shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, na hata uhuru wa vyombo vya habari unavyobinywa nchini, sehemu kubwa ya changamoto husika bado hazijaisha.
Rais Magufuli amejipambanua kuwa Rais mwenye kupenda kutumia mkono wa chuma katika kutimiza adhma yake ya kuhakikisha vyama vya upinzani na Asasi za Kiraia zinazoikosoa serikali hazifurukuti. Mikutano ya hadhara imekwishapigwa marufuku na jeshi la polisi na watendaji wa serikali wanaohaha kumridhisha Rais. Wanasiasa wanaoikosoa serikali wametishwa na kusakwa na jeshi la polisi na baadhi yao kuwekwa korokoroni ili kuwaziba midomo. Lengo la rais Magufuli na serikali yake ni dhahiri: kutumia vitisho na vyombo vya dola ili kuvidhoofisha na ikiwezekana, kuvifuta kabisa kwenye ramani vyama “vya kweli” vya upinzani nchini.
Mbali na wanasiasa, Serikali ya Rais Magufuli imechukua pia hatua kadhaa kuviziba mdomo vyombo vya habari vinavyoikosoa serikali. Wamiliki wa vyombo vya habari, Magazeti, vituo vya Televisheni na Radio vinafungiwa, kuonywa na kutishiwa kwa kisingizio cha kutoa habari za uchochezi, watu kadhaa wamefunguliwa mashtaka mahakamani kwa kuonekana maoni yao ni kashfa kwa Rais huko kwenye mitandao ya Kijamii. Sheria ya Mitandao inatumiwa sana kuwabana wakosoaji wa Serikali.
Kwa miezi hii 6 tangu nitoe ule waraka wa kwanza hali husika haijabadilika kabisa, na kwa kiasi kikubwa imezidi zaidi. Kasi ya kudogosha nguvu ya Bunge pamoja na taasisi nyengine za uwajibikaji imekuwa kubwa zaidi, tishio kwa wamiliki wa vya vyombo vya habari, wanahabari pamoja na vyombo vya habari vyenyewe nalo limekuwa wazi, wakati zuio kwa siasa za vyama vya siasa (kwa maana ya Mikutano ya hadhara na Maandamano) liko palepale. Hivyo niseme hali imekuwa mbaya zaidi.
2.1.           Matokeo Yake Kwa Vyama Vya Upinzani Nchini
Tangu kuhuishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini kwenye miaka ya tisini, vyama vya upinzani vimejikita kwenye njia za jadi za uenezi, ambazo ni mikutano ya hadhara, maandamano na makongamano. Hivyo basi, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kumeathiri sana uwezo wa vyama vya siasa kunadi sera na kuvuna wanachama.
Wakati haya yakivikumba vyama vya upinzani, Chama tawala kinaendelea kuwatumia viongozi na watendaji  wa serikali (Rais, mawaziri, wakuu wa wilaya, wabunge, madiwani na wakurugenzi, nk) kukitangaza chama hicho katika inayoitwa “Mikutano ya kuhimiza maendeleo”. Fursa hiyo kwa vyama vya upinzani inapatikana katika maeneo tu ambayo vyama hivyo vina wabunge na madiwani, au halmashauri ambazo wanaziongoza.
2.2.          Athari Na Faida Kwa ACT Wazalendo
Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekiathiri chama chetu pia, muundo wa chama chetu nao ulijiegemeza katika njia za asili za uenezaji chama (mikutano ya hadhara, maandamano nk), hata ziara ya kutambulisha chama ya mwaka 2015, ambayo ndiyo ziara kubwa zaidi tuliyowahi kufanya, nayo ilikuwa katika muundo wa mikutano mikubwa ya hadhara. Hivyo kwa kuzuiwa mikutano ya hadhara (nje ya jimbo moja tunaliliongoza, na Kata kadhaa nchini), kumekuwa na athari kubwa kwa chama chetu.
Lakini ni ukweli pia kuwa uwezo wetu wa kiuchumi umeshuka mno mara baada ya uchaguzi mkuu, msingi wa chama chetu katika kuwa na vyanzo vya kiuchumi haukuwa mzuri, tangu awali hatukujenga utamaduni wa kuhamasisha wanachama na wafuasi wetu wakichangie chama kama chanzo kikuu cha mapato ya chama, tulijikita katika kutegemea michango mikubwa ya viongozi wa kuu wa chama, ambao mara baada ya uchaguzi nao waliathirika kwa kuwa na madeni makubwa ambayo yamepunguza uwezo wao wa kukichangia chama. Jambo hilo limepunguza kwa kiasi flani hata uwezo wetu wa kuzunguka mikoa mbalimbali nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara, hivyo zuio hili kwa kiasi kikubwa limesaidia kutupa sababu dhidi ya ukata wetu.
Lakini hiyo haipaswi kuwa sababu ya kuacha haki hii ya vyama vya siasa kuzuiwa, maana ni kinyume na Katiba na inaviza ukuaji wa Demokrasia yetu pamoja na uenezaji wa Sera za chama chetu katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.

3.     Hali Ya Uchumi: Wananchi Wana Hali Ngumu Sana
Eneo jengine muhimu la waraka huu ni juu ya hali ya uchumi ya nchi, eneo hili serikali ya awamu ya tano imefanya vibaya sana. Kiashiria kikuu ni utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 ambao mpaka mwezi machi mwishoni bajeti katika wizara nyingi utekelezaji wake haukuzidi hata 50%. Hata Bajeti ya mwaka huu wa fedha uwasilishwaji wake umeonyesha kuwa matumaini ya uchumi kuwa mzuri hayapo tena, kuna hali kubwa ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi. 
Maeneo mengi ya nchi kuna uhaba mkubwa wa chakula na badala ya Serikali na hasa Rais kuwa matumaini Kwa wananchi akiwa Comforter In Chief, kumekuwa na maneno makali ya kuwakatisha tamaa wananchi. Bei za vyakula nchini zimepanda mno kiasi cha wananchi kushindwa kumudu chakula ili waweze kufanya kazi na kukuza Uchumi. Vyakula vikuu kama mahindi, sukari, mafuta ya kupikia, ngano nk bei imekuwa juu mno.
Taarifa za Serikali kupitia ripoti za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake juu ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na Monthly Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna mfumuko mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania - Mahindi, ambapo bei ya chakula hicho kikuu nchini imepanda kwa zaidi ya 30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.
Leo bei ya kilo moja ya mahindi nchini iko sawa au ni zaidi ya bei ya kilo moja ya mchele kwenye miji mbalimbali nchini, sukari bei juu, mafuta ya kula bei juu nk. Kwa wakati wa mjini hata bei ya gesi kwaajili ya kupikia majumbani imepanda, wananchi wamerudia matumizi ya mkaa, tujiandae na uharibifu wa misitu nchini. Ofisi ya takwimu ya Taifa imetoa Taarifa ya kuonyesha kuwa Mfumuko wa Bei umepanda kwa kasi na sasa umefika asilimia 6.4 Kwa mwaka unaoishia Machi, 2017.
Ukuaji wa sekta binafsi umedorora na kushuhudia biashara maelfu kwa maelfu zikifungwa na kusababisha ajira nyingi kupotea na ajira chache kutengenezwa. Manispaa ya Ilala peke yake imefunga biashara 2900 na hivyo kupoteza chanzo cha mapato ya Manispaa. Lakini hata mikopo ya Kibenki kwa sekta binafsi imepungua mno, ikiwa ni kiashiria cha mdororo wa sekta binafsi. Jana kulikuwa na mkutano wa baraza la biashara la Taifa, uliofanyika ikulu jijini Dar es salaam, wawakilishi wa wafanyabiashara na wale wa sekta binafsi walilieleza hili kwa upana.
Kwenye uwekezaji nako hali si nzuri, uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya nchi umepungua sana. Matamko ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu mwelekeo wa Uchumi yanatuma ujumbe hasi kuhusu uwekezaji wa mitaji nchini, na hivi sasa kila mwekezaji kwenye macho ya Serikali anaonekana mpiga dili (katika mkutano wa jana Ikulu, ndugu Mengi – kwa niaba ya sekta binafsi, alilieleza hili). Juhudi zote za kuhamasisha uwekaji wa mitaji nchini zilizofanywa tangu Serikali ya awamu ya tatu, zimefutwa katika mwaka Mmoja na nusu tu wa Serikali ya awamu ya tano. Hali ni ya kusikitisha sana.
Tatizo jengine kubwa ni suala la ajira, ukiondoa ajira zilizopotea kwa mdororo wa sekta binafsi, lakini pia hakuna ajira mpya serikalini tangu awamu ya tano iingie madarakani. Vijana mbalimbali waliomaliza masomo yao ya Ualimu, Utabibu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvivu bado wako mtaani bila ajira kwa mwaka sasa. Hata walioajiriwa mwanzoni ajira zilisitishwa kwa kisingizio cha uhakiki wa watumishi wa Umma. Kukoleza maumivu kwenye kidonda ni hatua ya kufukuza wafanyakazi 10,000 waliodaiwa kughusi vyeti.
Serikali imeajiri walimu 3000 tu wa ualimu wa masomo ya sayansi na madaktari wasiozidi 300, japo kwenye mei mosi imejitapa kuwa itaajiri watumishi 52,000 mwaka huu (jambo ambalo haitafanya), kuongeza mishahara na kupandisha watumishi vyeo. Hatua zote hizo hazitoshi katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kwenye Kilimo (ambayo ndiyo sekta inayohusisha wananchi wengi zaidi nchini) hali ni mbaya zaidi. Taarifa ya ya robo mwaka ya Benki Kuu nchini, BOT quarterly economic bulletin ya Disemba 2016 inaonyesha kuwa sekta ya Kilimo ilikua kwa kasi ya 0.6% tu kutoka ukuaji wa 2.5%. Asilimia 75 ya Watanzania wote wamejiajiri katika sekta ya Kilimo, hivyo mdororo huu ya sekta ya Kilimo kutoka ukuaji wa 2.5% mpaka ukuaji wa 0.6% ni ishara mbaya mno kwa ustawi wa zaidi ya robo tatu ya Watanzania.
Kwa Vijijini 78% ya Watanzania wanajihusisha na Kilimo. Hii maana yake ni kwamba wananchi wengi vijijini hawafanyi uzalishaji, jambo hili ni hatari sana, ni dalili kuwa ufukara wa watu wetu unazidi. Ni kwa sababu hii, pamoja na uchumi wetu kukua kitakwimu, 7% kwa mwaka, lakini bado wananchi wetu walio wengi wanaishi kwenye dimbwi la ufukara. Maana ukuaji huo wa Uchumi hauhusishi kilimo, hauhusishi zaidi ya robo 3 ya Watanzania.
Ukuaji huu mdogo wa Kilimo unapaswa kutushtua, kwani ni hatari sana, ni hatari mno. Maana unajenga uchumi unaowaacha karibu zaidi ya robo 3 ya Watanzania kwenye ufukara, ni uchumi unaopanua matabaka ya mafukara na matajiri.Ukuzaji wa viwanda, ambayo ndiyo sera kuu ya msingi ya Serikali ya awamu ya tano nao umeshuka mno, taarifa za serikali zinaonyesha juu ya kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani, ikiwa ni athari pia ya kushuka kwa uwezo wa manunuzi wa watanzania (purchasing power). Jambo hilo limefifisha matumaini ya Tanzania ya wiwanda.
Athari kubwa zaidi iko kwa wakulima, maana ndoto yao ya kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo kupitia viwanda vidogo vya usindikaji na uzalishaji bidhaa haionekani kutimia, hata korosho ambalo ndio zao lililotuingizia fedha za kigeni zaidi tumeziuza zikiwa hafi, hatukufanya ubanguaji nchini na hivyo kuongeza thamani. Hali iko hivyo pia kwenye pamba yetu na mazao mengine ya kibiashara kama Karafuu na mkonge. Mazao hayo, kungekuwa na sera nzuri yangewezesha mamilioni ya ajira nchini kwenye sekta ya nguo, ubanguaji korosho na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge. Si huko tu, uvunaji nao wa samaki katika bahari na maziwa yetu haujaonekana kuzalisha ajira za kutosha zenye tija.
Sekta za huduma nazo hazikufanya vizuri, bado kuna changamoto kubwa sana kwenye sekta ya elimu pamoja na juhudi kiasi za serikali,changamoto ambazo zinazorotesha ndoto ya ubora wa elimu inayotolewa. Kwenye elimu ya juu hali ndio ni mbaya zaidi, vijana wengi wa kitanzania wamekosa fursa na haki yao ya elimu kwa kukosa mikopo.Sekta ya afya nayo halikadhalika, bajeti ya dawa kwa mwaka 2016/17 iliyopangwa haikufikiwa hata nusu, hivyo kuchangia hali ya ukosefu wa Dawa katika vituo vya afya mbalimbali nchini, urari wa madaktari wanaohudumia wagonjwa bado umebaki vile vile kuwa ni mara mbili ya Kiwango kinachotakikana duniani, hata Bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya afya haionekani kutatua changamoto hizi.
Yote hayo yana athari kwenye uchumi wa nchi, yamepunguza kipato cha wananchi, yamechangia ugumu wa maisha. Yamefuta matumaini waliyokuwa nayo watanzania na yamewakatisha tamaa.
Chama chetu kikikazania kuyasemea masuala haya (ambayo ni masuala ya wananchi) kitajipambanua kwa upekee. Kwenye Mpango Mkakati wa miaka 5 wa Chama chetu tumesema dhahiri kuwa tunataka Siasa za Maendeleo. Hivyo kibwagizo cha Demokrasia Ni Maendeleo au Demokrasia na Maendeleo Ni muhimu sana katika Siasa za Zama hizi za sasa.

4.     Kigoma Ujiji: Nafasi Ya ACT Wazalendo Kuonyesha Utofauti Wa Kiuongozi
Hali hiyo ya kiujumla ya uchumi wa Taifa inatupa nafasi kubwa sana ya kuonyesha mapungufu ya Serikali hii ya sasa ya CCM, inatupa nafasi nzuri ya kuonyesha ubaya wa sera zao na ubaya wa usimamizi wao wa sera husika, ni jambo linatupa fursa ya kujinadi kwa kuonyesha mapungufu ya Serikalia pamoja na kuainisha njia mbadala za utatuzi wa hali hiyo kwa Watanzania.
Lakini kufanya hayo tu hakutuhakikishii ushindi kwenye Uchaguzi 2020 (ushahidi tuliuona kwenye chaguzi ndogo mbalimbali za udiwani nchini), suala la kuchaguliwa halina mahusiano sana na uzuri wa kukosoa tu na kutoa njia mbadala, ni muhimu sana nasi tuonyeshe mfano kwa kuongoza vizuri katika maeneo ambayo tumepewa dhamana ya uongozi. Pamoja na kuisimamia Serikali kwenye uendeshaji wa nchi kiujumla, Chama chetu kina ridhaa ya kuendesha Halmashauri ya Kigoma Ujiji. Kwa kiasi flani kipimo tunachokitumia kupima Serikali kuu ya masuala mbalimbali ya uongozi ndicho hicho kitatumika kutupima nasi katika uendeshaji wetu wa mambo ya kiuongozi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ambayo sisi tumepewa dhamana ya kuyaongoza – hasa hasa Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa sana katika kuendesha Serikali kwa uwazi, utaratibu wetu wa kuainisha mapato yote ya halmashauri kwa kila mwezi ni hatua njema sana ya kuanzia. Hati chafu ya Halmashauri ya Kigoma Ujiji, kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 ni jambo linalotutia doa (hasa kwa kuwa pia katika kipindi hiko chama pia kimepata hati chafu), ni jambo ambalo linatuondolea uhalali kama chama wa kuionyoshea kidole serikali kuu ya matumizi mbalimbali mabaya ya fedha za umma.
Ni muhimu chama chetu kihakikishe kuwa jambo hilo la hati chafu halijirudii ndani ya chama na kwenye Halmashauri katika mwaka wa fedha wa 2016/17 na kuendelea. Ni muhimu tuonyeshe mfano kwa kuongoza kwa ufanisi, uwazi na uadilifu (kwa kuhakikisha Sera zetu za Kijamaa zinaleta Uchumi Shirikishi unaongeza Ajira, kunakuwa na huduma bora za kijamii za maji, afya na elimu, na kuwa watu wetu wanakuwa na akiba kwa kuwaingiza kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na hivyo kuboresha uwezo wa o wa kiuchumi).
Uongozi wetu mzuri katika eneo dogo tulilopewa dhamana sasa inapaswa kuwa ndio shabaha ili iutupe uhalali wa kuomba ridhaa ya kuongoza eneo kubwa zaidi mwaka 2020.
5.     Athari za Yote Haya Kisiasa: Umaarufu wa Serikali Dhidi ya Ukuaji wa Chama
Kuna mabadiliko kiasi kwenye hili tangu miezi 6 iliyopita (Kamati Kuu ya Septemba 5, 2016) nilipowasilisha waraka juu ya hali ya kisiasa nchini. Nilieleza kuwa juu ya matendo yote kidikteta ya serikali ya awamu ya tano, bado imani ya wananchi kwa serikali na kwa rais Magufuli ilikuwa kubwa mno (ukubalikaji wa Rais Magufuli ulikuwa ni kwa 94% ya Wananchi wote waliohojiwa). Propaganda ya Serikali juu ya maendeleo (pamoja na husda iliyozalishwa kutokana na utumbuaji majipu) iliwaingia sana wananchi na kuamsha matumaini yao.
Hali hiyo ilikuwa kikwazo mno kwetu kuikosoa Serikali, ilifanya kazi yetu ya kutoa sera mbadala iwe ngumu mno kueleweka kwa wananchi kwa kuwa matumaini yao kwa serikali yalikuwa makubwa mno. Fursa iliyoko kwetu ni kuwa hali hiyo haipo sasa, utafiti wa mwisho (uliofanyika disemba 2016 – Januari 2017) wa taasisi hiyo hiyo iliyoonyesha Rais Magufuli anakubalika kwa 96% (Juni 2016) uilonyesha kuwa umaarufu wake umeshuka kwa zaidi ya 18% - mpaka 76% (Januari 2017).
Lakini ushukaji wake huo haukuvisaidia vyama vya upinzani pia, mfano Chadema umaarufu wao ulishuka pia kwa zaidi ya nusu, kutoka 32% (Juni 2016) mpaka 16% (Januri 2017), halikadhalika CUF na UKAWA kwa ujumla. Jambo hilo linaonyesha kuwa wananchi pamoja na kuanza kuichukia serikali lakini pia wamepoteza matumaini na siasa, maana umaarufu wa vyama vyote vikuu vya siasa nchini unashuka.
Sisi ACT tumepata faida ndogo, ukuaji wa ufuasi wetu ulipanda kwa asilimia 1, kutoka 1% (Juni 2016) mpaka 2% (Januari 2017), upandaji huo wa ufuasi na kupendwa si mkubwa, lakini ni jambo la kujipongeza sana. Wakati wa tathmini na utengenezaji wa mpango mkakati wa chama (Januari 2016) changamoto kubwa ambayo tuliazimia kuikabili ilikuwa ni ‘Uwepo’ (Visibility) zaidi kabla ya Ufuasi, kwenye hili la ‘Visbility’ mafanikio yetu si mabaya, changamoto yetu ni kuongeza Ufuasi.
Chaguzi ndogo mbalimbali za Serikali za Mitaa zinaonyesha bado lipo tatizo la uwepo wetu, maana hatukushiriki kabisa kwenye chaguzi ndogo za Serikali za Mitaa za Lindi Mjini, Uyui mkoani Tabora na hata Kawe jijini Dar es salaam. Tuna wajibu wa kuhakikisha tunatatua hiyo changamoto ya uwepo wetu. Kushiriki chaguzi hizi ni kuonyesha uwepo wetu. Imani yangu ni kuwa tunayo fursa ya kufanya vizuri zaidi katika kuwafikia watanzania wengi zaidi ili kupanua wigo wa wafuasi, kuongeza uwepo (visibility) yetu na kupanua nafasi yetu katika ushiriki wa siasa nchini.
6.     Mitandao ya Kijamii: Njia Mbadala ya Uenezi wa Chama
Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma imefanya kazi nzuri sana katika miezi hii 6 tangu Kikao cha Kamati Kuu cha Septemba 5, 2016. Kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari (Magazeti na Televisheni) vya nchi yetu vimehodhiwa na vyama vikuu nchini (hasa CCM na Chadema), hivyo kuifanya kazi ya kutangaza uwepo wetu kuwa ngumu mno.
Hivyo kamati ilijitahidi kujikita katika usambazaji wa kazi na taarifa za chama kupitia mitandao ya Kijamii, zaidi Facebook (ambapo makadirio ni uwepo wa Watanzania zaidi ya milioni 4 kwenye mtandao huu wa Kijamii – Ikikadiriwa watafikia milioni 7 - 8 mwaka 2020), naweza kusema kwa dhahiri kuwa ACT Wazalendo ndio chama kinachofanya uenezi zaidi kuliko vyama vyote kwenye Mitandao ya Kijamii, hili ni jambo zuri sana, linapaswa kuendelezwa maana imeongeza mno Visibility ya chama.
Pamoja na mafanikio hayo, zipo changamoto kwenye njia hii ya uenezi wa chama. Kwanza wananchi wengi wa vijijini hawapo huku, pili mafukara na masikini wengi hawapo huku. Hivyo ni muhimu kujua kuwa huku kwenye mitandao ya kijamii sehemu kubwa ya wananchi tunaowafikia ni tabaka la kati na wananchi wa mjini ambao ni theluthi moja tu ya wapigakura wote nchini.
Changamoto nyengine kuu ni kuwa Viongozi wetu wengi wa chama hawajajikita kwenye njia hii ya uenezi wa chama, wao wanaamini zaidi kwenye njia za asili za uenezi (Mikutano ya hadhara) ambazo zimezuiwa na serikali. Changamoto ya mwisho ni kuwa njia hii ya mitandao ya Kijamii ina gharama kiasi, hasa kifedha, ili kufikia watu wengi zaidi njia hii inahitaji udhamini wa matangazo (sponsorship) ambao kwa mwezi si chini ya dola 200 (wastani wa shilingi laki 5).
Pamoja na njia hiyo, Utafiti unaonyesha njia kuu ya kuwafikia watanzania wengi zaidi (hasa mafukara, masikini na waishio vijijini) ni kupitia redio, mitandao ya Kijamii ni njia ya pili ya kuwafikia watanzania wengi zaidi na si njia kuu. Njia kuu ni redio (hasa redio za Kijamii zilizoko katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini).
Hivyo basi, ni muhimu Kamati yetu ya Uenezi kulitazama hili kwa undani, na kujitahidi kuja na mpango mkakati mzuri zaidi kuhakikisha tunazitumia zaidi redio nchini katika uenezi wa chama ili kuhakikisha tunalifikia kila kundi la Watanzania. Pamoja na hatua zote hizo, ni muhimu sana kupanua nguvu yetu katika Magazeti na televisheni mbalimbali nchini..
7.     Tathmini Juu ya Mwongozo wa Msingi wa Maamuzi Mbalimbali ya Chama
Tunapaswa kujitathmini upya kwa lengo la kuwa na njia nzuri ya kufanya maamuzi kwenye utendaji wa chama, tathmini husika itasaidia kutoa muongozo wa namna ya kuenenda katika kufikia maamuzi mbalimbali ya chama katika ngazi zote za uongozi wa Chama. Tathmini hii itatusaidi kuweka msingi na kuepusha sintofahamu katika masuala yote yatakayohitaji muongozo wa chama katika ufikiaji wa maamuzi yake. Napendekeza tathmini husika ijikite kwenye makundi matatu yafuatayo:
Ni masuala gani tunayasimamia bila soni kwa maslahi ya umma hata kama ni ya Serikali?
Masuala yote ambayo yana faida kwa jamii ambayo yanafanywa na Serikali basi tutakuwa nayo pamoja. Kwa mfano yafuatayo:
       I.            Masuala yote yanayohusu kusimamia Uwajibikaji wa Viongozi na kupinga Rushwa na Ufisadi: Jambo hili tunapaswa kuwa pamoja na Serikali, japo ni muhimu kuhakikisha Uimara wa Taasisi za Kidemokrasia na kiuwajibikaji Kama Bunge, Vyama vya Siasa, Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa (NAOT), TAKUKURU, Sekretariat ya Maadili ya Viongozi nk LAZIMA viwe Ni ajenda zetu za kudumu hata kama Serikali nayo itasimamia mambo hayo.
   II.            Miradi mikubwa ya Maendeleo ya Nchi na Wananchi: Ni Masuala ambayo hatupaswi kuona soni kuyasimamia hata kama watawala wanayasemea pia. Wajibu wetu Kama chama cha upinzani utakuwa ni kuhakikisha mambo hayo yanafanyika bila chembe ya Ufisadi hata kama ni Ufisadi unaofanywa na Ikulu au walio Karibu na Ikulu. Mathalani - Serikali imenunua Ndege mpya za ATCL, nii jambo la kupongezwa. Lakini ndege hizi zimelipiwa bei ya ndege mpya wakati inasemekana ni ndege zenye tatizo na wenzetu waliuziwa kwa bei ya chini zaidi. Hili lazima tuhoji na kupata majibu ya Serikali. Miradi mikubwa kama ya SGR, ni muhimu tuhakikishe inafanyika kwa ufanisi na bila ufisadi, kwa kusaidia hata ushauri wa njia mbadala za kupata fedha za utekelezaji wake, kushauri njia bora za utekelezwaji wake ili mradi husika uzalishe faida kwa haraka nk.
III.            Utu na Udugu wa Kitanzania: Imani yetu ni kuwa Watanzania wote ni wamoja, vyama vya siasa ni njia tu za kuifikia Tanzanianjema zaidi.
Masuala gani tunaungana mkono na Wapinzani wenzetu kwa ajili ya kuimarisha taswira yetu kama Upinzani?
Masuala yote ambayo yana faida kwa jamii ambayo yanaminywa na Serikali basi tutakuwa pamoja na wenzetu wa Upinzani kuyapigania. Kwa mfano masuala yafuatayo:
       I.            Uhuru wa Bunge: kuendesha mambo yake bila kuingiliwa lazima iwe Wajibu wetu MKUBWA.
   II.            Uhuru wa Mahakama: kuendesha mambo yake bila kuingiliwa lazima iwe Wajibu wetu MKUBWA.
III.            Utawala wa Sheria na Katiba: Ni dhahiri ni lazima kuungana na vyama vingine vya Upinzani kuhakikisha tunalinda Uhuru wa kufanya siasa, habari na mikusanyiko kama maandamano. Hizi ni Haki za Kikatiba  na Kisheria. Chama hakiwezi kukaa pembeni na kuacha wenzetu wakipigania haki hizi peke yao na kusubiri matokeo. Hatuwezi kuwa ‘Free Riders!’ (kuwepo wakati wa mafanikio tu wakati hatutaki kupambana kuondoa vikwazo vya kidemokrasia). Hata hivyo Ni muhimu sana kutumia njia za kikatiba na kisheria kudai haki hizi huku tukihakikisha Amani na utulivu wa Nchi unatamalaki.
IV.            Kupigania Uimara wa taasisi za Uwajibikaji na za Kidemokrasia: kama Bunge, Vyama vya Siasa, Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa (NAOT), TAKUKURU, Sekretariat ya Maadili ya Viongozi nk. Hili LAZIMA liwe Ni ajenda yetu za kudumu kwa kuhakikisha tunashirikiana na wapinzani wenzetu kuibana serikali.
    V.            Uhuru wa kujiendesha wa Serikali za Mitaa na Halmashauri: Dhidi ya matishio yoyote ya kiuchumi, kisheria na kidemokrasia kutoka serikali kuu.
VI.            Uhuru wa Vyama vya Siasa: Mfano Katazo dhidi ya Mikutano ya hadhara, maandamano nk.
VII.            Uhuru wa Habari: Kwa mfano vitisho dhidi ya wanahabari, wamiliki wa vyombo vya habari na ufunguajia wa vyombo vya habari.
VIII.            Uhuru wa Kujieleza: Tishio dhidi ya Uhuru wa kujieleza nchini liko dhahiri kabisa, kwenye suala hili tutasimama na wenzetu wote wa upinzani katika kuhakikisha tunapigania haki ya watanzania kujieleza kwa uhuru bila vitisho kwa kupiganiwa kufutwa kwa sheria mbalimbali mbaya ambazo ni kikwazo dhidi ya uhuru huo.
IX.            Ushirikiano katika chaguzi mbalimbali kwa kadiri haja itakavyojitokeza.

Ni masuala gani hatusimami na mtu kwa sababu ya kusimamia misingi ya chama chetu?
Masuala yote ya Kisera na Kiitikadi ya chama tutapaswa kuyasimamia hata kama tutabaki peke yetu kwenye kuyasimami. Kwa mfano masuala yafuatayo:
       I.            Muungano na Umajumui wa Afrika: Hususan Utangamano wa Afrika Mashariki ni moja ya Msingi wa Chama chetu. Uimara wa Muungano wetu wa Tanzania na umuhimu wa Afrika kuwa moja, ni mambo ambayo hata tukibaki peke yetu lazima tuendelee kuyasemea.
   II.            Uzalendo na Nafasi ya Nchi yetu Kimataifa: Kanuni kuu ya Kizalendo ni ‘wrong or right, my country first’. Tukishindwa kusimamia hili basi tunapaswa kukaa kimya tu kwenye jambo husika bila kutoa kauli ambayo itaathiri Taifa.
III.            Sera za Kijamaa katika masuala ya Kimataifa ya Kiuchumi na Kikodi: kama vile kubana mianya ya kikodi kwa makampuni makubwa ya Kimataifa, kuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kupambana na uhamishaji wa mitaji kutoka nchi masikini.
IV.            Hifadhi ya Jamii ili kuongeza uwezo wa kuweka akiba na kuongeza mtaji wa ndani katika uwekezaji nchini.
    V.            Sera za Kijamaa juu ya Masuala ya Kilimo: Kusimamia Fao la Bei, huduma za Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima, Uhakika wa Ruzuku ya Mbolea, Viwanda vya Kuongeza thamani ya Mazao ya Kilimo (Agro-processing Industires), na masuala ya masoko ili kuinua kipato cha wakulima.
VI.            Ushirikishwaji wa wananchi wenyewe katika Uvunwaji wa rasilimali za nchi (hasa madini, mafuta na gesi asilia) na pia Matumizi ya mapato yatokanayo na Uvunwaji husika.
VII.            Kupigania Uchumi – Shirikishi na wa Kijamaa unaozalisha ajira kama ilivyoainishwa kwenye azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha.
VIII.            Azimio la Tabora: Hili ni tamko la Kisera na Kiitikadi la Chama, jambo lolote la kisera na kiitikadi lililoainishwa kwenye Azimio la Tabora tutapaswa kulisimamia.
8.     Hitimisho 
Naomba Kamati Kuu ya Chama inayokutana leo hii hapa mjini Kahama katika maazimisho haya ya miaka mitatu ya chama chetu itafakari kwa kina juu ya Hali ya Siasa nchini na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukuliwa na Chama.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (Mbunge)
Kiongozi wa Chama – ACT Wazalendo
Kahama – Shinyanga
Mei 7, 2017


No comments: